2017-03-06 10:51:00

Hali ya mapato na matumizi ya Vatican inaendelea kuimarika!


Sekretarieti ya Uchumi Vatican katika taarifa yake kwa vyombo vya habari inaonesha kwamba katika kipindi cha fedha cha Mwaka 2015, Vatican pamoja na taasisi zake zote iliweza kupata faida ya kiasi cha Euro milioni 12.4. Mchango mkubwa ni ule unaotolewa na Makanisa mahalia mintarafu Sheria za Kanisa 1271. Majimbo yaliweza kuchangia jumla ya Euro milioni 24 na kiasi cha milioni 50 kilitolewa na Benki kuu ya Vatican, IOR, inayojihusisha na huduma kwa mashirika ya kitawa na shughuli za Uinjilishaji unaofanywa na Kanisa la Kiulimwengu. Matumizi makubwa ya Vatican yanatokana na gharama za watumishi wake kama ilivyokuwa hata kwa miaka mingine.

Takwimu zinaonesha kwamba, Vatican iliweza kukusanya kiasi cha Euro milioni 59.9 katika kipindi cha Mwaka 2015 na kwamba, fedha hii ni makusanyo makubwa kutoka katika Makumbusho ya Vatican. Taarifa hii ni matokeo ya Sera za Udhibiti wa Fedha za Vatican iliyopitishwa na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2014, kwa kuongozwa na Kanuni za Udhibiti wa Fedha ya Umma Kimataifa. Sekretarieti ya Uchumi ya Vatican imekwisha toa taarifa kwa Baraza la Uchumi la Vatican kuhusu mwenendo mzima wa sera za udhibiti wa fedha za Kanisa, unaotarajiwa kukamilika katika kipindi cha miaka michache ijayo, ili kuwa na udhibiti mkalifu wa fedha za Kanisa.

Baraza la Uchumi la Vatican limepongeza hatua mbali mbali zinazoendelea kuchukuliwa na Sekretarieti ya Uchumi Vatican, kiasi kwamba, mafanikio yameanza kuonekana tangu mwaka 2015, Baba Mtakatifu Francisko alipopitisha mchakato wa mageuzi makubwa katika Sekretarieti ya Vatican. Vigezo vikuu ni huduma makini, ukweli, uwazi na nidhamu katika masuala ya fedha za Kanisa. Kumekuwepo pia na mafanikio makubwa katika mchakato wa kuandaa bejeti ya Vatican na taasisi zake. Kwa mara ya kwanza katika historia, bajeti ya mwaka 2017 tayari imekwisha kutolewa kabla ya kuanza mwaka rasmi pamoja na kupitishwa na Baraza la Uchumi Vatican, tayari kwa utekelezaji wake. Udhibiti wa matumizi ya fedha za Kanisa utaendelea kufanyika ili kuhakikisha kwamba, kiwango cha bajeti kilichotengwa kinaheshimiwa. Baraza la Uchumi la Vatican limeipongeza Sekretarieti ya Uchumi ya Vatican kwa kujitoa na kujisadaka kwa ajili ya kuendeleza mchakato wa mageuzi yaliyopitishwa na Baba Mtakatifu Francisko ili kuboresha huduma ya Kanisa la Kiulimwengu kwa kuzingatia nidhamu, tija, weledi na ufanisi mkuu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.