2017-02-28 16:26:00

Watoto na wanawake wahamiaji na wakimbizi hupata mateso makubwa


Kwa mujibu wa ripoti mpya ya  Shirika la kuhudumua watoto duniani,UNICEF iliyotolewa tarehe 28 Februari 2017 ya kwamba watoto na wanawake wakimbizi wahamiaji  wanao kimbia mateso mara kwa mara wanateseka kijinsia, unyanyasaji , kutumikishwa na kuwekwa vizuizi wakati wa safari  kupitia baharini kutoka Afrika ya Kaskazini na Italia.
Ikipatiwa jina safari ya hatari ya watoto kupitia njia ya wahamiaji ya Mediteranea, ripoti hiyo inaeleza kwa kina hatari wanazokumbana nazo watoto wakimbizi wanaposafiri kupitia jangwa la Sahara, Libya na hatimaye kuvuka bahari kuingia Italia.


Robo tatu ya watoto ya wakimbizi na wahamiaji waliohojiwa kwa ajili ya utafiti wanasema wamekuwa wanakabiliwa na vurugu, unyanyasaji au mashambulizi katika mikono ya watu wazima wakati wa safari hiyo.Wakati karibu nusu ya wanawake na watoto waliohojiwa wanasema wamedhalilishwa kijinsia mara nyingi  wakati wa kuhama kutoka sehemu moja hadi nyingine, mara kadhaa na katika maeneo mbalimbali wanapofikia katika safari. Wengi wa watoto wameripoti kuteswa kwa matusi au kisaikolojia, wakati nusu yao wamepata mateso ya  vipigo au aina nyingine ya unyanyasaji wa kimwili. Kwa upande wa wasichana, wameonesha kuwa na matukio mengi zaidi ya kuliko wavulana.


Mwaka jana, watu wasiopungua 4,579 wamekufa wakijaribu kuvuka Mediterranean kutoka Libya, na mmoja katika 40 ya wale ambao walijaribu na imekadiriwa kuwa watu 700 ambao walipoteza maisha yao walikuwa ni watoto.Njia ya Kati ya Mediterranean, kutoka Afrika Kaskazini kuelekea  Ulaya, ndiyo watu wengi wanakufa kwa wingi  na miongoni mwao zaidi ni watoto na wanawake, anasema Afshan Khan Mkurugenzi wa Kanda na Mratibu Maalumu wa UNICEF katika mgogoro wa Wakimbizi na Wahamiaji Ulaya.


Anaongeza "Tunaushawishi Muungano wa Ulaya utenge rasilimali kuimarisha mipango ya ulinzi wa mtoto nchini Libya ili kuzuia watoto walio hatarini zaidi na pia kuinua uwezo kwenye vituo vya mapokezi na malezi." Anaongeza akisema;njia hiyo inathibitiwa na wafanya biashara haramu na watu wengine ambao wanawateka kwa urahisi kutokana na  kuwaona watoto na wanawake wamekata tamaa ,na kutafuta namna ya kukimbia kwa kutafuta maisha bora
Mapendekezo mengine matano ni ulinzi wa watoto wakimbizi na wahamiaji wanaosafiri peke yao, kuondokana na ushikiliaji watoto wanaosaka hifadhi, kuweka familia pamoja kama njia ya kulinda watoto, kuchukua hatua dhidi ya vichochezi vya ukimbizi na uhamiaji.Anasisitiza Afshan Khani kwamba mipango ya usalama na kisheria inahitajika kwa haraka ili kuwalinda watoto wahamiaji , wawezekuwe kupata mahali pa usalama na kuwa mbali na wahalifu hao.

Sr Angela Rwezaula

Idhaa ya Kiswahili ya Radio vatican

 








All the contents on this site are copyrighted ©.