2017-03-31 09:47:00

Familia ni Habari Njema kwa walimwengu!


Baba Mtakatifu Francisko anasema, familia bado inaendelea kuwa ni Habari Njema kwa walimwengu, kumbe waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya familia katika ulimwengu mamboleo. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Kardinali Kevin Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, Alhamisi tarehe 30 Machi 2017 wakati wa kuzindua maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya IX ya Familia Duniani itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Dublin, nchini Ireland kuanzia tarehe 22- 26 Agosti 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Injili ya familia: furaha ya ulimwengu”.

Maandalizi haya yanaongozwa kwa namna ya pekee kabisa na Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Injili ya Kristo ni chemchemi inayowapatia wanafamilia ari, nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia Injili kwa watu wa nyakati hizi. Lakini, ikumbukwe kwamba, Neno la Mungu lina makali kuwili; hata familia zinaweza kuwa ni chemchemi ya furaha na upendo wa dhati unaobubujika kutoka kwenye huruma ya upendo wa Mungu. Lakini pia, familia zisipokuwa makini kuweza kuwa ni mahali pa patashika nguo kuchanika.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu umewakumbusha waamini kwa namna ya pekee kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, tayari kuumwilisha katika uhalisia wa maisha! Kumbe, maadhimisho ya Siku ya IX ya Familia Duniani kwa Mwaka 2018. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maadhimisho haya yatakuwa ni fursa makini ya kuzamisha zaidi tafakari kuhusu Injili ya familia kwa kuongozwa na Wosia wa Kitume; Furaha ya upendo ndani ya familia ambao kwa sasa ni dira na mwongozo wa utume wa familia dunia.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Diarmuid Martin wa Jimbo kuu la Dublin anasema, maadhimisho ya Siku ya IX ya Familia Duniani ni fursa makini ya kutangaza na kushudia Injili ya familia na wala si kipindi cha mpito mintarafu maisha ya familia. NI wakati ambapo waamini wote wanahamasishwa kufanya tafakari ya kina kuhusu Injili ya familia kwa mwanga wa Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: Furaha ya upendo ndani ya familia. Ni mwaliko wa kumwilisha wosia huu katika uhalisia wa maisha ya kifamilia, ili kuweza kulipyaisha Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Askofu mkuu Martin anasema, Jumuiya za Kikristo zinapaswa kuwa ni mahali ambapo wanafamilia wanajisikia kupokelewa, kupendwa na kusaidiwa kukua na kukomaa katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na wala si mahaka ya kuwahukumu wale walioteleza, wakashindwa na kuanguka katika maisha ya ndoa na familia. Jumuiya za Kikristo ziwe ni mahali pa kushirikishana uzoefu na mang’amuzi ya maisha ya ndoa na familia, tayari kusimamia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia mintarafu Mafundisho ya Kanisa. Maadhimisho ya Siku ya IX ya Familia Duniani huko Dublin, yatajikita zaidi katika katekesi kuhusu maana ya upendo katika maisha ya ndoa na familia; dhamana, wito na wajibu wa familia ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Ni wakati muafaka wa kulipyaisha Kanisa nchini Ireland kwa ushiriki mkamilifu wa waamini walei ili kujenga tena matumaini yao katika maisha ya ndoa na familia bila kusahau utume wao ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.