2017-03-28 16:25:00

Sera za kilimo endelevu zitoe kipaumbele cha kwanza kwa binadamu!


Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwatia shime wadau mbali mbali wanaowajibika katika maendeleo ya sekta ya kilimo kuhakikisha kwamba, wanatekeleza vyema dhamana na wajibu wao, ili kuleta maboresho makubwa katika shughuli za kilimo, uzalishaji na biashara; sanjari na kukazia afya bora, lishe ya kutosha kadiri ya mahitaji ya mtu binafsi pamoja na kuzingatia mpango mkakati wa utekelezaji wa maamuzi yaliyokwisha kufikiwa!

Haya yamo kwenye ujumbe wa Baba Mtakatifu ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Bwana Janez Potocnik, Rais wa Jukwaa la Kilimo kwa siku za usoni, wakati wa mkutano wake, uliofanyika mjini Brussels, Ubelgiji, Jumanne, tarehe 28 Machi 2017. Baba Mtakatifu anakaza kusema, shughuli zote za kilimo zinapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu kama: mkulima, wakala wa uchumi au mlaji. Lengo ni kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kilimo na uhusiano wake na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, ukuaji wa uchumi pamoja na mahitaji msingi ya idadi ya watu duniani!

Baba Mtakatifu anasema, matarajio yanayofungamanishwa katika Maendeleo endelevu kwa ajili ya Jumuiya ya Kimataifa yanahitaji kwa kiasi kikubwa maboresho ya shughuli katika sekta ya kilimo sanjari na kujibu changamoto za utunzaji bora wa mazingira na udhibiti wa athari za mabadiliko ya tabianchi. Ukosefu wa ajira, kipato kidogo kwa watu wengi, lishe duni na utapiamlo wa kutisha ni mambo yanayotesa mamilioni ya watu sehemu mbali mbali za dunia. Ni kundi la watu ambalo limeondoshwa kutoka katika mchakato wa uzalishaji na matokeo yake linageuka kuwa ni sehemu ya wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta maisha bora zaidi sehemu mbali mbali za dunia.

Maendeleo ya sekta ya kilimo kwa siku za usoni anasema Baba Mtakatifu Francisko yanategemea kwa kiasi kikubwa mfumo wa uzalishaji unaotosheleza mahitaji ya watu wengi zaidi; kwa kuhakikisha kwamba, walau kila nchi inajitosheleza kwa uzalishaji wa chakula, kwa kuwa na mfumo mpya wa maendeleo na ulaji; kwa kuboresha mifumo inayowajali wakulima wadogo wadogo vijijini sanjari na utunzaji bora wa ekolojia na baianuai. Kuna haja pia ya kuzingatia sera za ushirikiano zitakazowajengea uwezo watu mahalia badala ya kuwatwika mzigo wa utegemezi kutoka nje. Wigo kati ya ukubwa wa changamoto na matatizo pamoja na matokeo yanayokusudiwa isiwe ni sababu ya kukatisha tamaa, wala kukuza utegemezi na badala yake iwe ni fursa ya kuwajengea watu uwajibikaji. Katika majadiliano kwenye Jukwaa la Kilimo, wajumbe wahamasishwe kushirikiana kwani kuna mengi yanayoweza kufanyika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.