2017-03-04 15:10:00

Papa Francisko kukutana na kuzungumza na "vigogo" wa Umoja wa Ulaya


Baba Mtakatifu Francisko tarehe 24 Machi 2017 majira ya saa 12:00 jioni kwa Saa za Ulaya, anatarajiwa kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu kutoka katika Nchi zinazounda Umoja wa Ulaya, kama sehemu ya mkesha wa maadhimisho ya Kumbu kumbu ya miaka 60 ya Mkataba wa Roma, uliotiwa sahihi kunako tarehe 25 Machi 1957. Haya yamesemwa na Dr. Greg Joseph Burke, Msemaji mkuu wa Vatican.

Mkataba wa Roma ndio mwanzo wa Jumuiya ya Ulaya ambamo wananchi wake wana uhuru wa kutembea, kupata huduma, ajira, mtaji na rasilimali mbali mbali. Jumuiya ambayo ina sera za pamoja kuhusu sekta ya kilimo, usafirishaji na biashara. Mazingira, lishe, chakula na afya; Elimu, utamaduni, ajira na haki jamii. Uchumi, viwanda, uhuru, usalama na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 25 Novemba 2014 alipata nafasi ya kuhutubia Bunge la Umoja wa Ulaya. Aliwaonya kuhusu mwelekeo wa Umoja wa Ulaya kutumbukia katika haki binafsi na kusahau mafao, ustawi na maendeleo ya wengi. Aliwataka viongozi wa Umoja wa Ulaya kushikamana katika kukabiliana na changamoto zinazowasibu walimwengu kwa kujikita katika ubinadamu na utu wema, Mwenyezi Mungu akipewa nafasi yake katika maisha ya mwanadamu!

Akipokea ”Tuzo ya Carlo Magno”, Baba Mtakatifu aliutaka Umoja wa Ulaya kuwa ni chemchemi ya maisha na matumaini kwa watu wake; kwa kuwasaidia maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii sanjari na kuondokana na utamaduni pamoja na utandawazi usioguswa na mahitaji ya jirani zao. Pamoja na mambo mengine, Baba Mtakatifu alikazia umuhimu wa kukuza na kudumisha uaminifu, ukweli, uwazi na utu wema; kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia dhidi ya utamaduni wa kifo; kwa kuwajengea vijana matumaini ya kuwa na leo na kesho iliyo bora zaidi kwa kutengeneza fursa za ajira kuliko hali ya sasa. Baba Mtakatifu anatamani kuona Umoja wa Ulaya unaosimikwa katika haki msingi za binadamu; Injili ya uhai, upendo na mshikamano wa dhati!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.