2017-03-01 09:33:00

Papa Francisko kutembelea Jimbo Katoliki la Carpi, 2 Aprili 2017


Baba Mtakatifu Francisko Jumapili ya tano ya Kipindi cha Kwaresima, tarehe 2 Aprili 2017 anatarajiwa kufanya hija ya kitume Jimbo Katoliki la Carpi, nchini Italia. Taarifa hii imetolewa na Askofu Francesco Cavina na kuthibitishwa na Vatican. Askofu Cavina anapenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuamua kuwatembelea ili kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo. Itakuwa ni fursa ya pekee kwa Baba Mtakatifu kutembelea na kukutana na familia ya Mungu Jimboni Carpi inayoendelea kujizatiti katika imani na matumaini baada ya kukumbwa na tetemeko la ardhi lililotokea Jimboni humo kunako mwaka 2012.

Kama sehemu ya maandalizi ya ujio wa Baba Mtakatifu Francisko Jimboni Carpi, Askofu Cavina anasema, katika maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria kupashwa habari kwamba atakuwa Mama wa Mungu, hapo tarehe 25 Machi 2017, Kanisa kuu la Jimbo Katoliki Carpi litafunguliwa rasmi, tayari kumpokea Khalifa wa Mtakatifu Petro. Familia ya Mungu Jimboni Carpi imeanza kujiandaa kikamilifu ili kumpokea na kumkirimia Baba Mtakatifu Francisko anayetarajia kuwatembelea na kuwaimarisha. Wanajiandaa kumsikiliza kwa makini; ili hatimaye, kumwilisha ushauri wake katika imani na matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.