2017-03-22 16:48:00

Itikieni kwa ukarimu mpango mkakati wa Saa 24 kwa ajili ya Bwana!


Mara baada ya katekesi yake , Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 22 Machi 2017 amewaalika jumuiya zote za kikristo kuishi kikamilifu katika mkakati wa saa 24 kwa ajili ya Bwana, ili kuweza kugundua sakramenti ya kitubio. Anasema hata kwa mwaka huu uwe ni fursa ya kuishi  neema katika kipindi cha kwaresima  kwenye makanisa kwa kufanya uzoefu wa kukutana na furaha ya  huruma ya Baba anaye pokea wote na kuwasamehe. Ikimbukwe kwamba,  hivi karibuni mwaliko huo ulitolewa katika Waraka wake wa Kitume, “Misericordiae vultus” yaani “Uso wa huruma” mbapo aliwaalika waamini kushiriki mpango wa mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana”.

Ni desturi inayoadishimishwa Ijumaa na Jumamosi zinazotangulia Jumapili ya 4 ya Kipindi cha Kwaresima. Huu ni mwaliko kwa waamini kukimbilia tena kiti cha huruma ya Mungu ili kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, tayari kuambata huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Sakramenti ya Upatanisho ni mahali muafaka pa kuadhimisha huruma ya Mungu katika maisha ya mwamini, kwani hapa mwamini, anagusa kwa mikono yake mwenyewe huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani.

Akiwasalimia mahujaji wote katika viwanja vya Mtakatifu Petro, Naba Mtakatifu Francisko ametoa salam kwa namna ya pekee  washiriki wa Mkutano kuhusu waamiaji  unao endelea mjini  Vatican na kusema anawatia moyo  wa kuendelea kuwajibika katika kuwapokea na kuwapatia mahali pa kukaa wakimbizi na wahamiaji, kwa kuwasaidia waweze kushiriki kikamilifukuzoea  lakini katika  kutambua haki na wajibu wao kwa wale wanaopokelewa au kuwapokea.Halikadhalika amewasalimia vijana wenye mtindio wa ubongo  kutoka chini ya Italia, na vijana wengine wote bila kuwasahau wagonjwa na wanandoa wapya.

Amekumbusha kuwa Jumamosi tarehe  25 Machi, 2017 Kanisa Katoliki linaadhimisha Sikukuu ya Bikira Maria kupashwa habari na Malaika Gabrieli kwamba atakuwa ni Mama wa Mungu,  hivyo vijana watambue na kusikiliza  mapenzi ya Mungu kama vile Mama Maria.Wagonjwa, amesema ,wasikate tamaa katika kipindi kigumu, wakitambua ya kwamba Bwana hawezi kuwapatia msalaba wenye nguvu zaidi ya uwezo wao. Na kwa Wana ndoa wapya, wajenge maisha yao ya ndoa juu ya mwamba wa Neno la Mungu.

Sr Angela Rwezaula

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.