2017-03-03 15:30:00

Tasaufi ya Injili ya furaha!


Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” anasema upendo wa Kristo unawasukuma waamini kuwashirikisha wengine furaha ya Uinjilishaji inayopendeza na kufariji, licha ya vikwazo na changamoto zinazoweza kujitokeza kwani kimsingi kila mtu anahitaji kuonja furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka ndicho kiini cha Habari Njema ya Wokovu inayoonesha upya wa milele unaofumbatwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Alhamisi, tarehe 2 Machi 2017 ameshiriki katika semina iliyoandaliwa na Jimbo kuu la Firenze kuhusu “Tasaufi ya Waraka wa Kitume wa Papa Francisko: Furaha ya Injili” kwa kukazia umuhimu wa Neno la Mungu; mafundisho hai ya Baba Mtakatifu Francisko anayewataka waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Furaha ya Injili inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha na utume wa Kanisa mahalia bila kusahau mchango mkubwa uliotolewa na Kardinali Elia Dalla Costa.

Ikumbukwe kwamba, furaha ni kiini cha Injili, huzuni ni matokeo yanayosababishwa na mashuhuda wa Injili. Kristo Yesu ni chemchemi ya furaha kama ilivyokuwa kwa Mtume Paulo, lakini leo hii kuna Wakleri wanaoogelea katika furaha iliyochangika kwa huzuni. Imani ni mhimili mkuu unaosimamisha Jumuiya kwani Kristo aliyeko ndani mwao ndiye kiini na chemchemi ya furaha. Kardinali Pietro Parolin anasema, haya ndiyo mambo makuuu yanayofafanuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kama kiini cha furaha ya Injili. Mwinjili Luka anapembua dhana ya furaha kwa kina na mapana, tangu pale Malaika wanapotangaza kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Furaha inabubujika katika mfano wa kondoo aliyepatikana tena, shilingi iliyoonekana na Mwana mpotevu anayerudi nyumbani kwa Baba mwenye huruma.

Kumbe, kimsingi, kila Mkristo, lakini zaidi Mapadre wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Furaha ya Injili, lakini kwa bahati mbaya wakati mwingine anasema Kardinali Parolin wanashindwa kutekeleza dhamana na wajibu huu msingi unaofumbatwa katika Injili ya Kristo Yesu. Mapadre wanapaswa kujibidisha ili kuhakikisha kwamba, furaha ya Injili inachanua na kueneza harufu nzuri, licha ya mapungufu yao ya kibinadamu! Mfano wa Mtume Paulo aliyetaka kutwanga kwa mawe pale Athene kutokana na malumbano na wanafalsafa juu ya Ufufuko wa wafu, hata hivyo Neno la Mungu likakua na kuota mizizi katika maisha ya wananchi wa Ugiriki, changamoto kwa watangazaji wa Injili ni kutokukata tamaa katika maisha na utume wao, daima Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo liwe mbele ya macho na akili zao!

Kardinali Parolin anakaza kusema, Yesu hakukata tamaa pale alipokuwa anakabiliwa na changamoto katika maisha na utume wake, bali alipiga moyo konde na kusonga mbele ili kuwafunulia watu Uso wa huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya maisha na utume wake, kwani hekima ya Mungu imefunuliwa kwa watoto wadogo, watu wanyenyekevu wanaoweza kukubali mpango wa Mungu katika maisha yao! Mtume Paulo katika shida na mahangaiko yake ya ndani, daima anamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa faraja anayowakirimia Wakristo ili nao waweze kuwafariji wale wote wanaoteseka katika dhiki mbali mbali, kwani Mungu ni asili ya faraja yao!

Hapa, Mapadre wanaalikwa kushiriki katika mateso na mahangaiko ya waamini kwa kutambua kwamba hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyotenda ndani yao kama anavyokaza kusema Hayati Kardinali Renato Martini. Kumbe, furaha na faraja katika mchakato wa Uinjilishaji vinaweza kububujika kutoka katika mateso na mahangaiko ya Kristo Yesu, yanayopokelewa kwa unyenyekevu kama anavyokaza kusema Kardinali Elia Dalla Costa. Hata leo hii, kuna Mapadre wanaojisadaka bila ya kujibakiza katika kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kati pamoja na watu wao, kiini cha furaha yao. Kanisa linapaswa kuwa ni chombo cha furaha, matumaini na mateso ya watu duniani kwa njia ya huduma makini.

Kardinali Parolin anasema, hata Mapadre wanapatwa huzuni lakini huzuni hii inapaswa kuwa ni kwa jinsi ya Mungu ambaye hufanya toba iletayo wokovu usiokuwa na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti. Mtume Paulo pia katika maisha na utume wake, wakati mwingine alilazimika kuandika Nyaraka zake kwa machozi kutokana na upendo mkuu aliokuwa nao juu yao, changamoto na mwaliko kwa Mapadre kuvumbua ndani mwao furaha ya kweli inayogusa undani wa maisha yao! Furaha ya kweli katika maisha ya Padre hurekebishika, hujibadilisha na hudumu kwani imejikita katika huruma na upendo wa Mungu unaojidhihirisha kwa namna ya pekee katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Kristo Yesu anapojisadaka kwa ajili ya waja wake.

Kardinali Parolin anawataka Mapadre kuwa ni chemchemi ya furaha kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia wanyonge katika ulimwengu mamboleo. Hizi ni juhudi za kuzisaidia Jumuiya za Kikristo ziweze kukua na kukomaa katika imani, matumaini na mapendo. Hii ndiyo changamoto kubwa inayotolewa na vijana wa kizazi kipya, ili kuwa na mwelekeo mpya kwa siku za usoni pasi na kung’ang’ania kwa majonzi kumbu kumbu ya miundo na desturi ambazo hazitoi tena uhai kwa ulimwengu mamboleo.

Hii ndiyo dhana ya kuzaliwa upya kutoka juu, inayoiwezesha Jumuiya ya Kikristo kutangaza na hatimaye, kuwa ni chemchemi ya furaha kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu daima yuko pamoja nao. Mapadre wanaalikwa kuwa ni uwepo endelevu wa Kristo: Kuhani na Mchungaji mkuu kati ya watu wake, katika ukweli na uwazi. Mapadre wanatumwa na kusukumizwa na upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili duniani, kwani furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wote wanaokutana na Kristo Yesu; wale wanakubali kupokea wokovu wake kwa kukombolewa kutoka katika lindi la dhambi ha huzuni; utupu wa ndani na upweke hasi, kwani pamoja na Kristo, furaha huchipuka upya daima! Ni vyema kupanda katika machozi ili kuvuna katika furaha ya Injili inayojikita katika matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.