2017-03-15 14:23:00

Matumaini ya Kikristo yanafumbatwa katika upendo kwa Mungu na jirani


Matumaini ya Kikristo yanafumbatwa katika furaha, dhiki na subira; kwa kudumu katika sala; kuwa kujisadaka kwa ajili ya mahitaji ya watakatifu wa Mungu; kwa kujikita katika ukarimu kwa wageni pamoja na kujibu kilio cha wahitaji. Kimsingi huu ni muhtasari wa Amri kuu ya upendo ambayo Kristo Yesu amewaachia wafuasi wake, yaani kumpenda Mungu na jirani na kwamba, huu ni wito wa hali ya juu kabisa kwa Wakristo na ni chimbuko la furaha ya matumaini ya Kikristo! Changamoto kwa waamini ni kuondokana na chachu ya unafiki katika upendo kwa kuhakikisha kwamba, upendo wao ni safi pasi na mawaa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Hii ni sehemu ya katekesi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 15 Machi 2017 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu amewataka waamini kuondokana kabisa na chachu ya unafiki inayoweza kujipenyeza kabisa hata katika upendo kutokana na madhara ya dhambi, kiasi cha kujikita katika masilahi binafsi; kwa watu kutaka kujionesha hasa kwa njia ya huduma ya matendo ya huruma; watu kutaka kushuhudia uwezo na nguvu zao kwamba ni watu wema kana kwamba, upendo ni juhudi zao binafsi. Ikumbukwe kwamba, upendo ni neema inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kukumbatiwa katika uhuru kamili na kuwashirikisha wengine uso mpole na mnyenyekevu wa Kristo, chemchemi ya upendo kamili!

Mtakatifu Paulo anawakumbusha waamini kwamba, mwanadamu ni mdhambi na upendo wake pia umechafuliwa kwa dhambi, lakini, Yesu anawatangazia matumaini mapya kwa kuwaonesha njia inayowaelekeza katika uhuru na wokovu unaowawezesha hata wao kumwilisha Amri kuu ya upendo, kiasi hata cha kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya upendo wa Mungu. Jambo hili linawezekana ikiwa kama waamini watamwachia nafasi Yesu Kristo Mfufuka katika mioyo yao ili aweze kuwaganga na kuipyaisha tena. Yesu ndiye anayewawezesha waamini kuonja huruma ya Baba wa milele kiasi hata cha kuthubutu kuadhimisha upendo wake.

Kumbe, inafahamika wazi kwamba, kile ambacho waamini wanakiishi na kukitenda kwa ajili ya jirani zao ni jibu muafaka kutoka kwa Mwenyezi Mungu anayethubutu kufanya makazi yake katika nyoyo za waja wake, ili kuwawezesha kuwa kweli ni majirani wema, tayari kuwahudumia kwa moyo mkunjufu wale wote wanaokutana nao katika hija ya maisha yao ya kila siku, kwa kuanzia na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; yaani, maskini ambao Kristo Yesu anawatambua na kuwapatia kipaumbele cha kwanza!

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Mtakatifu Paulo anataka kuwatia shime Wakristo kumwilisha ndani mwao fadhila ya matumaini, ili kweli waweze kuiishi Amri ya upendo kwa Mungu na jirani katika ukamilifu wake. Hii ni neema inayowawezesha waamini kutambua kwamba, kwa nguvu na jeuri yao binafsi hawana uwezo wa kupenda kwa dhati, kumbe, wanamhitaji Mwenyezi Mungu kupyaisha zawadi ya upendo ndani ya nyoyo zao mintarafu uzoefu na mang’amuzi ya huruma yake isiyokuwa na kifani!

Kwa njia hii, waamini wataweza kuthamini hata mambo madogo madogo na ya kawaida wanayotekeleza katika maisha yao kama njia ya kuonesha na kushuhudia upendo kwa jirani zao kama jinsi Mwenyezi Mungu mwenyewe anavyopenda; kwa kuwatakia mema, yaani waweze kuwa kweli ni watakatifu na marafiki wa Mwenyezi Mungu, kiasi hata cha kuweza kuwa na furaha kwa kuwasaidia maskini katika hali ya unyenyekevu kama ambavyo Kristo Yesu anatenda kwa kila mmoja wao hasa pale wanapokuwa mbali naye! Kwa kuwainamia wengine ili kuwapatia huduma makini kama alivyofanya Yesu, Msamaria mwema anayewaonea huruma na kuwasamehe dhambi zao.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mtakatifu Paulo amewafunulia siri ya kuwa na furaha katika matumaini katika hali mbali mbali za maisha kwani upendo wa Mungu daima unawaambata katika maisha yao. Waamini wakiwa na mioyo iliyopyaishwa kwa kutembelewa na neema ya Mungu na uaminifu wake; waamini wawe na ujasiri wa kuweza kufurahi katika matumaini, tayari kuwashirikisha hata na jirani zao, kile kidogo wanachoweza kwani daima wanapokea kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kipindi cha Kwaresima kiwe ni wakati muafaka wa kuimarisha matumaini ya Kikristo kwa kupyaisha huduma ya upendo kwa Mungu na jirani! Ni wakati muafaka wa kuboresha maisha ya kiroho na kudhamiria kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwimbia Mungu utenzi wa upendo kama ulivyoandikwa na Mtakatifu Paulo 1 Kor. 13: 4 – 7. Kwaresima ni wakati wa kumfungulia Mungu mioyo ili aweze kuwakirimia huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka. Matumaini yawasaidie waamini kumwilisha upendo usiokuwa na mawaa kwa Mungu na jirani zao.

Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza wanachama wa Chama cha Kitume cha Wafokolari wanaoadhimisha Jubilei ya miaka 50 ya uwepo na utume wao sehemu mbali mbali za dunia. Anawataka wawe kweli ni mashuhuda na vyombo vya wema, uzuri na utakatifu wa familia huku wakiongozwa na amani na upendo wa Kristo. Amevitaka vyama mbali mbali vya kitume kujenga na kuimarisha mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Vijana wa kizazi kipya, wanandoa na wagonjwa wakati wa Kwaresima wajitahidi kuwa karibu na Mwenyezi Mungu; wafunge na kuacha tabia na mazoea mabaya; wajilinde wenyewe na sala kiwe ni chakula chao cha kila siku kama njia ya kujisikia kwamba, Mwenyezi Mungu yuko kati pamoja nao! Matendo ya huruma: kiroho na kimwili yawapatie faraja pamoja na kuonesha huruma kwa jirani zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Rado Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.