2017-03-01 11:56:00

Kwaresima ni kipindi cha matumaini, imani, toba na wongofu wa ndani


Mama Kanisa amekianza Kipindi cha Kwaresima, yaani Siku 40 za Mfungo kwa Jumatano ya Majivu. Waamini wamepakwa majivu kama kielelezo cha toba na majuto, tayari kuongoka na kumrudia tena Mwenyezi Mungu kwa njia ya upya wa maisha! Majivu ni alama ya toba inayomkumbusha mwanadamu kwamba, ametwaliwa kutoka mavumbini na mavumbini atarudi tena, kumbe ni muda wa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zake!

Baba Mtakatifu Francisko katika Katekesi yake, Jumatano tarehe 1 Machi 2017 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amesema, Kwaresima ni safari ya matumaini inayowaandaa waamini kuadhimisha Fumbo la Pasaka, yaani, mateso kifo na ufufuko wa Kristo! Kumbe, Siku 40 zinaadhimishwa na Mama Kanisa katika Mwanga wa Fumbo la Pasaka, mwaliko na changamoto kwa waamini kutoka katika giza la maisha, tayari kumwendea na kumwambata Kristo Yesu, Mwanga wa Mataifa. Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani; muda muafaka wa kufunga, kujinyima na kujisadaka kama kielelezo makini cha kuratibisha na kuvifisha vilema na dhambi, tayari kufufuka na Kristo Yesu. Ni wakati muafaka kwa Wakristo kupyaisha utambulisho wao kama Wakristo, dhamana waliyojitwalia kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo kwa kuzaliwa kutoka juu kwa njia ya upendo wa Mwenyezi Mungu. Kwa asili, Kwaresima ni kipindi cha matumaini.

Hii ni kumbu kumbu endelevu ya mkono wa Mungu uliowakomboa Waisraeli kutoka utumwani Misri, wakaongozwa na Mussa Jangwani kwa muda wa miaka arobaini kuelekea katika Nchi ya Ahadi. Wakiwa njiani, Jangwani, Waisraeli wanapewa Amri Kumi za Mungu ili kuwafunda jinsi ya kumpenda Mungu, Bwana mleta uzima pamoja na kuwapenda jirani zao. Miaka 40 ni kielelezo cha kizazi kipya, kinachohamasishwa kusonga mbele kwa matumaini, ikilinganishwa na Babu zao waliokumbwa na kishawishi cha kutaka kurejea tena Misri, walipokuwa wanayakumbuka “Masufuria ya nyama”.

Licha ya patashika nguo kuchanika katika kipindi chote cha miaka 40, lakini bado Mwenyezi Mungu aliendelea kuwa mwaminifu kwa ahadi zake, kiasi cha kuwafikisha Waisraeli kwenye bandari na nchi ya matumaini. Akawatoa “Kutoka” utumwani na kuwapatia uhuru kamili. Yote yaliyotendeka katika kipindi cha miaka 40 yaani: majaribu na mateso; kuanguka na kusimama; yanapata maana yake kwa mwanga wa mpango wa Mungu katika historia ya ukombozi; Mwenyezi Mungu anawatakia watu wake maisha tele na wala si kifo! Furaha na wala si mateso!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kwa njia ya Pasaka ya Kristo Yesu ambalo ni “Fumbo la Kutoka kwake”, amewafungulia waja wake njia ya kufikia ukamilifu wa maisha ya uzima wa milele. Ili kutekeleza dhamana hii, Yesu alijivua utukufu wake, akajinyenyekesha, akawa mtii, hata kifo cha Msalaba. Kwa kuwafungulia waja wake njia ya uzima wa milele, Yesu amemwaga damu yake azizi na kwa njia hii watu wamekombolewa kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti! Baba Mtakatifu anakaza kusema, ukombozi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ni historia ya upendo inayomtaka mwamini kukubali na kushiriki kama anavyoshuhudia Bikira Maria na baadaye watakatifu waliofuatia!

Huu ndio mwelekeo wa “Fumbo la Kutoka” ambalo linawawezesha waamini kuvuka Jangwa kwa njia ya neema nyuma yake Kristo Yesu aliyeshawishiwa, lakini akasimama imara na kushinda kishawishi kwa ajili ya waja wake, changamoto kwa waamini ni kujizatiti zaidi ili kupambana na hatimaye, kushinda vishawishi na nafasi ya dhambi. Yesu anawakirimia waja wake maji hai kutoka kwa Roho Mtakatifu. Ni jukumu na dhamana ya waamini kujichotea maji na kuyanywa katika: Sakramenti, Sala na Ibada. Yesu ni mwanga unaovunjilia mbali nguvu za giza; waamini wanakumbushwa kuendelea kutembea katika mwanga ule mdogo waliopewa wakati wa Sakramenti ya Ubatizo. Kwa mwelekeo huu, Kwaresima ni Kisakramenti cha toba na wongofu kutoka katika utumwa wa dhambi kuelekea kwenye uhuru kamili; uhuru ambao unapaswa kupyaishwa kila wakati! Hii ni hija inayowajibisha sana kama ilivyo hata katika upendo, lakini ni safari ambayo imesheheni matumaini, Kwaresima ni mahali pa kuunda matumaini.

Shida na magumu ya kuvuka jangwa; majaribu na mashaka ya maisha, yote haya ni mambo ambayo yanaimarisha matumaini kama yalivyokuwa matumaini ya Bikira Maria, wakati wa mateso na kifo cha Mwanaye Mpendwa Yesu, akaendelea kuamini na kutumainia Ufufuko wake na ushindi wa upendo wa Mungu. Kwa mwanga wa tafakari hii, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuingia katika Kipindi cha Kwaresima, wakitambua kwamba, wao pia ni sehemu ya watu wa Mungu, kumbe wanapaswa kuianza safari ya matumaini!

Kimsingi, kipindi cha Kwaresima ni hija ya: toba na wongofu wa ndani, imani, furaha, matumaini; pamoja na nguvu ya huruma ya upendo wa Mungu. Waamini walioifia dhambi, wakatakaswa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu wanaweza kufufuka tena na Kristo! Ni wakati muafaka wa kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwaresima ni kipindi cha kujinyima, ili kujitakasa na malimwengu, ili kuwa watoto huru wa Mungu kwa njia ya Sala na Sakramenti za Kanisa. hiki ni kipindi cha kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani, kwa kushiriki kikamilifu katika kampeni za Kwaresima kwa ajili ya huduma kwa maskini na wahitaji zaidi, ushuhuda wa Injili ya upendo. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka waamini kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza ili kutekeleza safari ya toba na wongofu wa ndani; kwa kuvumbua tena zawadi ya Neno la Mungu, ili waweze kutakaswa, tayari kumhudumia Kristo Yesu anayejionesha kati ya maskini na wanyonge zaidi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.