2017-03-07 08:34:00

Kwaresima: Kipindi cha kutunza mazingira na huduma kwa jirani!


Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, ni wakati mwingine tena wa kujikumbusha  mambo muhimu katika maisha yetu, na la msingi zaidi ni kwamba, sasa tuko katika kipindi cha Kwaresima, kipindi ambacho kila mmoja wetu anatakiwa kujikita zaidi katika maisha ya sala, kufunga, kufanya matendo ya huruma  na kuzama zaidi katika tafakari ya Neno la Mungu. Hivyo leo hii nakualika ndugu msikilizaji upate kutafakari ujumbe  wa Kwaresima kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko unaoongozwa na kauli mbiu “Neno ni zawadi; jirani yako ni zawadi pia”.

Katika kipindi hiki cha Kwaresima twakumbushwa kushirikishana sana zawadi ya ulimwengu katika uumbaji, na zawadi hii ya ulimwengu  ni  ya watu wote na inahitaji  kutunzwa, tazama Mungu baada ya kuona vyote kuwa ni vyema, alimuumba mwanadamu ilia apate kuvitawala  vitu vyote. Sasa ni jukumu la mwanadamu kufurahia uumbaji huu kwa kuwajibika zaidi katika kuulinda, kuutunza na kuhudumisha. Tukumbuke pia mwandamu hakuumbwa mwenyewe, bali aliumbwa na mwenzake, na hili ni  jukumu la kupokeana na kupendana wenyewe kwa wenyewe kama sehemu ya uumbaji, huu ni ujumbe mzito na makini sana wakati huu wa Kwaresima. Katika hili, hebu tuangalie ule ujumbe wa  mtu tajiri na maskini lazoro katika Biblia Takatifu.  Hapa yule maskini Lazaro anaelezewa kiundani akiwa katika hali duni sana, akiwa hana nguo, vidonda vikiwa vimemwandama na hana chakula bali hutegemea tu makombo  yaangukayo katika meza ya yule tajiri. Lakini huyu ni mtu ana utu na utambulisho wake kama binadamu!

Katika mfano huu, tutafakari zaidi namna ya kupokeana na kusaidiana sisi kwa sisi,  wote tukiwa kama  viumbe wa Mungu. Na hili ni agizo la Mungu la kupokeana na kusaidiana, na pia ni ujumbe wa tafakari wa kipindi hiki cha Kwaresima.  Yule tajiri baada ya kifo chake anapata ujira wake kwa kukosa Mbingu, kwa sababu hakushirikisha alichokua nacha, bali yule  maskini Lazaro anapata thawabu mbinguni,  na  hili likiwa ni kwa  sababu ya  unyenyekevu wake, na mateso aliyoyapata angali hapa duniani. Kumbe, kila mmoja ni zawadi kwa mwingine, kila mmoja ampokee mwingine kama alivyo  na siyo kama  mgeni asiyejulikana. Kupokeana na kusaidiana huku kutajidhihirisha katika upendo, upendo kwa  mwanadamu na ulimwengu mzima.  Katika kusaidiana huku tunapata kuishi kiundani zaidi  kile kipengele cha matendo ya huruma. tutambue kuwa wapo wengi ambao hawana nguo, chakula wala malazi. Hawa ni wahitaji, tuwafikie kwa huruma na upendo na kupata kuwasaidia  katika hali yao hiyo duni na kufanya hivi ndio kushirikishana zawadi za uumbaji na wote tutapata fika mbinguni.

Katika hilo pia, zawadi ya ulimwengu  ni muhimu sana, wazazi wetu wa kwanza Adamu na Eva, walikabidhiwa Paradiso, ili kupata kuilinda, kadhalika ni jukumu la kila mmoja wetu  kupata kuieshemu kazi ya Mungu , kwa    kuipa heshima  na kutunza  viumbe vya ulumwengu huu, mazingiza na  wanyama wa ulimwengu huu. Katika kutambua umuhimu wa wenzetu na ulimwengu, basi kipindi hiki cha kwaresima chautualika kufungua mlango kwa wenzetu , hasa kwa wanaohitaji. Tufungue mioyo yetu kuwapokea wote kwani kila mmoja amejivika uso wa Yesu. Neno la Mungu lituwezeshe kuona na kutambua huruma hii ya Mungu katika kupokea na kupenda maisha, kuwasaidia  wanyonge na waliojeruhiwa.

 

Kutoka katika Stidio za Radio Vatican, ni mimi Padre, Agapiti Amani, ALCP/OSS.








All the contents on this site are copyrighted ©.