2017-03-22 15:47:00

Msithubutu kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya!


Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wanaoishi nje ya nchi wazingatie sheria za Taifa husika na kamwe wasijihusishe na biashara haramu ya dawa za kulevya. “Vita ya dawa za kulevya ni kubwa, hata hivyo Serikali tunaendelea kupambana nayo. Nchi ilikuwa inapoteza vijana ambao walikuwa wamejiingiza katika biashara haramu ya dawa za kulevya. Nawaomba msithubutu kuingia huko mtafungwa,” amesema. Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Jumatano, Machi 22, 2017 wakati akizungumza na Umoja wa Watanzania wanaoishi nchini Mauritius katika mkutano alioutisha kwenye hoteli ya Meridien mjini Port Louis. Amesema katika kudhibiti biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya Serikali iliamua kuunda Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na inafanya kazi vizuri. “Na tutakamata kila mtu anayejihusisha na biashara hiyo bila kujali cheo, uwezo na mamlaka aliyonayo,”. Amesema mamlaka hiyo inafanyakazi ya kutafuta wazalishaji, watumiaji na wafanyabiashara, lengo likiwa ni kuokoa vijana ambao wameshindwa kutimiza ndoto zao kutokana na madhara waliyoyapata baada ya kutumia dawa za kulevya.

Katika hatua nyinngine, Waziri Mkuu amewataka Watanzania hao walioko nchini Mauritius kujenga mshikamano wa pamoja na wawe na uzalendo na nchi yao. Pia wawe mabalozi wazuri wa kutangaza vivutio vya Taifa. Amesema ni vema wakatumia fursa walizonazo katika kutafuta wawekezaji na kuwashawishi waje nchini na kuwekeza kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za viwanda, uvuvi, nishati na utalii. Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohammed amewaomba Watanzania hao wazidishe mshikamano miongoni mwao kwa kuwa umoja wao ndiyo nguzo yao. “Mko hapa kwa ajili ya kutafuta elimu na wengine mnafanya kazi, shughuli ambazo zitawasaidia kuboresha maendeleo yenu na Taifa kwa ujumla, hivyo nawaomba mzingatie kilichowaleta,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa muda wa Umoja wa Watanzania waishio nchini Mauritius, Bw. Donald Kongwa ambaye ni Ofisa wa Benki ya Standard Chaetered nchini Mauritius amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba kipato wanachokipata watakitumia kwa kuwekeza Tanzania kwa lengo la kukuza uchumi wa Taifa. Aidha, amesema wanaunga mkono na kupongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kujenga uchumi wa viwanda, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, ujenzi wa miundombinu ya kisasa, ununuzi wa ndege pamoja na kuimarisha uwajibikaji na nidhamu kwa watumishi wa umma.

Wakati huo huo, Waziri mkuu Kassim Majaliwa ametembelea kiwanda cha kusindika samaki aina ya jodari na kuwakaribisha viongozi wa kiwanda hicho kuja nchini kuangalia maeneo ya uwekezaji wa viwanda vya samaki. Amesema Serikali imeweka sera nzuri za uwekezaji na pia ina maeneo mengi na mazuri kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vya samaki, ambayo ni bahari, mito na maziwa ambayo aina mbalimbali za samaki. Waziri Mkuu amesema hayo Jumanne, Machi 21,2017 wakati alipotembelea kiwanda cha samaki cha Mer des Mascareignes kilichoko jijini Port Louis nchini Mauritius. “Tanzania kuna fursa nyingi za uwekezaji hasa kutokana na mazingira yake. Mnaweza kuja kuwekeza kwenye viwanda vya usindikaji wa samaki tuna bahari, mito na maziwa yenye samaki wa aina mbalimbali,” alisema. Waziri Mkuu alisema Serikali imedhamiria kuimarisha uchumi wake kupitia sekta ya viwanda ili kuongeza tija kwa Taifa na kwa wananchi kiujumla hivyo wanahitaji wawekezaji waliotayari kuja kuwekeza nchini.

Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohammed alisema Tanzania inahitaji wawekezaji watakaowekeza kwenye uvuvi wa kina kirefu na ujenzi wa viwanda vya samaki. Dkt. Khalid alisema lengo la uwekezaji huo ni kukuza uchumi wa Taifa pamoja kupanua soko la ajira na kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi wake.

Naye Meneja Mkuu wa kiwanda hicho, Bw. Patrick Hill alisema wamefurahi na mwaliko wa kuja Tanzania kwa ajili ya kuangalia fursa na uwekezaji na kwamba wako tayari kushirikiana na Serikali. Alisema kampuni yao inajishughulisha na usindikaji wa samaki aina moja tu ya jodari na wananunua kutoka kwa makampuni makubwa ya uvuvi huku wateja wao wakubwa wakiwa ni Bara la Ulaya.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alitembelea kiwanda kingine cha Chantier Naval Del`Ocean Indien Limited (CNOI) ambacho kinatengeneza na kukarabati meli , boti na pantoni na kujionea uwezo mkubwa walionao, ambapo Watanzania wanaweza kuja kujifunza.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU.








All the contents on this site are copyrighted ©.