2017-03-17 15:58:00

Viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Tumbaku, Tabora wapigwa pingu


Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora kuwakamata viongozi wanne wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Tumbaku (WETCU) pamoja na kufunga ofisi za chama hicho hadi uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za chama hicho utakapokamilika. Pia Waziri Mkuu amevunja Bodi ya WETCU pamoja na Bodi ya Tumbaku Tanzania - TTB kwa sababu ya kushindwa kusimamia zao hilo pamoja na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo Alhamisi Machi 16, 2017 katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Isike Mwanakiyungi mkoani Tabora, ambapo amesema Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa TTB, Bw. Vita Kawawa pamoja na Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo Bw. Wilfred Mushi. Viongozi wa WETCU ambao Waziri Mkuu ameagiza wakamatwe ni Mwenyekiti Bw. Mkandara Mkandara, Makamu Mwenyekiti Bw. Msafiri Kassim, Mkaguzi wa Ndani na Mhasibu Mkuu. Pia amewasimamisha kazi watumishi wa kitengo cha uhasibu wa chama hicho hadi uchunguzi utakapokamilika. “Kuanzia sasa watumishi wote wa kitengo cha uhasibu pamoja menejimenti nimewasimamisha kazi pamoja na Mrajisi wa mkoa wa Tabora Deogratius Rugangila. Kamanda hakikisha ofisi hazifunguliwi kuanzia sasa hadi hapo timu ya ukaguzi itakapokamilisha kazi yake,” amesisitiza.

Waziri Mkuu amesema kwa muda mrefu wakulima wameteseka na zao hilo kukosa tija kwa sababu ya usimamizi mbovu wa viongozi wa ushirika na Bodi ya Tumbaku Tanzania jambo ambalo Serikali haiwezi kulivumilia.

Amesema “Hatuwezi kuwa na ushirika ambao hauwasaidii wanachama. WETCU walipokea sh. bilioni 15 ambazo walizikatia risiti na hazijaonekana. Pia waliwalipa wazabuni sh, bilioni 10 ambazo hawajazikatia risiti,”. “Wakati wanachama ambao ni wakulima wakiendelea kutesema WETCU walinunua gari la sh. milioni 269 kinyume na na maelekezo ya Mkutano Mkuu wa wadau ambao ulipitisha zitumike Shilingi milioni 40 tu,”amesema. Waziri Mkuu ameongeza kuwa chama hicho kimesababisha kupungua kwa uzalishaji kwa kiasi kikubwa kutokana na kuwa na menejimemti mbovu jambo ambalo limechangia wakulima wa tumbaku kukosa tija.

Amesema WETCU kimekithiri kwa matumizi mabaya ya fedha ambapo alitolea mfano suala la ukarabati wa ofisi tatu ikiwemo ya makao makuu ambayo ilipangwa ikarabatiwe kwa sh. milioni 33 wakatumia sh. milioni 170 na ofisi za Tabora na Urambo zilipangiwa sh. milioni tano kila moja na hazikukarabatiwa. Pia Waziri Mkuu amepiga marufuku ununuzi wa mbolea kutoka nje ya nchi wkatiikiwa inazalishwa hap nchini. Aidha, alimepiga marufuku matumizi ya kwa dola katika sekta ya tumbaku na badala yake zitumike fedha ya Kitanzania kwa sababu kitendo hicho kimekuwa kiwanyonya wakulima.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mheshimiwa Aggrey Mwanri, wakuu wa wilaya zote za mkoa huo pamoja na Maofisa Kilimo na Ushirika kuhakikisha wanasimamia vizuri zao hili ili liweze kuwa na tija kwa wakulima na Taifa kwa ujumla. Pia amewaagiza Maofisa Kilimo waende vijijini na kuwatambua wakulima wa tumbaku katika kila kijiji na kuwasajili. “ Kuanzia leo Maofisa Ushirika wabadilishe mienendo ya kazi nataka wasimamie zao la tumbaku kwa umakini zaidi.”

Wakati huo huo, Waziri mkuu awakaribisha Wairan kuwekeza nchini Tanzania:

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Iran ili waje kuwekeza kwenye viwanda mbalimbali vikiwemo vya kuchakata mazao ya kilimo na uvuvi. “Tumedhamiria kujenga Tanzania ya viwanda, tunawakaribisha wawekezaji kutoa Iran ili waje kuwekeza kwenye viwanda vya usindikaji mazao ya kilimo na uvuvi,” amesema.

Ametoa kauliIjumaa, Machi 17, 2017) alipokutana na Balozi wa Iran nchini Tanzania, Mheshimiwa Mousa Farhang kwenye makazi yake Oysterbay jijini Dar es Salaam. Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya Tano imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda ili kuongeza ajira na kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi wake, hivyo wanahitaji uwekezaji mkubwa kwenye sekta mbalimbali. Pia Waziri Mkuu amewakaribisha raia wa Iran kuitembelea Tanzania kama watalii kwa sababu kuna fursa nyingi za utalii ukiwemo mlima wa Kilimanjaro ambao unaongoza kwa urefu barani Afrika pamoja na mbuga nyingi zilizosheheni wanyama.

Kwa upande wake, Balozi Farhang ameipongeza Serikali ya awamu ya Tano kwa dhamira ya dhati ya kuimarisha uchumi na kupambana na dawa za kulevya na ufisadi. Amesema Tanzania ni mfano wa kuigwa na mataifa mengine barani Afrika. “Ufisadi na dawa za kulevya ni tatizo kubwa ambalo linazikabili nchi nyingi, hivyo kitendo cha Serikali ya Tanzania kupambana na tatizo hilo ni cha kupongezwa na kitaiwezesha kusonga mbele kiuchumi,” amesema. Balozi Farhang amesema anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mzuri na Iran ambao umedumu kwa miaka 40, hivyo ameiomba ifungue Ofisi ya Ubalozi nchini Iran ili kuimarisha uhusiano huo, ambapo Waziri Mkuu amekubali. “Tanzania na Iran wana uhusiano wa kihistoria ambao unadhihirishwa na uwepo wa Washirazi wengi husan visiwani Zanzibar ambao wanaasili ya Iran na maeneo ya kusini mwa Iran kuna Watanzania wengi hata muonekano wao ni wa Kitanzania,” amesema.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amekwenda nyumbani kwa marehemu Sir George Kahama Mikocheni jijini Dar es Salaam na kutoa pole kwa mjane Bi. Janneth Kahama pamoja na watoto na ndugu wa marehemu. Baada ya kuwasili nyumbani kwa marehemu, Waziri Mkuu alitia saini kitabu cha maombolezo kabla ya kuzungumza na majane Bi. Janneth na baadae alijumuika na waombolezaji kwenye viwanja vya nyumba hiyo.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU.








All the contents on this site are copyrighted ©.