2017-03-27 14:56:00

Kanisa kuu la Carpi latabarukiwa, tayari kwa maadhimisho ya Ibada!


Katika maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria kupashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu, Jumamosi, tarehe 25 Machi 2017, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kutabaruku Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Carpi, nchini Italia, baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa. Itakumbukwa kwamba, Kanisa hili lilibomolewa na tetemeko la ardhi lililoikumba sehemu ya “Emilia Romagna”, miaka mitano iliyopita. Sherehe hii ni sehemu ya maandamizi ya ziara ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko jimboni humo Jumapili tarehe 2 Aprili 2017.

Kardinali Parolin katika mahubiri yake amesema, majanga asilia yanaweza kugusa na kuwatikisa watu wengi, kiasi cha kuwaingiza hata kwenye majaribu na hali ya kukata tamaa, lakini ikumbukwe kwamba, matukio yote haya hayana sauti ya mwisho. Kwa ushirikiano wa dhati kati ya Kanisa, Serikali na wadau mbali mbali, Mwenyezi Mungu amewezesha kukamilisha ukarabati huu mkubwa uliofanywa kwa uweledi, ujasiri, juhudi, bidii na maarifa, kielelezo cha maisha mapya na kama sehemu ya mchakato wa kuganga na kuponya majeraha yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi lililotokea kunako mwaka 2012. Sasa ni wakati wa kusimama na kuanza kutembea kwa imani na matumaini, ili kujenga na kuimarisha mshikamano kati ya watu.

Kardinali Parolin amewataka waamini kujenga mwelekeo chanya hata pale wanapokabiliwa na changamoto za maisha! Kutabarukiwa kwa Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Carpi ni fursa na changamoto kwa waamini kumfungulia tena Kristo Yesu, akili na nyoyo zao, ili aweze kuwakirimia ujumbe wa amani, furaha, wokovu na uhuru kamili.

Kwa upande wake, Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, amezungumzia tukio hili kuwa ni chemchemi ya matumaini baada ya mateso, mahangaiko, wasi wasi na mashaka pamoja na kazi kubwa iliyofanywa na wajenzi, kielelezo makini na utambulisho wa wananchi wa Italia, licha ya changamoto na matatizo yanayojitokeza nchini Italia. Huu ni ushuhuda unaofumbatwa katika Injili ya Kristo. Kanisa Katoliki nchini Italia linapania kujizatiti zaidi katika maisha na utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kuwahudumia watu bila ya kujibakiza kama Mapadre na viongozi wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.