2017-03-30 17:07:00

Papa Francisko: katika sakafu ya moyo wa binadamu kuna chembe ya uasi


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake Alhamisi, tarehe 30 Machi 2017 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu anawapenda kwa upendo wa kweli kama Baba, kumbe, wanapaswa kuondokana na mambo yote yanayowatumbukiza katika utumwa. Mwenyezi Mungu katika Agano la Kale alionesha upendo usiokuwa na kikomo kwa watu wake licha ya Waisraeli kukengeuka na kumwasi mara kwa mara.

Hii ni changamoto hata leo hii kwa waamini kujiuliza ikiwa kama wanakengeuka na kumwasi Mungu ili kuambatana na miungu wa uwongo. Mwenyezi Mungu alikuwa na ndoto ya upendo kwa watu wake, lakini ikasalitiwa kutokana na Waisraeli kujitengenezea ndama wa shaba na kujiaminisha kwamba, huyu ndiye aliyekuwa mungu wao aliyewakomboa kutoka utumwamini Misri. Ni watu alioshindwa kuvumilia walau hata kwa siku 40 ambazo Musa alikuwa mbele ya Mwenyezi Mungu ili kupokea Amri za Mungu. Wakamsahau Mungu aliyewaokoa kwa mkono wa nguvu na kuanza kumwabudu ndama waliyemtengeneza kwa mikono yao.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, katika sakafu ya moyo wa mwanadamu daima kuna kishawishi cha kutaka kukengeuka na kumwasi Mwenyezi Mungu, kukimbia mbali na upendo wake aminifu. Watu wanataka kuabudu ndama wa kuchongwa; kwa kumezwa na malimwengu, kiasi hata cha kumsahau Mwenyezi Mungu. Lakini, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo, ndiyo maana anajitaabisha kuwatafuta watu wake ili waweze kutubu na kumwongokea. Ndiyo maana hata Yesu aliulilia mji wa Yerusalemu. Kumbe, waamini wanahamasishwa na Baba Mtakatifu Francisko kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwapatia neema na baraka ya kuondokana na kishawishi na kukengeuka na uasi; ili wawe tayari kuutafuta upendo wa Mungu na kuuambata katika maisha yao. Hii ni dhamana inayopaswa kutekelezwa kila siku ya maisha, ili kurejea tena mbele ya uso wa Mungu, kwani daima anawasubiri wanapomwendea kwa moyo wa toba na wongofu wa ndani kama alivyofanya Baba mwenye huruma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.