2017-04-01 11:09:00

Prof. Anne-Marie Pelletier kutunga tafakari ya Njia ya Msalaba, 2017


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Professa Anne-Marie Pelletier kuandaa Tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo, Roma, Ijumaa kuu tarehe 14 Aprili 2017. Mama Pelletier ni mtaalam na jaalim wa Sayansi ya Maandiko Matakatifu kutoka Ufaransa na hivi karibuni amekuwa mshindi wa Tuzo ya Mfuko wa Joseph Ratzinger, Papa Benedikto XVI kwa Mwaka 2014. Huyu ni mwanamke wa kwanza kuwahi kupewa tuzo la Joseph Ratzinger na ni mchangiaji mkubwa katika makala ya wanawake kimataifa!

Professa Anne-Marie Pelletie ni kati ya waamini makini wa Kanisa Katoliki nchini Ufaransa ambaye amejipambanua kwa kuwa mstari wa mbele katika kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wanawake ndani na nje ya Kanisa. Alizaliwa tarehe 13 juni 1946 huko Paris, Ufaransa. Ameolewa na amebahatika kupata watoto watatu. Kunako mwaka 1986 alitunukiwa Shahada ya Uzamivu katika Sayansi ya Dini. Tangu Mwaka 1969 hadi 1998 amekuwa akifundisha Sayansi ya Maandiko Matakatifu katika Vyuo vikuu mbali mbali hasa masomo ya: Fasihi, Taalimungu ya maisha ya ndoa; Sayansi ya Maandiko Matakatifu, Biblia na Liturujia; Tafsiri makini ya Maandiko Matakatifu.

Professa Anne-Marie Pelletie pamoja na mambo mengine anajihusisha na tafiti mbali mbali kuhusiana na utu wa binadamu mintarafu Mafundisho ya Kikristo; amekuwa pia ni mwezeshaji mzuri katika mafungo ya maisha ya kiroho, sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, ni mwandishi mahiri wa vitabu na mchangiaji mkubwa katika majarida mbali mbali ya kitaifa na kimataifa. Ni mtaalam pia wa majadiliano kati ya Wakatoliki na Wayahudi. Huyu ndiye ambaye Baba Mtakatifu Francisko amemkabidhi kuandaa Tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo, Ijumaa kuu, tarehe 14 Aprili 2017.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.