2017-03-30 11:30:00

Brexit! Kardinali Nichols hakuna nchi inayoweza kuishi kama kisiwa!


Serikali ya Uingereza tarehe 30 Machi 2017 imeanzisha rasmi mchakato wa kujiengua kutoka kwenye Umoja wa Ulaya kadiri ya Ibara ya 50 ya Mkataba wa Lisbon, tukio ambalo limewahuzunisha wananchi wengi ndani na nje ya Umoja wa Ulaya. Mchakato huu unatarajiwa kuhitimishwa hapo tarehe 29 Machi 2019. Kumbe bado kuna miaka miwili ya majadiliano kati ya Serikali ya Uingereza na Umoja wa Ulaya Kardinali Vincent Nichols anasema, hakuna nchi ambayo inaweza kuishi peke yake kama kisiwa.

Kuna idadi kubwa ya wananchi wa Uingereza hawakuridhika na uamuzi Uingereza kujitenga kutoka katika Umoja wa Ulaya, lakini ikumbukwe kwamba, kura ya maoni iliwapatia ushindi wale waliokuwa wanataka kujitengea kutoka katika Umoja wa Ulaya, kumbe haya ni maamuzi ya kidemokrasia ambayo yanapaswa kuheshimiwa, hata kama wananchi wengi kwa sasa ndio wamegundua athari zake katika maisha yao, mwanzoni wengi walidhani ni jambo la mzaha tu! Mabadiliko ya kiuchumi na kifedha ni mambo msingi yaliyozingatiwa na Uingereza katika maamuzi yake ya kujiengua kutoka Umoja wa Ulaya. Kwa sasa kumeibuka tena cheche za Ireland ya Kaskazini kutaka kujitenga na Uingereza, hali ambayo itadhohofisha umoja na mshikamano wa kitaifa. Kardinali Nichols anasema, kuna uhusiano wa karibu kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya; uhusiano ambao umejengeka katika misingi ya utamaduni, imani na mapokeo pamoja na ushuhuda! Kuna haja ya kushikamana na nchi nyingine duniani katika mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi, ukosefu wa fursa za ajira kwa vijana pamoja na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Kardinali Nichols anakaza kusema, majadiliano kati ya waamini wa dini na madhehebu mbali mbali ni muhimu sana katika kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano kati ya watu. Majadiliano haya yanaweza kusaidia mchakato wa kipambana na  vitendo vya kigaidi kwa kujenga na kuimarisha jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, amani na maridhiano, bila watu kutengwa kutokana na imani, tamaduni au mahali wanapotoka! Kanisa litaendelea kujenga na kuimarisha madaraja ya watu wa dini na imani mbali mbali kukutana, ili kuimarisha udugu, upendo na mshikamano. Ubaguzi wa aina yoyote ile ni hatari kwa maisha na mafungamano ya kijamii. Watu wajenge na kudumisha utamaduni wa upendo na mshikamano; kwa kuheshimiana na kusaidiana kama binadamu. Kardinali Vincent Nichols anasema, watu wana wasi wasi na hofu kuhusu mustakabali wa Uingereza kwa siku za usoni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.