2017-03-17 07:58:00

Uteuzi wa Maaskofu wapya Keta-Akatsi, Ghana na Laghouat, Algeria


Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Askofu Claude Rault wa Jimbo la Laghouat, Tunisia la kung’atuka kutoka madarakani. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemteua Mheshimiwa Padre John Gordon MacWilliam kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Laghouat. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule John Gordon MacWilliam alikuwa ni Padre Mkuu wa wa Kanda ya Wamissionari wa Afrika huko Algeria na Tunisia. Askofu mteule John Gordon MacWilliam alizaliwa tarehe 20 Novemba 1948. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi,baada ya kulitumikia Jeshi kwa muda wa miaka 17, kunako tarehe 4 Julai 1992 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre.

Kati ya Mwaka 1992- 1995 alijiendeleza kwa masomo ya Kiarabu na Kiislam mjini Roma. Kati ya mwaka 1995 hadi mwaka 2008 aliteuliwa na wakuu wake wa Shirika kufanya utume sehemu mbali mbali nchini Algeria. Tangu Mwaka 2008 hadi mwaka 2015 alidhamishwa na Shirika utume huko Tunisia sanjari na kuwa ni Mkurugenzi mkuu wa Kituo cha Lugha ya Kiarabu, Tunis, Tunisia. Tangu mwaka 2015 amekuwa ni Padre mkuu wa Kanda ya Shirika la Wamissionari wa Afrika, Kaskazini mwa Afrika.

Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu Gabriel Edoe Kumordji kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Keta-Akatsi nchini Ghana. Askofu Kumordji alizaliwa tarehe 24 Machi 1956 huko Accra, Ghana. Baada ya majiundo yake ya kitawa kwenye Shirika la “Neno la Mungu” (Society of the Divine Word, S.V.D.) akaweka nadhiri zake za daima hapo tarehe 8 Desemba 1980. Tarehe 12 Juni 2007 akateuliwa na Papa Mtsaafu Benedikto XVI kuwa Askofu na kuwekwa wakfu hapo tarehe 17 Aprili 2010.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.