2017-03-03 15:14:00

Mfungo wa kweli unafumbatwa katika huduma kwa maskini!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Ijumaa tarehe 3 Machi 2017 anasema, mfungo wa kweli unafumbatwa katika kujinyima ili kuwasaidia wengine katika shida na mahangaiko yao ya ndani! Katika kipindi cha Kwaresima, waamini wanahamasishwa kufunga, kusali, kutafakari Neno la Mungu na kuwasaidia jirani zao, kama njia makini iliyokubalika kwa ajili ya kumrudia tena Mungu kwa moyo wa toba na majuto ya kweli!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mwamini anayejitambua kuwa ni mdhambi, atajibidisha kujipatanisha na Mungu katika maisha yake, hasa wakati huu wa kipindi cha Kwaresima. Nabii Isaya anawaonya wale wanaofunga wakati wanatafuta anasa zao wenyewe kwa kuwaelemea wale wanaowafanyia kazi; wanafunga ili wapate kushindana, kugombana na kupigana kwa ngumi ya uovu. Hii anasema Baba Mtakatifu Francisko si saumu inayompendeza na kumfurahisha Mwenyezi Mungu, Mfungo wa kweli unajikita katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Yesu anawataka wafuasi wake kufunga bila shuruti wala unafiki kwani kwa kufanya hivi wanataka kuonekana mbele ya watu kuwa ni wenye haki, watakatifu na wachamungu, kumbe ndani mwao ni makaburi yenye mifupa iliyooza. Waamini wanaotoa sadaka na zaka zao Kanisani, waoneshe pia haki kwa wafanyakazi wao wa ndani kwa kuwapatia msahara wa haki unaokidhi mahitaji yao msingi. Watoe ajira kwa haki pasi na kuwanyanyasa wala kuwadhulumu wafanyakazi wao, mintarafu sheria, kanuni na mwongozo wa nchi husika ili hata wao waweze kuwajibika barabara katika kuzitegemeza familia zao.

Waamini wasioneshe ukarimu, ili kupigwa picha na kutundikwa kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii, kwani Baba yao aliyeko sirini anatambua kile wanachotenda kwa moyo wa ukarimu na upendo. Matendo ya huruma yasiwe ni kwa ajili ya kujinadi mbele ya watu, ili kusifiwa, kwani kufanya hivi ni unafiki unaochukiwa na Yesu. Waamini wanapotenda matendo ya huruma waoneshe moyo wa unyenyekevu, wale wanaopokea msaada kwa ajili ya maskini wasiwaibie maskini wala kutawaliwa na rushwa na kamwe wasiwe ni wabadhilifu wa maisha ya maskini. Baba Mtakatifu anasikitika kusema, lakini huu ndio ukweli wa mambo hata katika nyakati hizi.

Mfungo na saumu ya kweli anasema Baba Mtakatifu Francisko ni kufungua vifungo vya uovu, kulegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa; kuwagawia wengine chakula chako, kuwakirimia maskini waliotupwa nje, kuwavika walio uchi na kuwahurumia na kuwasaidia wale wote wanaohitaji msaada wako. Hii ni changamoto kubwa mbele ya waamini wakati huu wa Mfungo wa Kwaresima, ili kuangalia ni kwa jinsi gani wanavyofunga, wanavyojinyima, wanavyotoa sadaka, wanavyosali na kuwasaidia jirani zao. Matumizi ya waamini yawe ni changamoto pia ya kuangalia na kuguswa na shida za jirani zao maskini na wahitaji zaidi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.