2017-03-24 14:28:00

Rais wa Fiji akutana na kuzungumza na Papa Francisko mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 24 Machi 2017 amekutana na kuzungumza na Rais Jioji Konousi Konrote wa Fiji ambaye baadaye amekutana na kuzungumza pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake, katika mazungumzo yao, wamegusia uhusiano mwema uliopo kati ya Vatican na Fiji sanjari na mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Fiji katika ujumla wao. Baadaye, wamechambua kwa kina na mapana athari za mabadiliko ya tabianchi; umuhimu wa kuzingatia utashi wa kimaadili unaofumbatwa kwa namna ya pekee kabisa katika mshikamano na watu pamoja na nchi maskini zaidi duniani, bila kuwasahau vijana wa kizazi kipya wanaopaswa kufundwa juu ya ulinzi na matumizi bora ya mazingira nyumba ya wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.