2017-03-22 13:51:00

Baraza la Makanisa Ulimwenguni: Kiu ya haki duniani!


Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anasema, Kipindi cha Kwaresima ni wakati muafaka wa kutafakari kwa kina kuhusu umuhimu wa hija ya haki na amani Barani Afrika, sanjari na “kampeni ya majuma saba kwa ajili ya maji”. Anasema, maji yana nguvu na ni sehemu muhimu sana ya maisha ya binadamu kama ilivyo haki na amani kwa Bara la Afrika. Umefika wakati kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kukumbatia haki ili kuzima kiu ya walimwengu wanaoendelea kumlilia Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia haki, amani na ustawi.

Dr. Olav Fykse Tveit ameyasema hayo, tarehe 20 Machi 2017 wakati alipokuwa anahubiri kwenye Kikanisa cha Kiekumene kilichoko mjini Geneva, nchini Uswiss. Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kushirikiana kikamilifu na mpango wa Mungu katika kutafuta na kudumisha misingi ya haki, ili kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu. Kipindi cha Kwaresima kiwajengee waamini utamaduni wa kusikiliza, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao.

Neno la Mungu linafafanua ukosefu wa haki msingi sehemu mbali mbali za dunia, changamoto ni kuwa kweli mashuhuda na vyombo vya haki ya Mungu duniani. Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, mwanadamu ameweza kukombolewa kutoka katika lindi la dhambi na mauti na kufanywa haki kwa njia ya Kristo! Kimsingi binadamu hawezi kuishi bila maji na kwamba, maji ni rasilimali muhimu sana katika ustawi na maendeleo ya binadamu. Maji yawasaidie waamini pia kuwa ni mashuhuda wa upendo na huruma ya Mungu kwa waja wake. Kama jinsi maji yalivyo na umuhimu wa pekee katika maisha ya mwanadamu ndivyo ilivyo kiu ya haki kwa wale wanaoitafuta usiku na mchana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.