2017-03-24 13:30:00

Jumuiya ya Ulaya miaka 60: Kipaumbele: utu na heshima ya binadamu!


Jumuiya ya Ulaya ilianzishwa rasmi tarehe 25 Machi 1957 kwa Mawaziri wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa kutoka katika nchi 5 walipotia mkwaju uanzishwaji wa Jumuiya ya Ulaya. Huu ukawa ni mwanzo wa Jumuiya ya Uchumi Barani Ulaya pamoja na Jumuiya ya Nishati ya Atomik Barani Ulaya. Katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Ulaya, mambo makuu manne yanapewa kipaumbele cha kwanza: Ulinzi na usalama; Ukuaji wa uchumi na Maendeleo ya kijamii.

Jumuiya ya Ulaya ina nguvu kubwa sana ya kiuchumi, inaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa maboresho ya maisha ya kijamii ndani na nje ya Bara la Ulaya; ukuaji wa uchumi, mshikamano na mafungamano ya kijamii sanjari na ukuzaji wa soko huria. Nchi 27 wanachama wa Jumuiya ya Ulaya zinataka kwa namna ya pekee kukuza uchumi  na kutengeneza fursa za ajira hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya wanaoonekana kukata tamaa kutokana hali ngumu ya maisha.

Hapa viongozi wakuu wa Jumuiya ya Ulaya wanasema, kuna haja ya kukuza na kudumisha mshikamano unaofumbatwa katika kanuni auni, ili kuimarisha mfumo wa fedha za Ulaya. Jumuiya ya Ulaya itaendelea kushirikiana na kushikamana katika sera za mambo ya nchi za nje, ulinzi na usalama sanjari na kuendeleza mchakato wa ukuzaji wa biashara. Lengo ni kutaka Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kuwa na nguvu ya kiuchumi katika jukwaa la kimataifa.

Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha uongozi wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa muda wa miaka minne, kila wakati alipopata nafasi ya kuzungumza na wakuu wa Jumuiya ya Ulaya yaani: alipotunukiwa Tuzo ya “Carlo Magno” hapo tarehe 6 Mei 2016 na tarehe 25 Novemba 2015 alipohutubia Bunge la Jumuiya ya Ulaya huko Strasbourg. Baba Mtakatifu amekazia zaidi kuhusu changamoto zinazopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Ulaya: amani, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; haki msingi za binadamu; wakimbizi na wahamiaji; fursa za ajira na vijana.

Baba Mtakatifu amegusia pia tema ambazo ni tete kwa Jumuiya ya Ulaya kama vile: umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; umuhimu wa kutambua na kuenzi utambulisho wa Ulaya; kwa kusimamia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anawataka viongozi wa Jumuiya ya Ulaya kujipanga tena ili kudumisha demokrasia, haki msingi za binadamu, uhuru, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni wajibu wao kuganga na kuponya madonda ya vita, kinzani na ubaguzi; mambo yanayohatarisha amani, ili hatimaye, kujenga madaraja ya watu kukutana.

Utambulisho wa Jumuiya ya Ulaya daima unafumbatwa kwa watu wanaotoka katika tamaduni mbali mbali, changamoto ni kuendelea kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; mambo yanayofumbatwa katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi kama njia ya watu kukutana ili kufahamiana na kushirikiana kwa dhati kabisa! Jumuiya ya Ulaya inapaswa kuibua mbinu mkakati wa sera za uchumi shirikishi zinazojikita katika usawa ili kukidhi mahitaji msingi ya binadamu na wala si faida kubwa ambayo imepelekea mtikisiko wa uchumi kimataifa na madhara yake bado yanaendelea kuonesha makucha yake. Kanisa kwa upande wake anasema Baba Mtakatifu Francisko litaendelea kutangaza na kushuhudia Injili Barani Ulaya; Injili inayofumbatwa katika huruma ya Mungu inayoganga na kuponya madonda ya udhaifu wa mwanadamu; kwa kukazia umoja, upendo na mshikamano kati ya watu, ili kweli wote waweze kuwa wamoja!

Baba Mtakatifu anawataka wakuu wa Jumuiya ya Ulaya kujikita katika mchakato wa kuipyaisha Ulaya kwa kuvuka kinzani, migawanyiko na ubaguzi, ili kuambata misingi ya haki, amani, umoja na udugu kati ya watu wanaoaminiana na kuthaminiana; kiini cha yote haya ni utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni changamoto ya kusimama kidete kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa na sera za utoaji mimba na kifo laini. Binadamu anazo haki zake ambazo kamwe hawezi kupokonywa kutokana na ubinafsi au sera tenge!

Ugonjwa mkubwa unaowasumbua raia wengi wa Bara la Ulaya ni upweke hasi, ambao umepekenyuliwa pia na mtikisiko wa uchumi kimataifa na hivyo kusababisha hali ngumu zaidi, changamoto kubwa ni kuwajengea wananchi matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi; kwa kupenda na kutetea Injili ya uhai; kwa kuimarisha umoja katika utofauti; kwa kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Kazi na fursa za ajira; mazingira bora ya kazi, uzalishaji na huduma ni mambo msingi sana katika mchakato wa ujenzi wa familia na malezi kwa watoto ndani ya familia.

Jumuiya ya Ulaya inapaswa kuonesha mshikamano wa umoja na upendo kwa kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi badala ya kuwatelekeza ili wamezwe na mawimbi ya bahari ya Mediterrania ambayo imegeuka kuwa kaburi lisilokuwa na alama! Ni wajibu wa wanasiasa kuhakikisha kwamba, wanawajengea raia imani juu ya umuhimu wa Jumuiya ya Ulaya kwa kukuza amani, urafiki na udugu; kwa kujenga uchumi unaombata utakatifu, utu na heshima ya binadamu. Jumuiya ya Ulaya inapaswa anasema Baba Mtakatifu kuangalia historia yake ya nyuma ili kuiambata, kuwa na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi kwa kuondokana na woga pamoja na wasi wasi usiokuwa na mvuto wala mashiko! Bara la Ulaya linapaswa kusimama kidete kulinda na kutetea: maisha, utu, heshima na mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.