2017-02-28 07:49:00

Tangazeni na kushuhudia Injili ya huruma na upendo wa Mungu kwa watu!


Kardinali Carlos Osoro Sierra wa Jimbo kuu la Madrid, Hispania ni kati ya Makardinali walioteuliwa na kusimikwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa kukunja jamvi la maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Jumamosi, jioni tarehe 25 Februari 2017 alikabidhiwa rasmi Kanisa la Bikira Maria Tastevere, kuwa ni kituo chake cha huduma kama Kardinali. Hili ni Kanisa ambalo linatumiwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kama madhabahu ya kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Kardinali Carlos Osoro Sierra, katika mahubiri yake anasema, hata yeye anapenda kujitoa bila ya kujibakiza katika maisha na utume wake kama Padre na Askofu kutekeleza dhamana ya kutangaza na kushuhudia Injili hasa miongoni mwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kanisa hili ni mahali pa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya huduma makini kwa maskini sanjari na kuimarisha umoja, upendo na mshikamano wa kidugu.

Ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye asili ya wokovu wa watu wake na hapo kwake wanaweza kupata kitulizo cha kweli cha maisha, mwamba na nguzo thabiti ya faraja na mahusiano kati ya watu. Mwenyezi Mungu kamwe hawezi kuwasahau watu wake, hata pale mwanadamu anapokengeuka na kutopea katika malimwengu kutokana na ubinafsi, uchu wa fedha, mali na madaraka kiasi hata cha kudhalilisha utu na heshima ya binadamu, lakini bado anajitaabisha kumtafuta ili kumwokoa mwanadamu kwani ameumbwa kwa sura na mfano wake.

Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanakumbushwa kwamba, wao ni watumishi na wahudumu wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, zawadi kubwa ambayo wanashirikishwa katika maisha na utume wa Kristo Yesu. Waamini wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani, upendo, msamaha, upatanisho na mshikamano wa dhati. Waamini wawe mstari wa mbele kupambana na ubinafsi kutoka kutoka katika undani wa sakafu ya maisha yao; wawe ni mashuhuda wa Injili ya amani dhidi ya vita, utamaduni wa kifo sanjari na ukosefu wa haki msingi za binadamu.

Kardinali Carlos Osoro Sierra anakaza kusema, kama waamini wanatumwa sehemu mbali mbali za dunia kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya wokovu, inayojengwa na kusimikwa katika imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Hapa, kipaumbele cha kwanza ni kutafuta Ufalme wa Mungu, kwani mengine yote watapewa kwa ziada! Waamini wawe na ujasiri wa kutafuta na kuambata mambo msingi katika maisha badala ya kuwa na wasi wasi na hofu ya mambo ya kidunia, kwani hawawezi kumtumikia Mungu na mali. Yesu Kristo aliyejitoa Sadaka Msalabani anaendeleza sadaka hii katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, awasaidie waamini kumwona Mwenyezi Mungu aliyejifunua kwa njia ya Kristo Yesu katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake kwenye Fumbo la Pasaka, yaani Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo, chemchemi ya imani na matumaini ya Kanisa. Yes uni kielelezo makini cha huduma kwa binadamu: kiroho na kimwili; awasaidie waamini wote wawe kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya huduma na upendo kwa wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.