2017-03-07 08:04:00

Familia ya Mungu Ghana yawekwa wakfu kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu!


Katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 40 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Ghana na Vatican sanjari na miaka 60 ya uhuru wa Ghana, Kardinali Giuseppe Bertello, mwakilishi wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya, Jumamosi, tarehe 4 Machi 2017 ameiweka wakfu familia ya Mungu nchini Ghana chini ya ulinzi na tunza ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, chemchem ya huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa waja wake. Kumbe, waamini wanahamasishwa kuwa na huruma na mapendo kama Baba yao wa mbinguni alivyo!

Kardinali Bertello amesifia na kupongeza mafanikio makubwa yaliyopatikana nchini Ghana katika kipindi cha miaka 60 tangu ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Mwingereza. Demokrasia imejengeka na kuimarika kwa kiasi kikubwa; kumekuwepo na ukuaji na maendeleo makubwa katika medani mbali mbali za maisha ya kijamii na kiuchumi; mahusiano ya kitaifa, kikanda na kimataifa yameimarika zaidi kiasi cha kusaidia kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Licha ya matatizo na changamoto zilizojitokeza katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru, Ghana imeendelea kuwa aminifu kwa kanuni na misingi yake inayojikita katika utu na heshima ya binadamu!

Kardinali Bertello katika Ibada ya Masifu ya Jioni, ametumia fursa hii kuiweka wakfu familia ya Mungu nchini Ghana chini ya ulinzi na tunza ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kama ilivyokuwa tarehe 3 Machi 1957, siku chache tu kabla ya Ghana haijajipatia uhuru wake kutoka kwa Mwingereza. Waamini wamekumbushwa kwamba, kwa tukio hili la kuwekwa wakfu, Mwenyezi Mungu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na vipaumbele vyake, Kristo Yesu akiwa ni dira na mwongozo katika mchakato mzima wa maisha yao. Kama ilivyokuwa wakati wa kupigania uhuru, wananchi wa Ghana walipomkimbilia Kristo Yesu kwa moyo wa unyenyekevu, ili aweze kuwalinda na kuwaongoza, bali waendelee kumtumainia katika maisha yao!

Kardinali Bertello anasema, alibahatika kuwa Balozi wa Vatican nchini Ghana akashuhuduia uchaji wa Mungu uliooneshwa na familia ya Mungu nchini humo; akajionea mwenyewe utajiri na uzuri wa Ghana; akaguswa sana na ukarimu pamoja na upendo wa wananchi wa Ghana kwa Kanisa, hali ambayo iliendelea kusaidia ujenzi wa umoja na urafiki kati ya watu. Katika mahubiri yake, Jumapili ya kwanza ya Kwaresima, amewataka waamini nchini Ghana kutambua uwepo wa Mwana wa Mungu katika hija ya maisha yao ya kiroho, ili kweli aweze kuwakomboa kutoka katika vishawishi vya Ibili, ili kamwe wasimezwe na malimwengu.

Waamini wanapaswa kuyatafsiri matukio mbali mbali ya maisha yao kwa mwanga wa Injili; wajenge utamaduni wa kusoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha yao kama njia ya kudumisha majadiliano ya kina na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala na tafakari ya Neno la Mungu. Ili kuweza kufanikisha azma hii, kuna haja kwa waamini kutafuta muda muafaka na nafasi ya kuweza kuingia katika jangwa la maisha yao ya kiroho, ili kumpatia Mungu na nafasi. Changamoto kubwa hapa anasema Kardinali Bertello ni kujenga moyo thabiti wa kupambana na vishawishi, dhambi na mazingira yanayoweza kuwatumbukiza katika dhambi na hivyo kuvuruga uhusiano wao na Mwenyezi Mungu. Neno la Mungu linapaswa kumwilisha katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha Imani tendaji bila kusahau kutoa na kupokea msamaha kama sehemu ya hija ya upatanisho wa kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.