2017-03-04 14:22:00

Tambueni dhambi na madhara yake; ukuu, huruma na upendo wa Mungu


Kipindi cha Kwaresima ni muda muafaka wa toba na wongofu wa ndani, ili kumkimbilia Mungu asili ya sala, baraka na msamaha wa kweli katika maisha ya mwanadamu. Ni muda uliokubalika wa kufanya tafakari ya kina kuhusu kazi ya ukombozi iliyotekelezwa na Mwenyezi Mungu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Mwanaye Mpendwa Kristo Yesu. Ni kipindi cha kufunga na kujinyima kama njia ya kuratibu vilema, kwa kukazia mambo msingi katika maisha. Kwaresima ni kipindi cha kuamsha dhamiri kuhusu dhambi na madhara yake katika maisha ya mtu binafsi na jamii katika ujumla wake, tayari kujenga na kudumisha uchaji kwa Mungu.

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Kwaresima kwa Mwaka 2017 uliotolewa na Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli. Anasema, Kwaresima ni muda wa kuchunguza dhamiri, tayari kukimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu unaofunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu katika maisha ya waamini! Kristo Yesu ni dira na mwonozo wa maisha unaopaswa kufuatwa kwa unyofu; kwa njia ya toba na wongofu wa ndani; kwa kumwilisha imani katika maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa matendo ya huruma yenye mvuto na mashiko katika maisha ya watu! Ni wakati uliokubalika wa kufikiri na kutenda kadiri ya mwanga wa Injili.

Kwa njia hii, waamini wataweza kupata huruma na neema katika maisha yao kutoka kwa Mwenyezi Mungu anayeona yale yaliyofichika katika sakafu ya maisha ya mwanadamu. Kipindi cha Kwaresima ni wakati wa mapambano ya maisha ya kiroho yanayopaswa kutekelezwa kwa unyenyekevu, kwa kutambua hali halisi ya maisha ya mwamini, tayari kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Hapa mwamini anapata maondoleo ya dhambi, ushirika wa Roho Mtakatifu na kuanza kuelekea katika utimilifu wa wa Ufalme wa Mungu. Upya wa maisha ya mwamini unajionesha kwa namna ya pekee na dhamiri nyofu, ya mwamini aliyetubu, kwani dhamiri nyofu ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hapa ni mahali patakatifu ambapo Mwenyezi Mungu anaongea na waja wake.

Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli anawaalika Wakristo kukiishi kipindi cha Kwaresima, kwa toba, wongofu wa ndani, upya wa maisha; kiasi na unyenyekevu mkuu kama utambulisho wao. Ni wakati wa kuishi na kushibana na Kristo Yesu; kwa kuonesha umoja na Kanisa; upendo kwa Mungu na jirani sanjari na kukazia zaidi maisha ya kiroho. Ni kwa njia na pamoja na Kristo, mwamini anaweza kupyaisha maisha yake ya kiroho, kwa kuondokana na mambo ambayo yanasigana na kupingana na tunu msingi za maisha ya Kiinjili. Dhamiri nyofu pawe ni mahali pa kushuhudia uhuru kamili; faraja na wokovu.

Wakati wa kipindi cha Kwaresima, Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, anapenda kuwatembelea waamini wote katika maisha yao ya kiroho, ili kuwasaidia katika mapambano dhidi ya vishawishi, udhaifu wa kimwili pamoja na kumezwa mno na malimwengu; kwa kutembea na kusali kwa pamoja, ili kumwomba Kristo Yesu, Mfalme wa wafalme,  na Bwana wa mabwana aje ili aweze kujisadaka na kuwa chakula safi kwa waamini wake. Awezeshe waamini kupata amani ya ndani, kwa kujikinai dhidi ya dhambi; awawezeshe kusoma na kulitafakari Neno la Mungu, ili kujichotea neema na nguvu, tayari kuadhimisha Fumbo kuu la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anahitimisha ujumbe wake wa Kwaresima kwa mwaka 2017 kwa kuungana na waamini wote kuutukuza Msalaba wa Kristo na kwa maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Mungu pamoja na ya watakatifu wote, waweze kila mmoja wao kutekeleza wito wake na kuendelea kuuboresha kwa njia ya utukufu wa Kristo Mfufuka, chemchemi ya nguvu, neema na utukufu milele yote, Amina!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.