2017-03-27 09:03:00

Wenyeheri wapya ni mashuhuda amini wa Injili ya amani na upatanisho!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika Jumapili tarehe 26 Machi 2017 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, aliyaelekeza macho yake huko Almerìa, nchini Hispania ambako Kardinali Angelo Amato, Rais wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko aliwatangaza watumishi wa Mungu Josè Alvazer- Benavides y de la Torre na wenzake mashuhuda wafiadini mia moja na kumi na nne kuwa Wenyeheri.

Hawa walikuwa ni wakleri, watawa na waamini walei: mashuhuda amini wa Kristo, Injili ya amani na Upatanisho wa kidugu. Mfano wa maisha na maombezi yao anasema Baba Mtakatifu Francisko, yalisaidie Kanisa katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa upendo. Baba Mtakatifu alitambua uwepo wa makundi ya mahujaji kutoka ndani na nje ya Italia, lakini kwa namna ya pekee kabisa, ametumia fursa hii kumpongeza na kumshukuru Kardinali Angelo Scola, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Milano kwa mapokezi ya kukata na shoka waliyomwonesha na kumwonjesha Baba Mtakatifu Francisko kiasi hata cha kujisikia kuwa nyumbani wakati wa hija yake ya kitume Jimbo kuu la Milano, Jumamosi tarehe 25 Machi 2017. Familia ya Mungu Jimbo kuu la Milano katika ujumla wake imeonesha ukarimu kwa Baba Mtakatifu Francisko kiasi hata cha kumwezesha kuonja ukarimu wa watu wa Milano uliokuwa umebebwa mikononi mwao! Takwimu zinaonesha kwamba, zaidi ya watu milioni moja wameshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu huko Jimbo kuu la Milano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.