2017-03-30 16:48:00

Papa Francisko: Nendeni mkagange na kuponya majereha ya binadamu!


Shirika la Wamissionari wa Somaschi kuanzia tarehe 14 Machi hadi tarehe 1 Aprili 2017 linaadhimisha Mkutano wake mkuu wa 138 tangu kuanzishwa kwake. Mkutano unaongozwa na kauli mbiu “Tuvuke ng’ambo ya pili ya Ziwa pamoja na ndugu zetu ambao tunakata kuishi na kufa kwa ajili yao”. Haya ni maneno ambayo yanachota utajiri wa historia ya Shirika unaofumbata tunu ya kinabii. Kunako mwaka 1921 Shirika hili lilivuka mabonde na milima kutoka Ulaya na kuelekea Amerika na huo ukawa ni mwanzo wa utume wa kimissionari uliofumbatwa na familia hii ya kitawa!

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 30 Machi 2017 amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirika la Somaschi na kuwataka kujikita katika mchakato wa Uinjilishaji mpya kwa kuendelea kuwa waaminifu kwa karama ya mwanzilishi wa Shirika lao sanjari na kusoma alama za nyakati, daima wakiendelea kumwilisha matunda ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Wasomaschi iliyoadhimishwa kuanzia mwaka 2011 hadi mwaka 2012. Wakati huo, Papa Mstaafu Benedikto XVI aliwataka kufuata mfano bora wa Mtakatifu Jerome Emiliani, kwa kuambata umaskini wa vijana wa kizazi kipya; kimaadili, kimwili, kimaisha, lakini zaidi umaskini wa upendo ambao ni kiini cha matatizo makuu yanayomsibu binadamu!

Mtakatifu Emiliani alishiriki katika mchakato wa kulipyaisha Kanisa kwa njia ya matendo ya huruma, kwa kuendelea kuwa mwaminifu katika Injili, Jumuiya ya Kikristo na Kijamii, kwa kuwasaidia watoto wadogo na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kuwaonjesha maendeleo endelevu ya binadamu! Baba Mtakatifu anataka wanashirika hawa kutoka kifua mbele kuwaendea wale watu waliojeruhiwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii kwa kutumia jicho angavu na pendelevu la Kristo Yesu!

Wajisadake kwa ajili ya kuwahudumia maskini, watoto yatima, vijana wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi na kwamba, mfumo wao wa elimu ujikite katika ustawi wa binadamu! Wawe na upendeleo kwa wakimbizi na wahamiaji; watoto yatima wanaoteseka kwa kukosa wazazi na walezi, hawa wote wanahitaji huruma na upendo wao! Wamissionari hawa waendelee kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kati pamoja na watu! Wathubutu kusoma alama za nyakati kwa kuondokana na miundo mbinu inayowakwamisha katika mchakato wa huduma ya upendo na kwa ajili ya ujenzi wa ufalme wa Mungu.

Watoe kipaumbele cha kwanza kwa Fumbo la Utatu Mtakatifu, ili kwamba, wema, upendo na huruma ya Mungu iweze kuwagusa katika maisha ya kidugu na utume wao! Wawe tayari kuwashirikisha waamini walei karama ya Shirika lao, tayari kusimama kidete kusaidia shughuli za huduma na maendeleo ya kijamii; kwa kutetea haki msingi za binadamu; haki za watoto na vijana; kwa kuwalinda ili wasitumbukizwe kwenye unyonyaji, ili waweze kukombolewa kwa nguvu ya Injili ya Kristo na kuwawezesha kupata ujuzi na maarifa.

Mtakatifu Elimiani aliishi nyakati za Mageuzi ya Kiluteri Duniani, aliteseka sana kuona Kanisa linameguka, ndiyo maana akaamua kujikita katika mageuzi ya Kanisa kwa kuambata matendo ya huruma, Utii kwa viongozi wa Kanisa na kuendelea kulitafakari Fumbo la Msalaba, chemchemi ya huruma ya Mungu; akakazia Katekesi; Uaminifu katika Sakramenti za Kanisa na hasa zaidi katika Ibada ya Ekaristi Takatifu sanjari na upendo kwa Bikira Maria. Akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, akajikita katika mchakato wa utamadunisho, changamoto na mwaliko wa kuendelea kuwafunda makatekista, waamini walei na wakleri; huku wote wakishirikiana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa mahalia.

Baba Mtakatifu anawataka wawe mstari wa mbele katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene. Watambue pia kwamba, Mtakatifu Emiliani alitangazwa na Papa XI kuwa msimamizi wa watoto yatima na vijana waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi, changamoto kubwa kwa sasa ni kuendelea kuboresha elimu kwa vijana ili waweze kuwa imara katika imani, huru katika kufikiri na kutenda; wawajibikaji, mashujaa na wakarimu katika huduma. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawatakia heri na baraka katika mchakato mzima wa Uinjilishaji ndani ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.