2017-03-29 09:03:00

Familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Carpi, inamsubiri Papa Francisko


Kunako mwaka 2012 tetemeko kubwa la ardhi liliikumba Italia na eneo la Emiglia Romagna likaharibiwa sana na kusababisha watu 28 kupoteza maisha na wengine wengi kupata majeraha na vilema vya kudumu. Miundo mbinu ikaharibiwa sana kiasi cha watu wengi kujikuta hawana tena makazi; shughuli za uzalishaji na huduma zikasimama, watu wakakata tama ya maisha! Askofu Francesco Cavina wa Jimbo la Carpi, Italia anasema, Baba Mtakatifu Francisko anatembelea Jimboni mwake, ili kuwatia shime watu walioguswa na kutikiswa kutokana na majanga asilia, ili kwa imani na matumaini, waweze kusimama tena na kusonga mbele.

Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanataka kumkaribisha na kumkirimia Baba Mtakatifu Francisko atakapowatembelea Jimboni humo hapo tarehe 2 Aprili 2017 kama kielelezo cha upendo na mshikamano na familia ya Mungu Jimboni Carpi na Mirandola. Hili ni Jimbo ambalo halina umaarufu sana nchini Italia, lakini, limebahatika kutembelewa na Papa Mstaafu Benedikto XVI na kwa sasa Papa Francisko anajiandaa kuwatembelea ili kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI amewaandikia ujumbe wa matashi mema akiwakumbuka kwa sala na kwamba, Kanisa kuu lilotabarukiwa hivi karibuni liwe ni kielelezo cha mchakato wa ujenzi wa maisha ya kiroho, ambayo Kristo Yesu ndiye jiwe kuu la msingi!

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican Askofu Francesco Cavina wa Jimbo Katoliki la Carpi anasema, wazo la kutembelea Carpi na Mirandola ni la Baba Mtakatifu Francisko mwenyewe, aliyeonesha utashi wa kutembelea maeneo haya yaliyoathirika kwa majanga asilia kabla ya maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka kwa Mwaka 2017. Hii itakuwa ni nafasi kwa Baba Mtakatifu Francisko kujionea mwenyewe mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu na kile ambacho wamejitahidi kutekeleza katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Kwa namna ya pekee, ni furaha ya ajabu kwa kutabaruku tena Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Carpi, tarehe 25 Machi 2017. Kanisa hili liliharibiwa sana na tetemeko la ardhi, sasa limefunguliwa ili kutoa nafasi kwa waamini kumshukuru Mungu kwa wema, ukarimu na tunza yake ya Kibaba!

Tukio hili la kihistoria lilifanywa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa kuwakumbusha kwamba, Kanisa hili Mama ni mahali pa kuimarisha: imani na matumaini yanayotolewa ushuhuda katika uhalisia wa maisha ya waamini wenyewe. Baba Mtakatifu Francisko anampongeza kwa namna ya pekee Askofu Francesco Cavina kwa ushuhuda wake makini, uliomwezesha kuwa karibu sana na waamini wake wakati wa shida na mahangaiko yao kiasi kwamba, kweli amekuwa ni chemchemi ya matumaini kwao!

Tetemeko la ardhi lilisababisha uhaba mkubwa wa fursa za ajira na familia nyingi zilijikuta hazina makazi ya kudumu, kiasi cha kupatiwa hifadhi kwenye makazi ya muda. Kumbe, ujenzi wa makazi ya watu na miundo mbinu ya huduma za kiroho, kimwili na kijamii kwa sasa imekamilika. Lakini bado kuna changamoto kubwa zinazopaswa kuvaliwa njuga anasema Askofu Francesco Cavina hasa eneo la Mirandola ambako amemwomba Baba Mtakatifu Francisko kutembelea ili kujionea mwenyewe mahangaiko ya watu wake.

Baba Mtakatifu atabariki jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Parokia ya Mtakatifu Agatha, Nyumba ya mafungo ya Mtakatifu Antonio pamoja na ujenzi wa majengo ya huduma ya upendo yatakayotumiwa na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Jimboni Carpi, Caritas. Kanisa kuu la Mirandola lilikuwa limeharibiwa vibaya sana, lakini kutokana na ushirikiano wa wadau mbali mbali, kazi kubwa imefanyika. Ni wakati wa kumshukuru Mungu kwa wema, huruma na upendo wake. Waamini wanajisikia ari ya kutaka kurejea tena katika maeneo ya sala. Askofu Cavina anasema, baada ya kukamilisha ukarabati na kengele kuanza kusikika tena kwa ajili ya kuwaalika waamini kwa sala, siku moja amekutana na mzee mmoja ambaye alimpokea kwa dimbwi la machozi na kukiri kwamba, kabla ya tetemeko la ardhi, kengele za Kanisa zilipokuwa zinagongwa alijisikia kukereka sana!

Lakini, baada ya tetemeko la ardhi kuharibu rasilimali na amana waliyokuwa nayo, sasa anakiri kwamba, tetemeko hili limemletea mabadiliko makubwa katika maisha yake, amekuwa ni mtu mpya anapenda kwenda kusali ili kumshukuru Mungu kwa wema, huruma na tunza yake ya kibaba! Familia ya Mungu Jimboni Carpi ni watu wa kawaida, lakini mahiri kwa sanaa, ndiyo maana wanataka pia kumwonesha Baba Mtakatifu Francisko ukarimu kwa kumkirimia sehemu ya kazi ya mikono yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.