2017-03-15 06:38:00

Wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu wanapaswa kunolewa vyema!


Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” anasema, huruma ya Mungu kwa namna ya pekee kabisa inaadhimishwa kwenye Sakramenti ya Upatanisho, ambapo Mwenyezi Mungu anamkumbatia mdhambi na kumpatia tena neema ya kutubu na kumwongokea, tayari kuendelea na safari ya maisha ya kiroho. Mapadre wanakumbushwa kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu, dhamana wanayopaswa kuitekeleza kwa dhati, ili kweli huruma na upendo wa Mungu viweze kuwaambata waamini katika maisha yao hapa duniani.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwahamasisha Mapadre kuhakikisha kwamba, wanajiandaa vyema kwa ajili ya kuadhimisha huduma ya Fumbo la Sakramenti ya Upatanisho, kiini cha utume wao kama Makuhani wa Kristo na Kanisa lake. Kutokana na changamoto hii, Idara ya Toba ya Kitume kuanzia tarehe 14 hadi 17 Machi 2017 inaendesha mafunzo ya ndani kwa Wakleri na Majandokasisi wanaojiandaa kwa ajili ya Daraja Takatifu ya Upadre. Kumbe, mafunzo haya yanapania pamoja na mambo mengine kuwasaidia Wakleri kuadhimisha vyema Sakramenti ya Upatanisho kwa kujipyaisha katika mambo ya kitaalimungu, kisheria na maisha ya kiroho, daima wakitambua kwamba, maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho yanahitaji umakini mkubwa sana!

Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Toba ya Kitume anasema, mafunzo haya ya ndani kwa sasa yamefikia awamu yake ya XXVIII. Ni mafunzo ambayo yamekuwa yakihudhuriwa kwa namna ya pekee na Wakleri, Majandokasisi pamoja na Majaalimu kutoka vyuo vikuu vya Kipapa mjini Roma. Baada ya majiundo haya ya kina, washiriki wanatarajiwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 17 Machi 2017 majira ya mchana! Jioni kuanzia saa 11:00 kwa saa za Ulaya, Baba Mtakatifu anatarajiwa kuongoza Ibada ya Kitubio, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Wakleri watapata pia nafasi ya kuweza kuungamisha ili kuwamegea waamini huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani. Watapembua kwa kina na mapana dhambi ambazo kwa namna ya pekee kabisa zinawekwa chini ya hukumu na huruma ya Mama Kanisa.

Kardinali Mauro Piacenza atatoa mhadhara elekezi kwa kugusia amana na urithi wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, uliohitimishwa hivi karibuni, lakini huruma ya Mungu inapaswa kuendelea kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Kwa namna ya pekee, ataangalia jinsi ambavyo huruma ya Mungu inapaswa kumwilishwa katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji inayotekelezwa na Mama Kanisa.

Itakumbukwa kwamba, Idara ya Toba ya Kitume ni kitengo maalum cha Kanisa kinachojipambanua kwa ajili ya huduma kwa Mapadre waungamishaji pamoja na waamini wanaofanya toba. Padre Muungamishaji na Sakramenti ya Upatanisho; wajibu na haki ya waungamaji; mwelekeo sahihi wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya Sakramenti ya Upatanisho; vikwazo; changamoto za kimaadili, maongozi ya maisha ya kiroho; mwongozo wa toba mintarafu liturujia na shughuli za kichungaji. Makundi na hali maalum ya waamini wanaokimbilia toba na huruma ya Mungu katika maisha yao pamoja na masuala ya usawa wa kijinsia na maadili ya Kikristo! Haya ni kati ya mambo mazito yanayotolewa na viongozi wa Kanisa pamoja na wataalam waliotaalaumiwa katika Fumbo la toba na huruma ya Mungu kwa mwanadamu! Majiundo endelevu ni muhimu sana kwa Wakleri katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, ambamo changamoto mbali mbali zinaendelea kuibuliwa kila kukicha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.