2017-03-04 16:28:00

Yaliyojiri katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya Tanzania


Jumla ya watumishi wa umma 2,059 wamekwisharipoti Dodoma katika awamu ya kwanza ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli aliyoitoa wakati akikabidhiwa uenyekiti wa CCM, Julai 22, mwaka jana. Awamu ya kwanza ya Serikali kuhamia Makao Makuu Dodoma inajumuisha Mawaziri na Manaibu wao, Makatibu Wakuu na manaibu wao, baadhi ya wakurugenzi pamoja na wasaidizi wachache. Hayo yamebainika Ijumaa, Machi 3, 2017 katika Kikao cha Kazi cha Mawaziri na Naibu Mawaziri kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Hazina mjini Dodoma chini ya uwenyekiti wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. Katika mkutano huo, Waziri Mkuu aliwataka Mawaziri wote watoe taarifa za idadi ya watumishi wao waliohamia Dodoma hadi sasa, wamepanga kufanya zoezi hilo kwa awamu ngapi na lini watakamilisha zoezi hilo. Pia Mawaziri hao walitakiwa kueleza mahali zilipo ofisi zao kwani amepanga kuwatembelea na kuzungumza na watumishi.

Wakiwasilisha taarifa hizo, Mawaziri hao wote wamethibitisha kwamba tayari ofisi zao na wao wenyewe wameshahamia Makao Makuu Dodoma pamoja na watumishi wao wote walioko kwenye awamu ya kwanza na wameahidi kukamilisha kuhamisha waliosalia katika awamu nne hadi sita kulingana na ratiba ya Serikali. Aidha, Waziri Mkuu amesema baada ya Serikali kukamilisha ratiba ya kuhamia Makao Makuu Dodoma, Jiji la Dar es Salaam litabakia kuwa Jiji la kibiashara na wamepanga kuendelea kuliboresha ili shughuli hizo zifanyike kwa ufanisi zaidi.

Mapema, akizungumza na waandishi wa habari wakati akifungua kikao hicho, Waziri Mkuu alisema kati ya Julai 2016 na Januari 2017, Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya iliwakamata watu 11,303 ambao wanatuhumiwa kujihusisha na uzalishaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya. Alisema kati ya hao, watu 9,811, walikutwa na kesi za kujibu ambapo 9,174 wametiwa hatiani, 238 hawakukutwa na hatia na wengine 478 upelelezi wa kesi zao unaendelea. Pia alisema tangu Tume mpya iundwe Februari mwaka huu, jumla ya watuhumiwa 79 wametiwa mbaroni na uchunguzi wa kesi zao unaendelea. “Wengi kati ya hao, wameshikwa na vithibitisho, ingawa uchunguzi wa kesi zao bado unaendelea. Na hawa ni wale waliokamatwa na dawa za viwandani kama heroine na cocaine. Hatujawaingiza wale waliokamatwa na mirungi au bangi. Bado mikoa inaendelea na kazi, na hii operesheni ni ya nchi nzima,” alisema.

Uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao chimbuko lake ni agizo lililotolewa Oktoba Mosi, 1973 kwenye Mkutano Mkuu wa 16 wa chama cha TANU. Tangu wakati huo Serikali zote ziliendelea kufanya juhudi mbalimbali za kuandaa miundombinu na hata awamu ya nne ilisimamia kwa kiwango kikubwa uwekaji wa miundombinu hiyo. Serikali ya awamu ya tano iliamua kuhamia Dodoma baada ya kuridhishwa na ujenzi wa miundombinu na maeneo ya kutolea huduma za kijamii kwa wageni na wenyeji.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU.








All the contents on this site are copyrighted ©.