2017-03-08 15:10:00

Yesu Kristo ni utimilifu wa Sheria na Unabii!


Ndugu zangu, karibuni tena tusikilize na kutafakari pamoja neno la Bwana dominika hii ya pili ya kipindi cha kwaresima.  Katika somo la kwanza, tunasikia habari juu ya utii wa Abrahamu kwa mwito wa Mungu na itikio lake linakuwa wokovu kwake na kwetu. Mtu mmoja akiokoka ni roho nyingi pia zinaokoka.  Katika somo la pili, Mtume Paulo anaongea juu ya uvumilivu unaovuta heri – mvumilivu hula mbivu kama wanavyosema waswahili. Kwa njia yake Kristo, sisi tumekombolewa. Yesu ametuita kwa wito mtakatifu, si kadiri ya matendo yetu bali kwa neema yake,  kwa njia yake tumepata uzima.

Somo la injili latoka sehemu ambayo twasoma kila jumapili ya  pili ya kwaresima – kung’ara sura Bwana. Tendo hili linafanyika mbele ya mitume watatu – Petro, Yakobo na Yohane hawa wanauona ufunuo wa Mungu katika utimilifu wake. Kwa hakika mitume hawaoni tu huo utukufu mara moja au katika lile tukio tu pale, bali wanapata pia ufunuo wa kile kitakacho kuja hapo baadaye. Huku kung’ara sura, huo ufunuo, ni changamoto, ni tendo takatifu – linatuamsha sisi. Ni msukumo tuone pia upendo na ukuu wa Mungu kwetu. Ni ukumbusho kwamba mahusiano yetu na Yesu, yaani utimilifu wake u mbinguni. Inatukumbusha haja ya kuangalia upya uwepo wa Mungu, ni mwaliko wa kubadilika na ndiyo lengo la kwaresima.

Kuga’aa kwetu sisi huanzia na sakramenti ya ubatizo. Huu ndio mwanzo wa mabadiliko na hitaji la kung’aa kwetu. Kwa ubatizo tunakuwa wenyeji wa jumuiya ya kikristo. Kwa sakramenti ya ubatizo tunamvaa Kristo na tunakuwa watu wake Kristo.

Kwa Sakramenti ya ubatizo, mwanadamu anapata nafasi ya kuanza upya. Hii nafasi iko wazi mbele ya Mungu. Tazama somo la kwanza juu ya habari ya wito wa Abrahamu. Angebaki katika hali yake asingeupata wokovu wa Mungu, asingepata upendeleo wa Mungu. Kwake ilikuwa ni mshangao, lakini pia kwake na kwetu inakuwa ni changamoto katika kuelewa mpango wa Mungu katika maisha yetu!

Kwa kifupi, tunaona kuwa mpango wa Mungu wa ukombozi wetu ndiyo ukamilifu wetu na kinyume chake ni maafa. Sura 11 za kwanza katika  Kitabu cha Mwanzo zinaonesha  maangamizi matupu.  Mwanadamu anapobaki peke yake anaangamia. Mungu alipoingilia kati, kuanzia sura ya 12, mara wokovu ukapatikana. Tunaelewa wazi kuwa, ili kupata wokovu ni lazima Mungu aingilie kati lakini pia ni lazima mwanadamu aitike wito huu. Matokeo yake ni neema ya Mungu kuonekana. Abrahamu anaitika na Mungu anambariki. Historia ya maisha ya mwanadamu inabadilika. Badala ya maangamizi unapatakina wokovu.

Huku kung’ara sura katika Somo la Injili, kunatupatia nafasi kusikia habari juu ya ukuu wa utukufu wa Mungu unaoonekana wazi. Musa anawakilisha Sheria, Torah na Eliya anawakilisha manabii. Hawa ndio walioandaa njia kwa ujio wa Kristo. Petro na wenzake wanasujudu ukuu wa Mungu. Mwanadamu akimwabudu Mungu, tayari anashiriki kwenye tendo la wokovu. Mungu anapotuokoa, tayari anaonesha utukufu wake ulio wa kuabudiwa. Kung’ara kwake sura Yesu ni tangazo la utukufu uliokuwepo, uliopo na utakaokuja ambao ni wake kwa vile ametuokoa kwa kifo na ufufuko wake. Uwepo huo wa Mungu kwetu ndio unaotubadilisha. Jibu letu ni kusadiki.

Katika Injili tunasikia sauti ya Mungu ikisema – huyu ni mwanangu mpendwa, msikilizeni yeye. Huu ni wito kwa mfuasi kumsikiliza mwana wa Mungu. Inaonekana kuwa wale mitume watatu hawakutambua mpango wa Yesu – kwamba ilibidi ateswe, afe na afufuke. Ilibidi awapatie nafasi ya pekee mlimani na awafunulie zaidi siri za mbinguni – waliposikiliza vizuri walielewa. Hapa ikaongezeka zaidi, siyo kusikia tu bali pia kusadiki.

Huu ndio mwaliko uliopo mbele yetu wa mabadiliko ya ndani, ya moyo, akili, masikio n.k.  Leo tunaalikwa tutoke katika mazingira yetu, twende mlimani, tukakae pamoja na Yesu, tumsikilize, tena ili tupate kumsadiki. Tunaalikwa tutoke katika mazoea yetu hasa yale ambayo hayana tija kimwilil wala kiroho. Hatuna budi kujiangalia vizuri na kuona sura zetu na mfanano wake. Tuangalie vizuri kama kweli sura zetu zina mfanano wa kimungu. Tunaalikwa kama Abrahamu leo kutoka katika himaya zetu na kwenda kwenye himaya ya Mungu, mahali papya na makao mapya.

Kipindi cha Kwaresima ni muda wa kuangalia upya ufuasi wetu na kuutambua huruma na upendo wa Mungu ambaye anatualika: kutubu, kuongoka ili tubalidilike, tung’ae, tuanze upya, tumvae roho wa Mungu, ili hatimaye, tuweze kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Anatualika tubadilike katika maisha yetu na kujenga mahusiano mapya na Mungu pamoja na jirani zetu kama kielelezo makini cha imani tendaji! Haitoshi kufunga, kusali na kulitafakari Neno la Mungu linalotupasha kuhusu ukuu na utakatifu wa Mungu, bali Neno hili linapaswa kumwilishwa katika matendo ya huruma; kielelezo makini cha imani tunayoiungama yaani: Kanuni ya Imani, Imani tunayoiadhimisha, yaani Sakramenti za Kanisa, Imani tunayojitahidi kuuishi, yaani Amri za Mungu na hatimaye, Imani tunayoisali, yaani Sala ya kuu ya Kanisa, Baba Yetu na Masifu! 

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.