2017-03-16 15:21:00

Papa Francisko akutana na Rais wa Lebanon!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 16 Machi 2017 amekutana na kuzungumza na Rais Michel Aoun wa Lebanon ambaye baadaye amekutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameandamana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican. Katika mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu Francisko na mgeni wake, wamegusia kuhusu uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili pamoja na kukazia mchango wa Kanisa Katoliki katika maisha, ustawi na maendeleo ya wananchi wa Lebanon.

Baba Mtakatifu amewapongeza wadau mbali mbali walioshirikiana kuhakikisha kwamba, Lebanon inafanya uchaguzi ili kumpata Rais mpya, changamoto na mwaliko kwa wadau mbali mbali kushirikiana na kushikamana nchini Lebanon kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya wengi nchini Lebanon. Katika mazungumzo yao, viongozi hawa wawili wamegusia pia vita inayoendelea nchini Syria na jitihada za Jumuiya ya Kimataifa kupata suluhu ya kisiasa katika mgogoro huu ambao umesababisha majanga makubwa kwa wananchi wengi  wa Syria. Baba Mtakatifu ameipongeza Lebanon kwa kuonesha ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka Syria wanaoendelea kupata hifadhi nchini humo! Baadaye, Baba Mtakatifu na mgeni wake Rais wa Lebanon wamgusia masuala ya kikanda na kimataifa mintarafu vita sanjari na hali ya Wakristo huko Mashariki ya Kati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.