2017-03-28 09:05:00

Magonjwa ya moyo tishio la afya kwa watu wengi Barani Afrika!


Taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya Desemba 2016 inaonesha kuwa ugonjwa wa shinikizo la damu ndio ugonjwa ambao unaathiri watu wengi zaidi barani Afrika huku ikionesha asilimia zaidi ya 10 ya Waafrika wameshapata ugonjwa huo. Kwa mujibu ripoti hiyo imeelezwa kuwa sababu kubwa za kuzidi kuongezeka kwa ugonjwa huo kuwa ni watu kutofanya mazoezi, matumizi ya tumbaku au sigara na pombe zimetajwa kama njia kuu za kushindwa kupambana na magonjwa yote yasiyoambukiza ikiwemo Moyo, Kisukari na Saratani. Aidha ripoti hiyo imeonesha pia robo ya watu wazima kutoka nusu ya nchi za Afrika zilizofanyiwa utafiti wameathiriwa na sababu tatu za hatari zinazoongeza uwezekano wa kuwa na moja au zaidi ya magonjwa mengine hatarishi wakati wa maisha yao.

Wakati ambapo matumizi ya tumbaku au sigara na pombe yako kiwango cha chini barani Afrika kuliko sehemu zingine duniani, shinikizo la damu liko katika kiwango cha juu zaidi duniani, na kuathiri karibu nusu ya watu wazima barani Afrika. WHO imeeleza kuwa matatizo haya yanaweza kuzuiwa kwa watu kula vizuri, kunywa kwa kiasi na kufanya mazoezi na endapo tahadhari hizi hazizingatiwi, hali hii inaweza kupelekea kuzigharimu serikali mabilioni ya pesa kwenye matibabu ya wagonjwa wake. Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazojizatiti kudhibiti na kupambana na ugonjwa wa moyo ambao ni miongoni mwa magonjwa tishio kwa watoto wadogo.Inakadiliwa kuwa kati ya watoto 1,000 wanaozaliwa kila siku duniani, wanane miongoni mwao wanazaliwa wakiwa na ugonjwa wa moyo.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya imejipanga kikamilifu katika kukabiliana na magonjwa ya moyo kwa Watanzania.  Daktari bingwa wa Moyo kutoka katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Tulizo Shemu anasema Aidha hospitali hiyo inahudumia wagonjwa wan je zaidi ya 1000 na wagonjwa wanaolazwa 100 kwa wiki. Dkt. Shemu anaongeza kuwa tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo, mambo mbalimbali yameweza kufanyika ikiwemo kupunguza vifo vinavyotokana na maradhi ya moyo kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Anaongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 2017 taasisi hiyo imefanikiwa kuongeza idadi ya wagonjwa wanaohudhuria kliniki ya wagonjwa wa nje kutoka 100 na kufikia 200, hatua inayotokana na mwamko wa wananchi kuwa na uelewa kuhusu magonjwa ya moyo. “Tumepunguza vifo vitokanavyo na maradhi ya moyo kwa kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari ili kuwafanya wananachi kuyafahamu magonjwa ya moyo na jinsi wanavyoweza kuyaepuka na kukabiliana nayo”alisema Dkt. Shemu. Kwa mujibu wa Dkt. Shemu katika kipindi cha mwaka 2016 taasisi hiyo imefanya uchunguzi wa tiba kwa wagonjwa 973, ambapo kati yao wagonjwa 620 walipatiwa matibabu ya moyo bila kufungua kifua na wagonjwa 353 walipatiwa matibabu kwa kufanyiwa upasuaji wa kufungua kifua.

Dkt. Shemu anasema katika miaka ya nyuma upasuaji wa magonjwa ya kufungua kifua na bila kufungua kifua ulifanyika nje ya nchi na kusababisha Serikali kutumia fedha nyingi kuwapeleka wagonjwa nchini India kutibiwa. “Kutokana na huduma hii kutolewa na taasisi yetu hapa nchini kwa mwaka 2016 tumefanikiwa kuokoa zaidiyaTsh. Bilioni 2.6 kwa wagonjwa kwani kila mgonjwa mmoja akienda kutibiwa nchini India atagharimu zaidi yaTsh. Milioni 27”  anasema Dkt. Shemu

Akizungumza malengo ya mwaka 2017, Dkt. Shemu alisema taasisi hiyo imepanga kufanya upasuaji kwa wagonjwa 1700 wakiwemo wagonjwa 700 wa kupasua kifua na wagonjwa 1000 kwa kutumia mtambo wa catheterization usiohusisha upasuajiwa kufungua kifua, ambapo huduma hizo zitahusisha wananchi wote wenye matatizo ya moyo wakiwemo watoto na watu wazima. Akifafanua Zaidi Dkt. Shemu alisema kuwa nia ya taasisi hiyo ni kuhakikisha kuwa matatizo ya moyo yanapungua hapanchini, ambapo wamejipanga kutoa elimu ya moja kwa moja kwa Watanzania ikiwa ni pamoja kutoa elimu mashuleni kwa wanafunzi kwani magonjwa mengi ya moyo yanapatikana katika umri mdogo.

Aliongeza kuwa JKCI imejipanga kuimarisha ushirikiano na wadau na washirika wake wa nje zikiwemo taasisi za Save Health Child ya Israel, Hospitali ya Apolo Bangalole ya India, Almuntada ya Saudi Arabia, Open Heart International ya Australia na Mending Kids ya Marekani ili kubadilishana ujuzi wa kazi na wataalamu ili kuboresha utoaji wa huduma za matibabu ya moyo nchini. “Kwa kuwa mgonjwa anayefanyiwa upasuaji wa moyo anahitaji damu nyingi tunawaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kuchangia damu na uchangiaji huu usifanyike kwa mara moja bali uwe wa mara kwa mara”alisema Dkt. Shemu. JKCI ni hospitali ya taifa inayotibu moagonjwa ya moyo na kufundisha magonjwa ya moyo mishipa ya damu na kufanya utafiti. Hospitali hiyo pia inahudumia na upokea wagonjwa wa moyo kutoka nchi jirani ikiwemo Rwanda, Burundi, Visiwa vya Comoro na Uganda. Ni wajibu wa vyombo vya habari kuendelea kutoa elimu kwa wananchi hususani wa maeneo ya vijijini wajitokeza na kupata huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo yanayotolewa na taasisi hiyo.

Na mwandishi maalum.

Dar es Salaam.








All the contents on this site are copyrighted ©.