2017-03-02 14:59:00

Papa Francisko: uvuvio wa maisha ya Mungu ulete mageuzi ya upendo


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano ya Majivu, tarehe 1 Machi 2017 amezindua Kipindi cha Kwaresima kwa sala na maandamano ya toba kutoka kwenye Kanisa la Mtakatifu Anselmi, Roma, kuelekea kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Sabina, Jimbo kuu la Roma ili kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu pamoja na Ibada ya kupakwa majivu, mwanzo wa kipindi cha Kwaresima kinachofumbatwa kwa namna ya pekee katika: toba na wongofu wa ndani; sala na tafakari ya kina ya Neno la Mungu; kufunga na kujinyima kwa ajili ya jirani pamoja na kudumisha maisha ya Kisakramenti, tayari kuifia dhambi, ili hatimaye, kufufuka pamoja na Kristo Yesu!

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Sabina amekazia umuhimu wa: kufunga na kusali; kutubu na kumrudia tena Mwenyezi Mungu na kwamba, mwaliko huu unawagusa watu wote na wala hakuna anayetengwa na kubaguliwa hata kidogo, ili kwa pamoja waweze kuanza hija ya kwenda kumwabudu Mwenyezi Mungu; mwingi wa neema, amejaa huruma, si mwepesi wa hasira ni mwingi wa rehema. Huu ndio mwaliko hata kwa waamini katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo kukimbilia na kuambata uso wa huruma ya Mungu, kwani Kwaresima ni njia inayowaelekeza waamini katika ushindi wa huruma ya Mungu dhidi ya mambo yote yanayotaka kuwakandamiza na kuharibu kabisa ule utu wa wana wa Mungu.Kwaresima ni njia ya ukombozi kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti kuelekea katika uhuru kamili; kutoka katika mateso na mahangaiko, kuelekea katika chemchemi ya furaha ya kweli; kutoka katika kifo, kuelekea kwenye maisha ya uzima wa milele.

Baba Mtakatifu anasema, waamini kwa kupakwa majivu wamekumbushwa asili yao kwamba, walitwalia kutoka mavumbini na mavumbini watarudi tena! Haya ni mavumbi ambayo yamepuliziwa upendo wa Mungu na hivyo, kuwa ni chemchemi ya maisha, jambo ambalo Mwenyezi Mungu anapenda kuendelea kulifanya kwa wanadamu, ili kuwaokoa na msongo wa roho unaosababishwa na ubinafsi, uchoyo na ukimya usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Ni msongo wa roho unaokwamisha mapigo ya moyo, lakini uvuvio wa maisha ya Mwenyezi Mungu unawaokoa wanadamu dhidi ya msongo wa roho unaotaka kuzimisha imani kama “moto wa kibatari”;  msongo wa roho unaogandisha upendo utadhani barafu na kufuta matumaini kama ndoto ya mchana!

Maisha ya Kwaresima ni  kujiambatanisha na uvuvio wa maisha ambao Mwenyezi Mungu anaendelea kumkirimia mwanadamu hata katika matope ya historia ya maisha yake. Baba Mtakatifu anakaza kusema, pengine, waamini wengi hawayafahamu maisha haya kwani wamekuwa wakiyatenda kwa mazoea, kiasi kwamba, yamekuwa ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wao, hata kama madhara yake yanaonekana wazi, hata kiasi cha kuzimisha matumaini na kuanza kuvuta hewa ya uchungu na hali ya kukata tamaa; kujawa na hofu pamoja na uadui. Kwaresima ni kipindi cha kuyakataa mambo yote yanayochafua moyo wa mtu, kiasi cha kushindwa kuguswa na mahangaiko ya wengine; kubeza zawadi ya uhai, hasa kwa wale wanaoishi kwa unafiki.

Kwaresima ni kipindi cha kukataaa maneno ya uchafuzi na uchonganishi, yasiyokuwa na kichwa wala miguu; kwa watu wanaojifanya wapembuzi yakinifu, lakini wasiothubutu kuambata matatizo changamani ya binadamu, hasa kwa wale wanaoteseka zaidi. Kwaresima ni kipindi cha kukuza na kudumisha maisha ya sala na sadaka; kwa kufunga na kuwasaidia jirani. Kwaresima ni kipindi cha kuondokana na matendo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu, ili kweli wote waweze kuguswa kwa dhati kabisa na madonda ya Kristo Yesu yanayojionesha miongoni mwa ndugu zake walio wadogo zaidi; Kwaresima ni kipindi cha kuimarisha tasaufi inayojikita katika imani thabiti kwa kukataa utamaduni wa ubaguzi na nyanyaso dhidi ya watu wengine. Baba Mtakatifu anasema, Kwaresima ni kipindi cha kufanya kumbu kumbu juu ya huruma na upendo wa Mungu kwa maisha ya kila mwamini; Mwenyezi Mungu ambaye kamwe hachoki kuwahurumia waja wake; daima anawapatia fursa ya kuanza tena upya safari ya maisha yao. Kwaresima ni kipindi cha shukrani kwa mashuhuda wa Injili ya huruma na upendo wa Mungu; watu ambao wamejisadaka usiku na mchana ili kuwajalia wengine kuwa na matumaini, kiasi hata cha kuwaunga mkono ili kuanza upya tena!

Kwaresima ni muda muafaka wa kuanza kupumua tena vyema, kwa waamini kumfungulia Mwenyezi Mungu mioyo yao, kwani ndiye peke yake mwenye uwezo wa kubadili mavumbi ya maisha yao kuwa katika ubinadamu! Hakuna sababu ya kurarua mavazi mbele ya matatizo na changamoto za maisha, bali kutengeneza nafasi ya kutenda matendo mema zaidi kwa wengine; kwa kuondokana na mambo yale yanayowatenga na wengine; mambo yanayowafungia katika ubinafsi kiasi hata cha kufa ganzi! Kwaresima ni kipindi cha kumwilisha upendo ili maisha ya waamini yaweze kuwa ni utenzi wa shukrani. Mwishoni Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema nguvu ya uvuvio wa maisha ya Mungu, ulete megeuzi yatakayopelekea mavumbi ya binadamu kuwa ni upendo wenye mvuto na mashiko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.