2017-03-22 14:18:00

Kipofu akutana mubashara na Yesu, asimulia yaliyomsibu!


Dhana ya upofu au uoni hafifu au ulemavu wa macho au uwezo wa kuona ina mapana na marefu yake. Kwa mfano tunapoongea kuhusu upofu tunaona kuwa sote tuna upofu wa aina fulani – kwa mfano kwa wakati mmoja hatuwezi kuona vyote n.k. Tunaona mpaka umbali fulani tu au kama tu kuna mwanga n.k. Hata aliye na macho kamili hawezi kuona kila kitu. Mtoto mdogo anapozaliwa hufanana na kipofu kwa maana kuwa hawezi kutumia vizuri macho yake, halafu pole pole huanza kuona na huanza kutofautisha vitu.  Binadamu hutazama na kuona kwa macho yake kama yako salama. Katika somo la kwanza – Samweli anatazama kwa macho ya kibinadamu ila kadiri ya mpango wa Mungu anakosea. Anasahau kuwa alitumwa na Mungu na hivyo mtazamo wake ungetakiwa kutumia jicho la Kimungu.

Kuona ni  tendo la kimiujiza pia, ila kwa vile tumezoea hatuoni tofauti hiyo – hapa anaingia  Yesu katika Injili ya leo – anamtoa toka usingizini yule ambayealikuwa haoni – anamfanya aone. Lakini zaidi ya hilo – kuna jicho la imani – haja ya kuvuka kile tukionacho katika ulimwengu huu – na kuingia katika ulimwengu wa Mungu. Kama tungesoma sura iliyotangulia – Yoh. 8:12 – Yesu  anasema mimi ni nuru ya ulimwengu – aniaminiye mimi hatatembea gizani tena. Yesu ni nuru ya mwili na roho.  Ndicho anachotukumbusha Yesu leo kwa kumponya yule kipofu. Haja ya kuona kwa jicho la kimungu. Anamtuma katika kisima cha Siloam, mahali pa ubatizo – anapokea zawadi ya Imani. Tunaona kuwa imani ya yule kipofu haipo katika Mungu ila katika Kristo. Injili yatuonesha namna ya kufika kwake Yesu. Yesu anaonekana mwanzoni na mwishoni – katikati yahitajika juhudi binafsi. Hitimisho la mgogoro – mstari 39 -41 – mimi nimekuja ili wasioona waone a wanaoona wawe vipofu. Anapofunguka macho – anatambua pia kuwa Yesu ni nani – kabla hakujua kuwa Yesu ni nani – ila baadaye anasema – mtu aitwaye Yesu alinipaka matope.

Baadaye, anaulizwa – unasemaje juu yake – yule aliyekufungua macho yako? Ni Nabii na anaendelea mbele – anatambua kuwa ametoka kwa  Mungu, anafanya yote kwa niaba yake. Anashuhudia.  Mwishoni – alipokutana tena na Yesu – anasema – Bwana naamini – na anainama kumwabudu – hivyo rasmi anamtambua kuwa Bwana na Mungu. Hii inatokea mwishoni kabisa. Alichofanya yeye ni kumruhusu Yesu kuingia katika maisha yake na kufuata maagizo yake. Angalia mfano huu – bibi Tarabushi – alitumwa kwenda kumwona shangazi yake mgonjwa na masharti aliyopewa njiani, usiongee na mtu yo yote. Njiani alikutana na mbwa mwitu na alipoulizwa unakwenda wapi akamweleza alichotumwa kufanya – kwamba anakwenda kumwona shangazi yake mgonjwa. Alichofanya mbwa mwitu alimwelekeza njia ndefu naye akachukua njia fupi, akafika kwa shangazi yake akamuua na kumla. Alipofika bibi tarabushi alipokelewa na mbwa mwitu aliyejifanya mgonjwa na akiwa amelala kitandani kama mgonjwa. Akamvamia na kumwua.huyu asingaliuawa kama angefuata maagizo aliyopewa toka nyumbani.

Pengine Mwinjili Yohane/Kanisa linaweka mbele yetu leo swali. Na mimi Je,  niko wapi katika maisha yangu ya imani? Yesu Kristo wa Nazareti ni nani kwangu? Ninaona nini? Tunaambiwa kuwa ukivaa miwani nyeusi kila ukionacho ni cheusi n.k. sisi tunaona nini katika maisha yetu ya kawada na yale ya kiimani? Katika Mt. 17:5 tunasoma – huyu ni mwanangu mpendwa – msikilizeni yeye – kung’ara sura. Je kweli tunamsikiliza Mwana wa Mungu? Kwamba Yesu ni mtu, ni Nabii aliyetoka kwa Mungu – ulimwengu wote unatambua hilo. Watu wengi kama si wote tuko pamoja. Ila hii haitoshi. Mwislamu – akielewa vizuri Korani – anatambua kuwa Yesu ni Nabii – lakini ufahamu huu haumfanyi yeye na mimi kuwa wakristo. Kitakachotuvusha/tofautisha kuwa mkristo katika maana halisi ni pale tunapotamka/kiri kama yule kipofu kuwa Kristo ni Bwana na kumwabudu kama Mungu.

Imani ya kikristo si imani katika kitu fulani – kwamba Mungu yupo, anaishi n.k ila ni imani katika mtu. Katika injili Yesu hatupi orodha ya vitu ili tuabudu – ila asema – MWAMINI MUNGU, NIAMINI  PIA NA MIMI – Yoh. 14.1.  Ni changamoto kubwa hapa. Ndiyo changamoto ya imani yetu leo.  Ili kujifunza toka kwake Yesu ni lazima tukubali ujinga wetu. Ili kuponywa ni lazima tuukubali upofu wetu: Ili kusamehewa ni lazima kuungama dhambi zetu. Jibu la yule aliyeponywa ni zuri na changamoto kwetu sote – mimi sijui mengine ila kuwa nimepona na sasa naona. Inashangaza kweli habari juu ya mapenzi yake Mungu – yule aliyekuwa kipofu, mwombaji – anapona – anakuwa mfuasi na anashuhudia. Tunaimarishwa na Neno la Mungu toka Mt. 3:17 – baada ya ubatizo – na sauti ikatoka mbinguni – huyu ni mwanangu mpendwa, ninapendezwa naye. Waliokuwa na elimu ya Maandiko Matakatifu hawakuweza kufikia hatua hiyo, wao waliyafahamu Maandiko yeye alikutana na Yesu moja kwa moja au kwa lugha ya kisasa "Mubashara" na akamwamini. Wao wanakataa – wanabaki katika ugumu wa mioyo yao na upofu wao wa sheria, mila na desturi zao. Wanakataa hata muujiza wa Mungu. Wanabaki vipofu. Wanapoteza muda kutafuta kwa nini amepona, kwamba kwa vile alikuwa mdhambi basi asingestahili kupona. Hawafurahii kupona kwake. Wanasema hakustahili – yeye ambaye alipokuwa kipofu hakuna aliyekuwa na muda naye.

Sisi ni wafuasi wa Yesu sasa – tunaponyaje upofu uliopo kati yetu? Haja ya kufanya jambo fulani – halisi na si maneno maneno tu. Je, mimi/wewe ni kipofu/farisayo au mfuasi wa Yesu? Kipofu hawezi kumwongoza kipofu mwenzake.  Na kama ni mfuasi – umeshaponya vipofu wangapi? Shida yetu ni ipi? UWEZO WA KUONA AU UPOFU WA IMANI? Tutafakarishwe na mfano huu.

Miaka mitatu iliyopita nilishiriki ibada na sherehe parokiani Mpwapwa  ya  miaka 50 ya maisha ya ndoa ya wazazi wa Padre Limu. Wakati wa mlo nilikaa kulia kwa mtu mmoja. Huyo mtu ni kipofu wa kuzaliwa na ni mwalimu. Wakati sherehe ikiendelea n.k huyo mtu alianza kunieleza na kunikumbusha makutano yetu miaka 10 iliyopita alipotembelea Jumuiya yetu wakati nikiishi “St. Gaspar College Morogoro”. Alikaa kwetu siku tatu na akanikumbusha kuwa pia nilimsindikiza kituo cha basi Msamvu. Mimi sikumkumbuka kabisa mpaka aliponishirikisha hiyo habari. Angekaa kimya nisingemkumbuka. Hakika nilijisikia vibaya sana. Yule aliye kipofu amenitambua wakati miye mwenye macho sikuweza kumtambua. Niliona aibu sana. Hapa ikanipa changamoto kubwa. Sasa kipofu hapa ni nani? Mimi au yeye? Je sisi tunaona nini? Kumbukumbu zetu za maisha, mitazamo yetu n.k zikoje? Tunaamabiwa kuwa tusipoteze muda wetu kulaani giza, bali tuwashe taa ili daima ziangaze na kutoa mwanga.

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.