2017-03-23 11:06:00

Jukwaa la Uchumi Afrika: Mkazo: fursa za uchumi, hati moja na jumuiya!


Jukwaa la Uchumi Barani Afrika katika kikao chake huko Mauritius kilichowahusisha wadau mbali mbali kutoka Afrika imekuwa ni fursa ya kupembua kwa kina na mapana sera na mikakati itakayoliwezesha Bara la Afrika kucharuka katika masuala ya uchumi endelevu ifikapo mwaka 2060. Jukwa hili limekuwa ni mahali pa kuweka sera na mikakati ya muda mrefu na mfupi inayopaniwa kufikiwa Barani Afrika katika muda uliopangwa. Kumbe, mkutano wa Mauritius kwa mwaka huu, ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati uliofikiwa na Umoja wa Afrika katika mkutano wake wa Mwezi Julai, 2016 huko Kigali, Rwanda. Wajumbe wa Jukwaa hili wameamua kufungua fursa za kiuchumi, kuanzisha mchakato wa kutumia hati moja ya kusafiria sanjari na kuimarisha Jumuiya za Kikanda!

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema viongozi wa Mataifa ya Afrika wamekubaliana kufungua fursa za kiuchumi baina ya nchi hizo pamoja na kuweka utaratibu wa kutumia hati moja ya kusafiria. Alitoa kauli hiyo Jumatano, Machi 22, 2017 wakati akizungumzia makubaliano yaliyofikiwa katika uzinduzi wa Jukwaa la Uchumi Barani Afrika (AEP) uliofanyika nchini Mauritius Machi 20 hadi 21, 2017. Waziri Mkuu alimwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli. Waziri Mkuu alisema viongozi hao wamekubaliana kwamba mataifa ya Afrika yawe na hati moja ya kusafiria, ambayo itawawezesha wananchi kuingia nchi yoyote ndani ya bara hilo bila ya vikwazo kwa lengo la kurahisisha muingiliano wa watu na bidhaa.

Alisema jambo jingine walilokubaliana ni kuimarisha Jumuiya zao ikiwemo ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na kuzishawishi nchi nyingine ambazo hazijajiunga kujiunga jumuia hizo. Alisema viongozi hao walijadili namna watakavyoweza kuinua uchumi na kuweka mikakati ya kuimarisha viwanda, ambapo Tanzania ipo katika nafasi nzuri kwa kuwa tayari inatekeleza mpango wa kukuza uchumi wake kwa kupitia sekta ya viwanda. “Viwanda ndiyo mkombozi wa changamoto mbalimbali barani Afrika ikiwemo ya ajira, hivyo Serikali ya awamu ya Tano imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda ili kuongeza ajira na kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi wake,” alisema.

Jukwaa hilo lilizinduliwa Machi 20, 2017 na Waziri Mkuu wa Swazland Bw. Barnabas Sibusiso Dlamini kwa niaba ya Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) na Rais wa Chad, Idriss Deby. Pia Bw. Dlamini alimuwakilisha Mfalme Muwsati wa III. Bw. Dlamini alisema nchi za Afrika zinatakiwa kuboresha mitaa yake na kujikita katika kutoa elimu ya masuala ya sayansi na viwanda ili kuwajengea wanafunzi uelewa wa masuala hayo angu wakiwa na umri mdogo. Alisema iwapo wanafunzi wataanza kujifunza masuala ya viwanda kuanzia shule watakuwa na uelewa wa kutosha wa masuala hayo jambo ambalo litawarahisishia kupata ajira katika viwanda mbalimbali, hivyo kuondokana na tatizo la ajira linalozibakili nchi nyingi za Afrika.

Uzinduzi wa jukwaa hilo ulikuwa na ajenda nne ambazo zilihusu sekta ya viwanda, kukuza biashara miongoni mwa nchi za Afrika, kukuza ujuzi katika taaluma mbalimbali na kurahisisha muingiliano wa watu na bidhaa baina ya mataifa hayo. Jukwaa hilo lilifanyika kwa siku mbili lilihudhuriwa na viongozi wakuu wa nchi za Afrika, wanazuoni, wafanyabiashara pamoja na watu kutoka kwenye asasi mbalimbali za kiraia barani Afrika.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametembelea kiwanda cha Compagnie Mauricienne De Textile Ltee kinachotengeneza nguo kwa kutumia teknolojia ya kisasa nchini Mauritius chenye uwezo wa kutengeneza tani milioni 40 hadi 50 kwa mwaka. Aidha, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji hao kuja nchini Tanzania na kuwekeza katika viwanda vya kutengeneza nyuzi pamoja na nguo kwa kuwa kuna malighafi za kutosha kwa ajili ya uzalishaji huo.

Waziri Mkuu alitembelea kiwanda hicho kilichoko katika mji wa Latour Koenig Jumatano, Machi 22, 2017 na kujionea namna wanavyotengeneza nguo kwa kutumia teknolojia ya kisasa na kuamua kuwakaribisha waje kuwekeza nchini Tanzania. “Tumefarijika na uwekezaji wenu na tumejionea namna ambavyo mnavyoendesha kiwanda chenu kuanzia utengenezaji wa nyuzi hadi nguo, hivyo tunahitaji viwanda kama hivi nchini Tanzania kwa sababu sisi tunazalisha pamba nvingi na yenye ubora unaokubalika kimataifa,” alisema.

Waziri Mkuu alisema madhumuni ya kuwakaribisha wawekezaji hao kuja Tanzania na kuwekeza katika viwanda vya kutengeneza nyuzi yanalenga kuboresha kilimo cha pamba na kuwawezesha wakulima kupata tija.  “Tunalima pamba nzuri na hawa hawalimi wananunua kutoka nje ya nchi yao, hivyo wakija kuwekeza Tanzania itawarahisishia kupata malighafi ya uhakika na kwa urahisi ”. Alisema viwanda hivyo vitasaidia maendeleo ya kilimo cha pamba kwa sababu vitatoa ajira kwa wananchi wengi na kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umasikini wa kipato. Mbali na kuwakaribisha wawekezaji hao, pia Waziri Mkuu alitoa wito kwa wananchi wenye uwezo kuhakikisha wanajenga viwanda vya nyuzi kwenye mikoa yote inayozalisha pamba ili waweze kuiongezea thamani kabla ya kuiuza.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Fedha wa kiwanda hicho Bw. David Too Sai Voon alisema wamefurahishwa na mwaliko wa kuja Tanzania kwa ajili ya kuangalia maeneo ya uwekezaji wa viwanda vya nyuzi na nguo. Bw. David alisema kiwanda chao kilianzishwa mwaka 1986 na kwa sasa kimeajiri wafanyakazi 18,000 ambapo mauzo yao kwa mwaka ni dola milioni 200.“Nguo tunazotengeza ni za kiwango cha kimataifa na tunauza katika maduka makubwa Barani Ulaya,”

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU.








All the contents on this site are copyrighted ©.