2017-03-06 11:31:00

Mitandao ya kijamii na diplomasia ya Vatican


Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano yanaendelea kurahisisha mawasiliano kati ya taasisi na wadau wake; kati ya viongozi na raia wake; kati ya Kanisa na waamini wake. Kanisa daima limejitahidi kuwa kati pamoja na watu kwa njia ya mawasiliano makini yanayogusa vipaumbele vya maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Kutokana na changamoto hii, ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwa ni kinara katika teknolojia ya mawasiliano ya jamii kwa kutumia mitandao ya kijamii ili kufikisha ujumbe wake. Haya yamesemwa hivi karibuni na Monsinyo Lucio Adrian Ruiz, Katibu mkuu wa Sekretarieti ya Mawasiliano Vatican wakati wa uzinduzi wa warsha juu ya “mitandao ya kijamii na diplomasia ya Vatican”.

Hili ni tukio ambalo liliandaliwa kwa namna ya pekee na Ubalozi wa Uingereza mjini Vatican kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Mawasiliano Vatican. Warsha hii imehudhuriwa na wadau mbali mbali wanaojihusisha na tasnia ya habari za kidigitali ndani na nje ya Kanisa. Washiriki hawa wametumia fursa hii kupembua kwa kina na mapana mchango wa mitandao ya kijamii katika uwanja wa mawasiliano pamoja na kuangalia uwezekano wa taasisi kuwasiliana kwa njia ya mifumo ya kisasa ya mawasiliano ya jamii, baada ya mitandao ya kijamii kushika kasi ya ajabu katika mawasiliano katika ulimwengu mamboleo!

Wajumbe wa warsha hii wamekiri kwamba, Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, anagusa akili na nyoyo za watu wengi. Hadi sasa katika akaunti yake ya twitter ana wafuasi milioni 32 wanaopata ujumbe wake katika lugha tisa za kimataifa. Kwa mtazamo huu, Baba Mtakatifu Francisko ni kinara katika mitandao ya kijamii, dhana ambayo imeungwa mkono na washiriki wa semina hii, kwani huu ni ujumbe unaowafikia waamini na wale wasioamini, kwani mara nyingi Baba Mtakatifu anagusia changamoto zinazowakabili watu katika ulimwengu mamboleo: kiroho na kimwili.

Mheshimiwa Sally Axworthy, Balozi wa Uingereza mjini Vatican akizungumza na Radio Vatican anakaza kusema, mawasiliano kwa njia ya mfumo wa kidigitali yanaendelea kushika kasi ya ajabu na muhimu sana katika mahusiano ya kidiplomasia. Kumbe, bado kuna maeneo ambayo kwa njia ya mitandao ya kijamii, Vatican na diplomasia katika medani za kimataifa yanaweza kuendelezwa kama njia ya ushirikiano wa kimataifa kama inavyoonekana na kushuhudiwa na Baba Mtakatifu Francisko. Mitandao ya kijamii ni nyenzo muhimu sana ili kuwafikia watu wengi zaidi na kwa wakati mmoja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.