2017-03-10 10:04:00

Utekelezaji wa mkataba wa amani DRC ni dira na matumaini ya wengi!


Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Watu wa Congo, DRC linaendelea kuonesha wasi wasi na hofu kubwa juu ya mustakabali na hatima ya nchi yao kutokana na Serikali pamoja na vyama vya upinzani kushindwa kutekeleza mkataba wa amani uliotiwa mkwaju, mwishoni mwa Mwezi Desemba, 2016! Kushindwa kutekelezwa kwa mkataba huu kunaweza kuitumbukiza DRC katika majanga makubwa ya uvunjivu wa amani na utulivu. Tangu tarehe 1 Februari 2017 alipofariki kigogo wa upinzani huko Brussels, Ubelgiji, Bwana Etienne Tshisekedi, mchakato wa mageuzi nchini DRC ukasimama, kiasi hata cha kuanza kuzua hofu na mashaka. Kuteuliwa kwa Bwana Felix Tshisekedi, Mtoto wa Hayati Etienne Tshisekedi kuongoza vyama vya upinzani kumepokelewa kwa hisia tofauti sana na wapenda amani nchini DRC.

Itakumbukwa kwamba, DRC ilipaswa kufanya uchaguzi mkuu mwishoni mwa Mwezi Desemba 2016 ikashindikana, Rais Joseph Kabila akaliomba Baraza la Maaskofu Katoliki DRC kusaidia mchakato wa upatanisho ili kulinda demokrasia, haki, amani, ustawi na mafao ya wengi. Muafaka ukafikiwa kati ya Serikali na vuguvugu la upinzani “Rassemblement” hapo tarehe 31 Desemba 2016. Dhamana ya Kanisa Katoliki katika mchakato wa upatanisho kati ya Serikali ya Joseph Kabila na vuguvugu la upinzani umepelekea vitendo vya kufuru kwa baadhi ya Makanisa nchini DRC, kitendo ambacho kimeshutumiwa sana na Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, kwani amani, maridhianao, upatanisho na umoja wa kitaifa ni kwa mafao ya wananchi wote wa DRC na wala si kwa ajili ya Kanisa peke yake!

Umoja wa Mataifa ulishutumu sana vitendo hivi vya kihuni vinavyotaka kuitumbukiza DRC katika machafuko ya kisiasa yanayoweza kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao! Maaskofu wanakaza kusema, amani ikitoweka ni vigumu sana kuweza kuirejesha tena katika akili na nyoyo za watu! Kumbe, jambo la msingi kwa wakati huu ni kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na utekelezaji wa Mkataba wa Amani uliotiwa sahihi mwishoni mwa Mwezi Desemba 2016, ili Serikali ya mpito chini ya Rais Kabila iweze kuundwa na kuanza kushughulia mchakato wa uchaguzi mkuu ambao ulipaswa kufanyika mwishoni mwa Mwaka 2017, lakini kwa sasa kunaonekana kwamba ndoto hii, pengine isitekelezwe kwa wakati muafaka!

Baraza la Maaskofu Katoliki DRC linawataka wanasiasa nchini DRC kujenga utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wote wa DRC, ili kuweza kutekeleza Mkataba wa Amani ambao ni matumaini ya wanachi wa DRC. Wanasiasa waaminiane, waheshimiane na kuthaminiana ili kweli makubaliano yatakatofikiwa yawe ni kwa ajili ya ustawi na demokrasia nchini DRC.

Kucheleweshwa kwa mchakato wa uchaguzi mkuu ni mchezo mchafu unaoweza kuleta maafa makubwa kwa wananchi wa DRC wanasikitika kusema Maaskofu. Wanasiasa pamoja na Serikali ya Rais Joseph Kabisa waoneshe ukomavu wa kisiasa, demokrasia ya kweli na maendeleo ya wengi kwa kuendeleza mchakato wa uundwaji wa Serikali ya mpito ili kurejesha amani, ustawi na umoja wa kitaifa nchini DRC, chachu makini ya ustawi na maendeleo ya wengi dhidi ya chuki na uhasama vinavyotaka kuwapekenya wananchi wa DRC, ili hatimaye, wasambaratike, ili wachache waendelee kula “kuku kwa mrija” hata kama kuna watu wanaoteseka na kumwaga damu isiyokuwa na hatia nchini humo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.