2017-03-11 07:28:00

Papa Francisko kutembelea nchini Colombia 6 - 11 Septemba 2017


Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko uliotolewa kwake na Rais Juan Manuel Santos na Baraza la Maaskofu Katoliki wa kutembelea Colombia kuanzia tarehe 6 -11 Septemba 2017. Akiwa nchini humo, Baba Mtakatifu atapata fursa ya kutembelea miji ya: Bogotà, Villavicencio, Medellìn na Cartagena. Hayo yamethibitishwa na Dr. Paloma García Ovejero, Msemaji msaidizi wa Vatican, Ijumaa tarehe 10 Machi 2017. Ratiba elekezi ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Colombia iko mbioni kutolewa hadharani.

Askofu mkuu Luis Augusto Castro Quiroga , Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Colombia kwa kushirikiana na Kardinali Rubèn Salazar pamoja na Askofu mkuu Ettore Balestrero, Balozi wa Vatican nchini Colombia wamezungumza na waandishi wa habari nchini Colombia kuhusiana na hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini humo inayoongozwa na kauli mbiu “Demos el primer paso” yaani “Tupige hatua ya kwanza”.

Huu ni mwaliko kwa familia ya Mungu nchini Colombia ya kupiga hatua katika mchakato wa ujenzi wa amani na upatanisho kwa kufuata nyayo za Baba Mtakatifu Francisko ambaye amejipambanua kuwa kweli ni “Mmissionari wa upatanisho”. Wananchi wa Colombia kwa muda wa miaka 50 wamekuwa wakipigana vita ya wenyewe kwa wenyewe, jambo ambalo liliwawagawa na kuwasambaratisha wananchi wa Colombia. Kumbe, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Colombia inapania pamoja na mambo mengine kuimarisha mchakato wa ujenzi wa haki, amani na upatanisho nchini Colombia. Ili kufanikisha mchakato huu muhimu katika maisha, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kuna haja ya kujikita katika toba na wongofu wa ndani, ili kubadilika, tayari kukutana na wengine. Huu ni wakati muafaka kwa Colombia kugundua utambulisho wake kama taifa, ili kuudumisha kwa nguvu zote bila kutoa tena nafasi ya kutoweka kwa amani, upendo na mshikamano wa kitaifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.