2017-03-03 14:30:00

Kuna viumbe vinatoweka kabisa! Mbinu mkakati wa kutunza mazingira


Taasisi ya Kipapa ya Sayansi kwa kushirikiana na Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii kuanzia tarehe 27 Februari hadi tarehe 1 Machi 2017 zimeendesha Warsha ya Kimataifa kuhusu utunzaji bora wa mazingira, iliyoongozwa na kauli mbiu “Kutoweka kwa viumbe hai. Jinsi ya kutunza mazingira tunayotegemea”.  Askofu Marcelo Sanches Sorondo kwa kushirikiana na Professa Wener Arber, Professa Peter Halilton Raven pamoja na Professa Patha Sarathi Dasgupta, viongozi wakuu wa taasisi za kipapa sayansi na sayansi jamii, tarehe 2 Machi 2017 walipata nafasi ya kuzungumza na waandishi wa habari mjini Vatican kuhusu tamko la wajumbe wa warsha hii ya kimataifa.

Wajumbe hawa wanasema, kuna hatari kubwa ya kutoweka kwa viumbe hai na sababu msingi za kasi hii zinafahamika, kumbe kuna haja ya kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inalinda na kutunza mazingira bora. Kuna kasi kubwa ya kutoweka kwa viumbe hai duniani. Ikumbukwe kwamba, binadamu kwa kiasi kikubwa anategemea viumbe wengine kwa ajili ya kujipatia chakula, dawa pamoja na malighafi kwa ajili ya shughuli za uzalishaji na huduma kwa jamii. Takakata zinazozalishwa zina umuhimu wake katika maboresho ya uso wa dunia, kumbe, kutoweka kwa viumbe hai duniani ni changamoto kubwa ambayo inaweza kusababisha madhara makubwa kwa binadamu na viumbe wengine duniani.

Kilimo ni uti wa mgonjwa wa uchumi wa mataifa mengi duniani na kwamba, kwa kiasi kikubwa binadamu anategemea kilimo kwa ajili ya kujipatia chakula na malighafi kwa ajili ya shughuli za huduma na uzalishaji viwandani. Idadi ya watu inaendelea kukua na kuongezeka kila kukicha, kiasi kwamba Pato Ghafi la Taifa limeongezeka maradufu tangu mwaka 1950. Idadi ya watu duniani inaendelea kuongezeka kwa kasi kubwa, hali inayiotishia utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kutokana na matumizi makubwa ya rasilimali ya dunia. Shughuli za binadamu zimepelekea uharibifu mkubwa wa mazingira na athari zake zinaendelea kuonekana sehemu mbali mbali za dunia. Kiwango cha acid baharini kimeongezeka maradufu, hali inayotishia maisha ya viumbe hao baharini.

Wajumbe wanasema, kumekuwepo na pengo kubwa la uchumi kati ya nchi tajiri na nchi maskini sana duniani. Wastani wa pato la watu tajiri kwa mwaka inakadiriwa kuwa ni Dola za Kimarekani $ 41. 000, ikilinganishwa na pato la watu kutoka katika nchi maskini duniani, hasa zile zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara ni sawa na dola za kimarekani $ 3, 500. Nchi tajiri duniani zinawajibika kwa kiasi kikubwa katika uchafuzi wa mazingira duniani. Maskini kutoka katika nchi zinazoendelea duniani wanahusika kwa kiasi kikubwa katika uharibifu wa misitu kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, shughuli za uzalishaji na huduma kwa jamii.

Mahitaji makubwa ya malighafi kutoka katika Nchi tajiri duniani yamepekea uvunaji mkubwa wa rasilimali ya dunia kiasi hata cha kuhatarisha mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu na madhara yake yanaonekana kwenye tabianchi. Kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikizatiti katika kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote sanjari na kuwa na sera bora zaidi za ugavi wa rasilimali ya dunia, kwa ajili ya mafao ya wengi.

Wajumbe wa Warsha juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote katika tamko lao wanakaza kusema, mshikamano  wa Jumuiya ya Kimataifa katika mapambano dhidi baa la umaskini duniani ni kati ya mikakati bora zaidi ya kupambana na uharibifu wa mazingira. Kuna haja pia ya kuwa na maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya hifadhi ya viumbe hai baharini, kama sehemu ya mchakato wa kudumisha mazingira bora zaidi. Ili kuweza kufikia utekelezaji wa malengo haya, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika kanuni maadili na utu wema kama zilivyofafanuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume  ”Laudato si”  yaani ”Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”.

Waraka huu ndicho kiini cha warsha hii juu ya utunzaji bora wa mazingira. Wajumbe wanasema, kuna haja pia ya kuwa na sera makini sanjari na mbinu mkakati wa kilimo bora na cha kisiasa kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa maendeleo endelevu ya binadamu! Kuhusu matumizi ya mazao ya kilimo yenye kurutubishwa vinasaba kwa njia ya bioteklojia ni suala changamani anasema Baba Mtakatifu Francisko kwani linahitaji uwekezaji mkubwa katika kugharimia, tafiti, utekelezaji na madhara yake katika maisha ya watu. Umefika wakati wa kuwa na mipango miji inayokidhi mahitaji msingi ya binadamu sanjari na kuhakikisha kwamba, hata yale maeneo yaliyoko pembeni mwa miji yanapata huduma msingi badala ya mwelekeo wa sasa wa kuyatelekeza.

Wajumbe wa warsha hii wanahitimisha tamko lao la pamoja kuhusu utunzaji wa mazingira nyumba ya wote kwa kukumbatia changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume  ”Laudato si”  yaani ”Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”  anayeitaka Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana kwa pamoja katika mchakato wa utekelezaji wa maendeleo endelevu, ili hatimaye, kujenga jamii inayosimikwa katika haki na amani; kwa kupambana na mambo yote yanayotishia maisha, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wanadamu wajifunze kupendana na kushikamana kwa dhati; kwa kujenga madaraja yanayowakutanisha watu, ili kamwe asiwepo mtu anayeachwa pembezoni mwa jamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.