2017-03-31 14:49:00

Roho Mtakatifu anawawezesha waamini kulifahamu Fumbo la Ufufuko


Padre Raniero Cantalamessa mhubiri wa nyumba ya kipapa anasema, kauli mbiu inayoongoza tafakari za kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2017 ni “Hawezi mtu kusema Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu”. (Rej. 1 Kor. 12: 3). Ni Roho Mtakatifu anayesaidia kuwaingiza waamini katika Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Ufufuko wa Yesu ni tukio ambalo linaweza kuchambuliwa kihistoria; Pili, katika mwelekeo wa kulitetea Fumbo la Ufufuko na mwishoni maana ya Fumbo la Ufufuko wa Yesu kutoka kwa wafu!

Haya ndiyo mawazo makuu yaliyojitokeza kwenye mahubiri yaliyotolewa na Padre Cantalamessa, Ijumaa tarehe 31 Machi 2017 mbele ya Baba Mtakatifu Francisko, waandamizi wakuu kutoka Vatican pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume waliopo mjini Roma. Itakumbukwa kwamba, Roho Mtakatifu ndiye anayewawezesha waamini kufahamu ukweli kuhusu Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, yaani Kristo Yesu na kumwabudu kama Bwana na Mungu kweli. Ni kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, ameweza kuwakomboa binadamu kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti.

Fumbo la Ufufuko wa Kristo ni kazi ya Roho Mtakatifu kama anavyosema Mtakatifu Paulo kwamba, amedhihirishwa kwa uweza kuwa Mwana wa Mungu, kwa jinsi ya roho ya utakatifu, kwa ufufuo wa wafu. Huu ni utimilifu wa unabii uliotolewa kwenye Agano la Kale kwa kinywa cha Nabii Ezekieli anayeonesha jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu kwa uweza wake aliwafufua umati mkubwa wa watu na kuwajalia maisha na matumaini.

Padre Cantalamessa anakaza kusema, Fumbo la Ufufuko wa Kristo ni tukio la kihistoria linalotangazwa na kushuhudiwa na Kanisa kuwa ni kilele cha ukweli wa imani ya Kanisa katika Kristo baada ya wafuasi wake kuingia katika giza la kashfa ya Fumbo la Msalaba, ikaonekana kana kwamba, walikuwa wamekufa kiimani na Yesu, maisha na utume wake vilikuwa vimezikwa pamoja naye. Kumbe, Kanisa linatangaza na kushuhudia kwamba, Yesu aliyeteswa na kufa Msalabani amefufuka kutoka kwa wafu. Yeye ndiye lile jiwe walilolikataa waashi lakini sasa limekuwa jiwe kuu la pembeni. Kristo Yesu ndiye mkombozi wa dunia.

Imani kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu iliwawezesha mitume na wakristo wa kwanza kusimama kidete katika imani, kiasi hata cha kukubali kuteswa, kunyanyaswa na hata kuuwawa. Hawakuona Yesu anafufuka, lakini walikutana na Kristo Mfufuka aliyewatokea kwa nyakati mbali mbali. Yesu aliteswa, akafa na kufufuka wakati wa utawala wa Pontio Pilato. Ufufuko wa Kristo ni amana, urithi na kiini cha Imani ya Fumbo la Pasaka, lililoshuhudiwa na kutangazwa na Wafuasi wa Kristo. Tukio hili la kihistoria halina budi kutazamwa kwa mwanga wa imani.

Padre Cantalamessa anasema, Agano Jipya na Liturujia ya Kanisa vina mwelekeo wa kulitetea na kuenzi Fumbo la Ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu kwa kuwa ni sehemu ya imani ya Kanisa. Paulo mtume anakaza kwa kusema kwa maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule waliyemchagua; naye amewapa wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu! Hii ni “Ndiyo” ya Mungu mintarafu maisha ya Mwanaye Mpendwa Kristo Yesu. Ufufuko wa Kristo ni Fumbo linalofafanua maisha na utume wa Kristo Yesu wa kuwakomboa watu kutoka katika lindi la dhambi na mauti sanjari na kuwajalia fadhila ya matumaini katika ufufuo wa wafu kwa njia ya Roho Mtakatifu.

Tukio hili linadhihirisha ukuu wa Mungu unaoshuhudiwa katika maisha ya watakatifu wake, kwani ni Mungu wa wazima na wala si Mungu wa wafu! Fumbo la Ufufuko ni kiini cha ufufuko wa miili na maisha ya uzima wa milele kwani wao wamefanyika kuwa kweli ni watoto wapendwa wa Mungu. Mwenyezi Mungu ni wa milele na kwa njia ya Fumbo la Ufufuko wa Kristo, waamini wanaweza kuonja: utukufu na umilele wa Kristo. Mtume Paulo anasema mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu, mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao! Padre Raniero Cantalamessa anahitimisha mahubiri yake kwa kusema, utamu wa ngoma ni kuicheza mwenyewe! Tafakari hii iwe ni cheche ya kutamani kuingia katika maisha ya uzima wa milele!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.