2017-03-11 13:40:00

Nendeni mkatafakari na kushuhudia: ukuu, utukufu na utakatifu wa Mungu


Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima inatupatia nafasi ya kutafakari tena na tena Fumbo la Pasaka yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu! Kwa maana kwa ajili ya mateso matakatifu ya Yesu Kristo, Mwana wa Baba wa milele, ulimwengu mzima umeona sababu ya kukiri: Ukuu, utukufu na utakatifu wa Mungu unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba. Waamini wanaalikwa na Mama Kanisa kutoka katika maisha ya mazoea na kuanza safari ya kutembea katika sheria ya Bwana, ili hatimaye, waweze kumshuhudia Kristo Yesu, Mwana wa Baba wa mbinguni, kwa kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, amani na maridhiano.

Ili kutekeleza yote haya waamini wanaalikwa kumsikiliza na kumkiri Yesu katika: Imani inayoungamwa na Mama Kanisa; Imani inayoadhimishwa katika Sakramenti za Kanisa, Imani inayomwilishwa katika Sheria na Amri za Mungu; hii ni imani inayofumbatwa katika ile Sala kuu ya Baba Yetu wa mbinguni pamoja na Zaburi; Imani hii inapaswa kushuhudiwa na wote.

Ndugu msikilizaji, Yesu alipokuwa anajiandaa kwa ajili ya kukabiliana na Fumbo la Msalaba, aliwachukua Mitume wake: Petro, Yohane na Andrea kwenda kushuhudia jinsi alivyogeuka sura ili kuonesha; ukuu, utukufu na utakatifu wake kwamba, kweli alikuwa ni Mwana wa Mungu, Masiha na Mkombozi wa dunia. Huu ni utimilifu wa Sheria, Torah na Unabii ulioaguliwa tangu Agano la Kale. Huu ni utukufu unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba. Yesu anatumia nafasi hii kuwaandaa ili hatimaye hata wao kwa wakati muafaka waendelee kuwa ni mashuhuda amini wa ukuu, utukufu na utakatifu wa Mungu kwa watu wanaowazunguka.

Mwinjili Mathayo anaonesha jinsi ambavyo Mitume hawa walivyofurahia kufunikwa na utukufu wa Mungu, kiasi hata cha kutamani kuendelea kukaa hapo hapo huku wakimwabudu na kumtukuza Mungu na kudhani kwamba, huo ulikuwa ni mwisho wa safari! Lakini, Yesu akawaambia, baada ya kushuhudia yote haya, sasa inukeni msiogope! Anawakumbusha kwamba, hakuna njia ya mkato! Yesu Kristo ni utimilifu wa ufunuo wa: ukuu, utukufu na utakatifu wa Mungu; unaofumbatwa kwa namna ya pekee katika Fumbo la Msalaba, kielelezo cha hekima, huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani!

Changamoto ni toba na wongofu wa ndani na kuendelea kuboresha ile neema ya utakaso waliyoipata wakati wa Sakramenti ya Ubatizo kwa: kufunga na kusali; kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha pamoja na kukita maisha katika Sakramenti za huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili! Mwenyezi Mungu ndiye lile Jua la haki, mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano kati ya watu, ili kweli utukufu na ukuu wa Mungu uweze kung’ara tena kati ya watu wa Mungu, ili kuwa tayari kutembea tena katika mwanga wa Kristo Mfufuka.

“Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, inayependezwa naye; Msikieni yeye! Kusikiliza maanaye yake ni kusadiki kwamba, Yesu aliyezaliwa, akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu ni Mwana mpendwa Mungu na Mkombozi wa ulimwengu. Yesu ni kiini cha imani ya Kanisa inayopaswa kumwilishwa na kushuhudiwa kama ilivyokuwa kwa Petro, Yohane na Yakobo, sasa ni changamoto kwa Wakristo wote; dhamana wanayoweza kuitekeleza kwa kujivika tunu msingi za Kiinjili, tayari kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu na hatimaye, maisha ya uzima wa milele. Baba Mtakatifu Francisko anatualika katika kipindi cha Kwaresima: kusoma, kutafakari na kumwilisha ile sehemu ya Injili ya Lazaro maskini na tajiri asiyejali wala kuguswa na mangaiko yaw engine. Kusikiliza ni kuguswa na shida, mateso na mahangaiko yaw engine, tayari kuyapatia majibu muafaka!

Ibrahimu Baba wa imani ni kielelezo cha neema na baraka ya Mungu kwa watu wake, kwani alithubutu kujiachilia mikononi mwa Mungu ili kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yake. Huu ni mwaliko wa kuitika, kuvumilia, kumsikiliza Mungu na kumwachia nafasi ili aweze kutuongoza katika sheria na unabii, ili kuutafakari: ukuu, utukufu na utakatifu wa Mungu; tayari kuushuhudia katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo cha imani tendaji! Tumwombe Mwenyezi Mungu neema ya kusikiliza, kukiri na kushuhudia ukuu, utukufu na utakatifu wa Mungu kwa wale wanaotunguka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.