2017-03-03 14:51:00

Maadui wa maisha ya kiroho! Chakula, ukuu na fahari!


Mwenyezi Mungu ametuumba na ametuweka duniani kusudi tumjue, tumpende, tumtumikie na mwisho tufike kwake mbinguni. Hayo ndiyo malengo ya kuumbwa kwetu ambayo yanafumbatwa na muunganiko wetu wa kudumu na Mungu. Mwanadamu anapokengeuka kwa sababu ya dhambi huwa anajaribu kuyapindua mawazo haya, anamwondoa Mungu katika nafasi yake halisi na mwisho hujitenga naye. Katika hali ya haraka haraka hujiona kuwa amefanikiwa na yupo huru kabisa. Kwa kuisikiliza sauti ya ibilisi hutafuta nafasi ya kujilinganisha na Mungu lakini mwisho wake ni kuitengeneza jamii ya mwanadamu yenye machungu na taabu nyingi.

Jambo la furaha kwetu ni kutokuharibiwa kabisa hadhi yetu ya kuwa wana wa Mungu. Sauti ya Mungu husalia bado ndani mwetu na daima hutualika kumrudia Mungu kusudi tuipate furaha ya kweli. Huu ndiyo wito tunaopewa katika majira ya Kwaresima, majira ambayo tumeyaanza siku chache zilizopita. Kuisikiliza sauti ya Mungu na kufanya toba na kurudi tena kwake. Kipindi hiki cha toba ni mahsusi kwa ajili ya kutuandaa na sherehe ya Pasaka iliyo kilele cha ukombozi wetu sisi wanadamu. Mungu wetu ni mwema na upendo wake ni wa milele. Yeye anatualika kumrudia akituhakikishia kuwa yupo tayari kutusikiliza na kutuokoa: “Ataniita nami nitamwitikia, nitamwokoa na kumtukuza.”

Kristo anatuonesha namna ya kupambana na inavyowezekana kupambana na maadui watatu ambao hututuoa katika ufuasi amini kwa Mwenyezi Mungu. Maadui hao kwanza ni mahitaji ya kila siku ya kibinadamu mfano wa chakula na mavazi, pili ni ulinzi na usalama wetu, na tatu ni mamlaka na mali za kidunia. Ni fursa ya kipekee mwanzoni mwa majira haya kwani tunahakikishiwa kuwa adui huyu yupo na pia tunapewa medani za kupambana naye vyema na kumshinda. Maisha yetu kiroho hufubaishwa na hatari hizi tatu ambazo hutuondoa katika kuwa waaminifu kwa Mungu na kupindisha yaliyo malengo ya uumbaji wetu.

Habari ya dhambi ya asili inatufunulia jinsi maadui hao walivyojipenyeza katika historia ya mwanadamu. Ibilisi alimkengeusha mwanadamu na kuipindua kabisa nia njema ya uumbaji. Mwanadamu ameumbwa katika namna njema sana na hata mzaburi anastaajabu na kwa kusema: “Mtu ni kitu gani hata umkumbuke, na binadamu hata umwangalie?”(Zab 8:4). Bila shaka anamwangalia mwanadamu huyu aliyeumbwa kwa sura mfano wa Mungu akimtofautisha na viumbe wengine. Mwanadamu amejaliwa utashi na uhuru wa kuchagua. Ni hadhi ya juu kabisa anayokirimiwa kiumbe huyu kuliko viumbe vyote na ndiyo maana hata uumbaji wote unawekwa chini ya uratibu wake.

Wivu na husuda ya ibilisi ilikusudia kumtoa mwanadamu katika uzuri huu. Mwanadamu anakubali kuhadaiwa na kuuza uhuru wake kwa ibilisi kusudi afanane na Mungu. Ushawishi wa mwovu shetani unamhadaa na kuisahau nafasi yake kama kiumbe na hivyo kujiweka katika nafasi ya muumbaji: “Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya”. Hili ni kusudio la kumfumba macho mwanadamu na kusahau kwamba tangu mwanzowa uumbaji aliumbwa katika hali ya kufanana na Mungu (Rej. Mw 1:26). Mwanadamu anahadaiwa na kiumbe mwenzake kuipinga amri ya muumba wake. Hapa tunaona mzizi wa dhambi kuwa ni pale mimi na wewe tunapopingana na sauti ya Mungu na kutaka kutekeleza yale tunayoyatamani na kushawishiwa na viumbe wenzetu.

Uwepo huu wa uovu katika historia ya mwanadamu unapata mwarobaini wake katika Kristo. Kwa nafasi tatu kama Injili ilivyotupambanulia anapambana na maadui watatu wa ufuasi wetu kwa Mungu na hivyo kuisimika thabiti nafsi yetu kama viumbe na kama wana wa Mungu. Kristo hamsikilizi shetani bali analisikiliza neno la Mungu. Ni dhahiri kwamba katika siku arobaini za mfungo mwili ungehitaji chakula pia tendo la kula kama tendo si ovu. Shida inajitokeza pale tunapoangalia kwa nini nile muda huu na kipindi hiki? Je, ni nini kinanisukuma kula? Kwa Kristo msukumo wa kula au anayeshawishi kula ni shetani. Hapa anatufundisha namna ya kuzishinda tamaa na hamu zetu za kibinadamu kwa kuweka mbele Neno la Mungu.

“Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila Neno litokalo kwa kinywa cha Mungu”. Adui huyu wa mahitaji muhimu ya kimwili na kibinadamu leo hii anajitokeza kwa namna ya pekee katika madai ya haki za binadamu. Haki hizi hudaiwa bila kujali namna zinavyolisukumia mbali neno la Mungu. Ni haki yangu kula, ni haki yangu kuvaa; tena zaidi sitajali hata kuwa na upendo kwa Mungu au kwa huyu ama yule kama haki yangu inakosekana. Mimi kwanza na si neno lingine.. Hapa kinachosikilizwa ni sauti ya haja zangu za kimwili na si sauti ya Mungu anayekuita kuonesha upendo kwa jirani yako.

Namna nyingine ambayo Kristo anatufundisha ni majaribu juu ya ulinzi wa Mungu. Hili uweza kujitokeza katika hali ya kuukebehi uwezo wa Mungu kwako. Mwanadamu yupo katika kutafuta miujiza na mambo ya ajabu. Mazingaombwe na kupiga bao ndivyo vinapewa kipao mbele. Ulinzi wa kichawi kupitia hirizi na mazindiko ndiyo mtindo wa kila siku. Wewe ni nani unayemjia na kumwambia mtegemee Mungu? Kilele cha kebehi hii kwa Kristo ilijionesha pale juu msalabani: “Aliokoa wengine na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu mteule wake” (Lk 23:35). Kristo anapambana na hali hii kwa kuonesha utegemezi thabiti kwa Mungu bila kumjaribu kama ni kweli au la kwamba anaweza kumlinda. Ni funzo la kuwa na tumaini kwa Mungu na kutojitafutia hatari au kutojibwetesha katika hili ama lile ati kwa sababu Mungu atakulinda. Yeye anatulinda daima katika namna zake na si kama tutakavyo sisi katika kumjaribu ili kuhalisha njia zetu ovu za ulinzi wa kidunia.

Tatu Kristo anatupatia funzo katika kishawishi cha utegemezi wa mali na madaraka ya kidunia. Kishawishi hiki hutuhadaa sana wanadamu kiasi cha kuvigeuza hivi vitu kuwa ni miungu yetu. Kristo anatuonesha jibu muafaka: “Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake”. Tunagutushwa na mahangaiko yetu ya kila siku kutafuta mali ya madaraka, mahangaiko yetu ya kuwekeza nguvu na rasilimali zetu huko na kumpiga Mungu kikumbo. Tunaishi leo hii katika jamii ambayo katika mifumo yake ya kijamii imerasimisha masuala hayo ya kidunia hata kama inapora nafasi ya mwenyezi Mungu. Si ajabu kuona siku za ibada haziheshimiwi tena kadiri ya amri na maagizo ya Mungu; ni jambo la kawaida leo hii kutafuta mali hata kwa njia za kumkufuru mwenyezi Mungu. Yote haya yanaonesha jinsi tulivyohamishia ibada zetu katika malimwengu.

Bwana wetu Yesu Kristo katika Dominika hii ya kwanza ya Kwaresima anatuwekea uhakika wa uwepo wa masuala hayo na yeye mwenyewe anakuwa mfano kwetu kwa kupambana nayo. Yeye anatufundisha njia ya ushindi hupatikana kwa kuinua daima macho yetu kumwelekea Mungu na kuisikiliza sauti yake. Medani za kiroho anazotumia ndizo pia zinazohimizwa katika majira haya ya kufanya toba. Yeye yupo karibu na Mungu kwa sababu kwanza anakuwa katika hali ya sala. Kipindi hiki cha siku arobaini amekuwa katika sala kwa kutafakari na kuisikiliza sauti ya Mungu. Pili yeye anakuwa katika namna hiyo ya sala huku amefunga. Wataalamu wa mambo ya kiroho hukiona kipindi cha mafungo kama nyenzo ya kumnidhamisha mwanadamu ili kujifunza kujikatalia hali fulani ya maisha, kujinidhamisha na pia kumweka katika hali ya uhutaji wa pekee wa mwenyezi Mungu.

Medani nyingine tufundishwayo na Kristo imejificha katika majibu yake kwa ibilisi. Hii namna ya kulitafakari Neno la Mungu katika ukweli. Ni wazi kwamba wapo watu wengi ambao hujikinai kuwa wanalisoma Neno la Mungu lakini kinachowavutia ni kile tu kinachowapatia maslahi na wala si ukweli wa mpango wa Mungu katika Neno lake. Hivyo tafakati yetu ya Neno la Mungu inapaswa kufanyika katika kweli. Kristo pia anatuonesha namna ya kuachana na kujitegemeza na mali za kidunia au kuachana na choyo na hivyo kujifunua kwa matendo ya ukarimu kwa wenzetu. Uchoyo na hamu ya kujilimbikizia hutupora upendo wetu kwa wengine walio wahitaji. Kristo anatuonya tusiabudu mali za ulimwengu huu bali Mungu peke yake. Tumwabudu Mungu katika nafsi za wenzetu hasa wale waliosukumiziwa pembeni na wenye kuhitaji misaada yetu ya kiutu.

Tuanze kipindi hiki kwa kujifunza kwa Kristo. Yeye ambaye kwa utii wake kwa Neno la Mungu ametuletea wokovu. Kwa maana “kama kwa kosa moja watu wote walihukumiwa adhabu, kadhalika kwa tendo moja la haki watu wote walihesabiwa haki yenye uzima. Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhali kwa kutii kwake mmoja watu wengi watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki.”

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.