2017-03-08 14:27:00

Kanisa kuendelea kusimama kidete kulinda na kutetea utu wa wakimbizi


Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani na Baraza la Maaskofu Katoliki Mexico baada ya mkutano wao uliofanyika hivi karibuni ili kupembua kwa kina na mapana sera na mikakati ya kisiasa kuhusu changamoto ya wahamiaji, inayokabiliwa na hali ngumu kwa wakati huu, wanasema, wahamiaji na wakimbizi wanayo haki ya kuheshimiwa na kuthaminiwa. Kanisa litaendelea kujizatiti kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, ustawi na mafao ya wakimbizi na wahamiaji. Kanisa linapania kuboresha huduma kwa wakimbizi, wahamiaji pamoja na familia zao katika maisha ya kiroho, kimwili na kisheria.

Mkutano wa Maaskofu kutoka Marekani na Mexico ulipachikwa jina “Tex-Mex”. Katika mkutano huu, Maaskofu wamesikitishwa na hali ya kutojali changamoto ya wakimbizi na wahamiaji kwa kuwageuzia kisogo watu wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Maaskofu wameshuhudia mateso na mahangaiko ya wakimbizi hawa kutokana na sera na mikakati ya kisiasa yenye mwelekeo wa kibaguzi, hali ambayo imepelekea mapambano kati ya wahamiaji na wakimbizi pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama.

Kumekuwepo na idadi kubwa ya wahamiaji na wakimbizi waliorudishwa makwao kwa nguvu na vitisho, hali ambayo inakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu. Maaskofu wanasema, kumekuwepo na mshikamano wa dhati kati ya wananchi wanaoishi kwenye mipaka ya Mexico na Marekani, kwa Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki, Caritas kuwa mstari wa mbele katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji. Maaskofu wanasema, wataendelea kumuunga mkono Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni na madaraja ya watu kukutana na kusaidiana badala ya ujenzi wa kuta za utengano zinazofumbata sera za ubinafsi na ubaguzi wa watu, mambo ambayo ni kinyume kabisa cha haki msingi za binadamu, utu na heshima ya watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu!

Mkutano huu, umekuwa ni kielelezo cha mshikamano wa upendo, furaha na matumaini kati ya Maaskofu wa Marekani na Mexico, ili kuendeleza umoja na matumaini kama alivyofanya Baba Mtakatifu Francisko mwezi Februari 2016 kwa kutembelea maeneo ya mpakani kati ya Marekani na Mexico. Mkutano huu ulitishwa na Maaskofu hawa ili kujibu changamoto inayotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu sera na siasa zake kuhusu wakimbizi na wahamiaji na kwamba, anadhamiria kujenga ukuta mkubwa utakaotenganisha nchi hizi mbili na kwamba, anapania kuwarejesha mamilioni ya wahamiaji na wakimbizi makwao, tukio ambalo halijawahi kutendeka nchini Marekani.

Lakini, Maaskofu wanakumbusha kwamba, ustawi na maendeleo makubwa ya Marekani kwa wakati huu ni matunda na jasho kubwa lililotolewa na wahamiaji na wakimbizi kutoka sehemu mbali mbali za dunia waliopewa hifadhi, wakathaminiwa na hatimaye, wakajisadaka kwa ajili ya maendeleo ya Marekani kama yanayoonekana hivi sasa! Mkutano huu umekuwa ni fursa ya kujikumbusha tena na tena changamoto iliyotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuhusu mkutano wa “Tex-Mex” kunako mwaka 1986.

Ni mkutano uliopembua kwa kina na mapana changamoto ya wahamiaji na wakimbizi, biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; magenge ya uhalifu wa kimataifa; ukarimu na upendo unaojionesha kwa ujenzi wa makazi ya wahamiaji pamoja na sera mbali mbali za shughuli za kichungaji zilizotekelezwa na Maaskofu wa Marekani na Mexico ili kujibu changamoto hizi. Changamoto ya wakimbizi na wahamiaji ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa wanasema Maaskofu Katoliki kwani hata Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ilionja suluba ya kuishi uhamishoni, ili kulinda na kutetea maisha ya Mtoto Yesu aliyekuwa anatafutwa na Mfalme Herode. Wakimbizi na wahamiaji ni watu wanaotafuta hifadhi ya maisha, fursa za kazi na ajira, ili kuboresha maisha yao. Hawa ni watu wanaokimbia vita, dhuluma, nyanyaso, majanga asilia na umaskini wa hali na kipato, kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao! Kumbe, Maaskofu wanasema, wakimbizi na wahamiaji wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa kwa kulinda na kudumisha haki zao msingi, utu na heshima yao kama binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.