2017-03-31 15:07:00

Mkutano wa Kimataifa kuhusu "Maendeleo ya watu"


Baraza la Kipapa la huduma ya maendeleo endelevu ya binadamu kuanzia tarehe 3 – 4 Aprili, 2017 litaadhimisha Mkutano wa Kimataifa kuhusu Miaka 50 tangu Waraka wa Kitume wa Mwenyeheri Paulo VI “Populorum progressio” yaani “Maendeleo ya watu” ulipochapishwa rasmi. Lengo la mkutano huu ni kufanya upembuzi yakinifu kuhusu misingi ya kitaalimungu, kiutu na kichungaji inayofumbatwa katika Waraka huu mintarafu uhusiano wake na wale wanaotekeleza dhamana na wajibu wao katika ustawi na maendeleo ya binadamu.

Lengo ni kuibua mbinu mkakati wa sera na shughuli za Baraza la Kipapa la huduma ya maendeleo endelevu ya binadamu ambalo limeundwa mwaka 2017 kama sehemu ya mageuzi yanayofanywa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Mkutano huu utawahusisha kwa namna ya pekee wajumbe wa Mabaraza manne ya Kipapa yaliyounganishwa na kuundwa Baraza hili jipya; wawakilishi kutoka katika Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia; Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki kitaifa na kimataifa pamoja na wanadiplomasia wanaowakilisha nchi na Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican.

Taarifa inaonesha kwamba, wawezeshaji wakuu ni pamoja na Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la huduma ya maendeleo endelevu ya binadamu atakayepembua mwelekeo wa kitaalimungu na utu wa mwanadamu. Kardinali Gerhard Ludwig Muller, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa atajikita katika mambo msingi ya maisha ya binadamu: kiroho na kimwili; uhusiano kati ya mwanamke na mwanaume; mtu na jamii. Kutakuwepo pia mchango utakaotolewa na mabingwa katika sekta mbali mbali za Baraza hili bila kusahau ushuhuda wa Kanisa katika huduma kwa maskini.

Maadhimisho haya yatazinduliwa kwa Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumatatu, tarehe 3 Aprili 2017 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 4 Aprili 2017 anatarajiwa kukutana na kuzungumza na washiriki wa mkutano huu kama sehemu ya maadhimisho ya Miaka 50 tangu Mwenyeheri Paulo VI alipochapisha Waraka wake wa Kitume “Populorum progressio” yaani “Maendeleo ya watu”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.