2017-03-14 10:43:00

Jubilei ya Miaka 25 Parokia ya Kiabakari, Jimbo Katoliki Musoma!


Ndugu waamini wenzangu, Kanisa Takatifu lafundisha siku zote pasipo shaka lolote kwamba kila Padre (haijalishi ni mtakatifu au la - maana atahukumiwa na yeye kutokana na maisha yake na matendo yake kama kila mtu yeyote yule na utakatifu wa huduma yake hautokani na utakatifu wake bali na utakatifu wa Mungu mwenyewe na neema na baraka zake zinazowafikia waamini kupitia kwa Padre huyo) ni alter Christus, kwa kilatini - Kristo mwingine.  Katika huduma ya kiroho na ya kichungaji ya Padre, Yesu Mfufuka mwenyewe anatenda kazi yake ya Ukombozi. Anazungumza na watu wake, anawabariki, anawasamehe dhambi zao, anawatia moyo, anawaonya, anawakanya, anawatahadharisha, anawakataza na kuhamasisha - kupitia kwa nafsi ya Padre.

Tunasoma katika Injili ya Mtakatifu Luka yafuatayo - “Yesu aliwaambia: “Enendeni, angalieni, nawatuma kama wana kondoo kati ya mbwa-mwitu. Msichukue mfuko, wala mkoba, wala viatu; wala msimwamkie mtu njiani. Na nyumba yo yote mtakayoingia, semeni kwanza, Amani iwemo nyumbani humu; na akiwamo mwana wa amani, amani yenu itamkalia; la, hayumo, amani yenu itarudi kwenu. Basi, kaeni katika nyumba iyo hiyo, mkila na kunywa vya kwao; maana, mtenda kazi amestahili kupewa ujira wake. Msihame-hame kutoka nyumba hii kwenda nyumba hii. Na mji wo wote mtakaouingia, wakiwakaribisha, vileni vyakula viwekwavyo mbele yenu; waponyeni wagonjwa waliomo, waambieni, Ufalme wa Mungu umewakaribia. Na mji wo wote mtakaouingia, nao hawawakaribishi, tokeni humo, nanyi mkipita katika njia zake semeni, Hata mavumbi ya mji wenu yaliyogandamana na miguu yetu tunayakung'uta juu yenu. Lakini jueni hili, ya kuwa Ufalme wa Mungu umekaribia. Nawaambia ya kwamba siku ile itakuwa rahisi zaidi Sodoma kuistahimili adhabu yake kuliko mji huo. (…) Awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma. ” (Lk 10:3-12.16).

Basi, Neno hili la Mungu linatufunidisha kinagaubaga kwamba endapo Padre, hasa Paroko wako, akiwa anatimiza wajibu wake katika nafasi ya kuwa Kristo mwingine na kwa uaminifu kwa Neno la Mungu na mafundisho sahihi ya Kanisa na anapokuambia Neno la Mungu, anapokushauri, anapokuasa, anapokuelekeza, anapokuonya, anapokuita ofisini kwa faida ya roho yako na wokovu wako, Yesu mwenyewe anakuambia, anakushauri, anakuasa, anakuonya, anakuita.  Maana yake mafudisho haya ni nini basi?

Usije ukawa kama Herode ambaye Yohane Mbatizaji alipotumwa na Mungu kumwambia kwamba si halali kwake kukaa na mke wa ndugu yake, badala ya kutii sauti ya Mungu na kutubu na kujirekebisha, alikata kichwa chake. Yesu mwenyewe alipoletwa kwake asubuhi ya Ijumaa Kuu na hapo Herode akawa na maswali mengi ya kumhoji Yesu, Yesu hakufungua mdomo wake maana wakati wa wokovu wa Herode ulikuwa siku ile Yohane Mbatizaji alipomjia kwa niaba ya Mungu na kumwonya. Kwa vile hakutii na kukata kichwa chake, Mungu hakuwa na ziada tena kwa ajili ya Herode. Usiwe kama Herode.

Ninapokuambia si halali kwako kuishi na kutenda kinyume cha maadili ya Kanisa ulivyofundishwa kabla ya Ubatizo wako au wakati wa mafundisho ya Komunyo ya Kwanza na Kipaimara na uliapa kwa kuweka Ahadi zako za Ubatizo, ninapokuambia si halali kwako kukaa hivi na mwanamke bila ndoa, ninapokuambia si halali kwako kuingilia ndoa ya mwenzio, si halali kwako kuvunja viapo vyako vya ndoa takatifu ulivyokula mbele ya Mungu lakini hujali hayo na unazini nje ya ndoa yako, ninapokuambia kwamba si halali kwako kumfukuza mke wako halali wa ndoa nyumbani kwa sababu ya fujo zako na ubabe tu au kumwona kama mali yako na kitu cha kutumia hovyo bila upendo na heshima, ninapokuambia kwamba si halali kwako kuondoka nyumbani na kupanga gesti na kukaa na hawala yako wakati umemtelekeza mke wako na hata matumizi humpatii na hutaki kujirekebisha licha ya kushauriwa na watu wengi - ujue anayekuambia haya ni Yesu mwenyewe.

Sasa, jinsi utakavyojibu kwa ujumbe huo wa Mungu - itakufanya uwe kama Herode au kama watu wa Ninawi waliotubu na kusalimika baada ya kumwamini na kumtii Nabii Yona. Wengine baada ya Misa mtatoka na mtanisema hovyo, mtanikata kichwa kwa kunikashfu na kunitukana kwa ujeuri na kiburi kwa kusudi la kuhalalisha ubaya wenu na kujituliza katika dhamiri zenu zilizo mahututi. Ili mwendelee na tabia na hali mbaya mliyo nayo kwa sasa. Wengine mtatoka mmeguswa katika dhamiri zenu mkiwa na nia ya kufanya chochote  wakati huu wa Kwaresima na Mwaka wa Jubilei ya Parokia yetu ili hali iwe nzuri ya maisha yako na ndoa yako na uweze kupokea Sakramenti za Kanisa, lakini mkishatelemka chini na kukutana na washauri na washawishi wenu, basi nia hiyo itatoweka.

Wengine wachache watazingatia na kutubu na kujirekebisha, watafika ofisini ili waulize kama yule kijana tajiri - nifanye nini ili niurithi Ufalme wa mbinguni? Mwaka huu ni wa Jubilei ya Parokia yetu. Ni mwaka wa kufanya toba na kurekebisha mahusiano yetu na Mungu, na Kanisa, na Parokia na watu wengine. Ni mwaka wa kampeni ya ndoa takatifu.  Baba wa Huruma anamwambia kila mmoja wetu - “Yesu Kristo ni Mwanangu mpendwa, nanyi wajibu wenu ni kumsikia na kumtii Yeye”. Hapa katika Parokia yetu Yesu Kristo yumo katika kusanyiko takatifu, yumo katika Neno hali linalosomwa na kuhubiriwa, yumo katika Ekaristi, yumo katika nafsi ya Padre anayechunga kondoo wa Bwana katika wadhifa wa Yesu Kristo mwenyewe, Kuhani wa Agano Jipya.

Ninajua kwamba Neno la Mungu litokalo kinywani mwangu halitarudi bure bila kufanya kazi iliyokusudiwa na Mungu katika nafsi za wale walio tayari kulipokea. Na sitawajibika mbele ya Mungu kwa yeyote kati yenu anayekaidi Neno la Mungu na kukataa wokovu - kwa mfano kwa kukataa kurekebisha hali ya ndoa, kufunga ndoa, kupatanishwa kwa wanandoa, kuondoa vikwazo vingine na kadhalika. Utawajibika wewe mwenyewe unayesikia Neno la Mungu lakini unaruhusu kwa makusudi mazima Neno hilo lidondoke chini na kukanyagwa na nguruwe za tamaa zako, kiburi, majivuno, ukaidi na kadhalika. Yote haya ni ishara wazi za dhambi dhidi ya Roho Mtakatifu.  Unadai unafunga Kwaresima, unadai unasali, unadai wewe ni mkatoliki wa kisasa, unadai unaongozwa na Roho Mtakatifu lakini wakati huo huo unatenda dhambi dhidi ya Roho Mtakatifu kwa kukataa ushauri wa Mungu, kwa kukataa kumsamehe mwenzio, kwa kukataa kuondoa vikwazo, kwa kukataa kupunguza tamaa ya mahari na kuwazuia watoto wasifunge ndoa na kuishi katika dhambi ya mauti. Nikuiteje basi? Sina zaidi kwa leo. Mwenye masikio na asikie na kuchukua hatua zinazostahili.  Na wengine? Waandae majibu ya kuridhisha watakaposimama mbele ya Muumba wao siku ya kufa kwao. Amina.

Padre Wojciech Adam Koscieliak

Kituo cha Hija Kiabakari, Jimbo Katoliki Musoma.








All the contents on this site are copyrighted ©.