2017-02-28 15:41:00

Jumatano ya Majivu: Misingi ya imani: Sadaka, Sala na Mfungo!


Mwaliko “Mnirudie mimi, kwa machozi, kulia na maombolezo.” Maneno haya ya Nabii Yoeli yanaweza kuwa kauli mbiu ya Kipindi cha Kwaresima ya mwaka huu. Kwa kawaida tumezoea kusikia kwaresima kuwa ni kipindi cha vilio, mifungo na maombolezo. Aidha kuna kujipaka majivu yanayotukumbusha kifo, na tunaambiwa: “Binadamu kumbuka kuwa wewe ni mavumbi na mavumbini utarudi.” Kisha tunaalikwa kutoa sadaka, kujikana na kujitesa. Mambo haya yote ni ya huzuni, ni ya uchungu na ya masikitiko. Kumbe Mungu ametuumba tuwe na furaha. Kwa hiyo lengo la kwaresima ni kutuongoza kwenye furaha. Lakini budi tutofautishe kati ya furaha na raha. Katika kipindi hiki tunaalikwa kuhakiki na kutathmini mambo ambayo hayakutupeleka kwenye furaha.

Kuna vipengele kadhaa katika Injili ya leo vinavyoweza kutuongoza kwenye kupata furaha ya kweli.  Kipengele cha kwanza cha kupata furaha ya kweli, ni kufanana na Mungu. Mara nyingi tunapofanya kitu kizuri au kitu cha kishujaa, tunapenda kutazamwa na tunajisikia vizuri kama tunatambuliwa, tunashabikiwa na kupongezwa. Wakati mwingine tunapenda kujificha ili tustaajabiwe, mathalani natafuta kukosekana katika nafasi fulani ili nitambuliwe kuwa nimekosekana. Huko kutaka kuonekana kwa nje inaathiri uchaguzi wa mambo yetu na kufutafnya tuwe watumwa wa ulimwengu. Tunapenda zaidi kutazamwa na watu kuliko na Mungu. Ndiyo maana Yesu anasema: “Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao.”

Kisha Yesu anasema: “naye Mungu aonaye sirini atakujazi.” Kama hatuishi mbele ya macho ya Bwana, bali tunapenda kufuata macho ya binadamu, hapo tunapoteza thawabu tuliyoandaliwa na Baba yetu wa mbinguni. Thawabu anayomaanisha Yesu hapa ni ule mtazamo wa Mungu unaotufanya daima tufanane naye zaidi. Kwani tunapomwelekea zaidi Mungu hapo tunakuwa binadamu zaidi na tunang’ara kwa upendo kama baba wa mbinguni na mapato yake ni kuwa na furaha ya kufanana na Mungu. Kwa hiyo “kujazi” ni kufanana na Mungu. Baada ya kutuletea alama hii ya kwanza, Yesu anatupendekezea namna mpya ya kuishi misingi ya imani ya dini yetu. Wayahudi walikuwa misingi mitatu ya imani yao kwa Mungu, nayo ni Sadaka, Sala na Kufunga. Misingi hii ipo katika kila dini hapa duniani. Yesu anataka kutuonesha namna mpya ya kuiishi misingi hiyo na tahadhari zinazoambatana nazo.

Msingi wa kwanza ni Sadaka. Yesu anasema: “Basi wewe utoapo sadaka.” Kutoa sadaka tunaelewa maana yake ni kumsaidia fedha maskini. Kumbe Wayahudi hawana neno la kutoa sadaka, badala yake wanalo neno Tzedakah, ambalo kwa kiswahili ni sadaka. Neno hili Tzedakah maana yake ni haki. Wanafunzi wa Yesu wanatakiwa kuunda ulimwengu mpya usiohitaji sadaka au ufadhili, bali ulimwengu wa haki tena haki ya Mungu, kwa sababu haki ya binadamu inasema “kila mtu na chake.” Mungu haki yake ni kumiliki mali, na binadamu ni mtunzaji tu wa mali hiyo ya Mungu. Lengo la Mungu kwa mali yake ni kwa matumizi ya wahitaji. Mt. Ambrosi alisema: “kumsadia maskini ni sawa na kumrudishia mali anayostahili awe nayo kwani mali hiyo ni ya Mungu.”

Kwa vyovyote hapa ulimwenguni binadamu anatakiwa atoe sadaka au ufadhili kwa wahitaji. Kumbe, Wayahudi waliishi thamani hiyo ya kutoa sadaka kwa namna potovu. Mathalani, katika kila kijiji kulikuwa na utaratibu wa kukusanya hela kwa ajili ya kusaidia yatima, wajane na wasafiri. Yule aliyetoa sadaka zaidi alipewa fursa ya kujieleza mbele ya kadamnasi na kupata hadhi ya kuketi viti vya mbele ili kuonekana na kumwagiwa sifa. Hali hii imejipenyeza hadi makanisani tunapomtangaza mtu anayetoa mchango mkubwa wa sadaka. Kadhalika katika jamii,  tunapotengeneza bango la cheki ya benki na kupiga picha kumwonesha mtoaji na mpokeaji. Ufarisayo huo hufanyika pia pale mmoja anapowachangia watoto yatima au wagonjwa nguo, chakula, maziwa ya kopo, au viti vya kukalia, hapo kutapigwa parapanda katika vyombo vya habari kama vile: radio, luninga na magazetini. Yesu hapendezwi kabisa na namna hii ya imani. Badala yake anapendekeza kutoa sadaka yetu kwa siri. Anasema: “usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu.”

Anaongeza kusema: “Basi wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.” Neno hili atakujazi, kwa kigiriki ni epotidomi, halina maana kwamba Mungu huyo atakupa mshahara, la hasha, bali epotidomi ni kufanana na Mungu anayependa bila masherti. Hii ndiyo thawabu inayomaanishwa hapa yaani kufanana na Baba wa mbinguni. Kwa kufanya hivyo, unajirudishia tena sura ile ya umwana uliyoipoteza kwa kujilimbikizia mali ya maskini kwa ubinafsi. Aidha anasema: “wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanalo mkono wako wa kuume.” Hapa yabidi kuwa makini sana tunapotoa sadaka kusudi tuweze kufanana na Baba wa mbinguni. Mungu anapotusaidia hatunyenyekeshi na kutufanya tujisikie wanyonge, bali anatuinua na kutupa hadhi yetu ya kibinadamu na kutufurahisha. Tujihadhali tunapomsaidia mwenye dhiki asijisikie mnyonge bali awe na furaha.

Nguzo ya pili ya imani ya kiyahudi ni Sala. Siku za leo thamani hii ya sala imechakachuliwa. Watu wanajiuliza kwa nini wasali na wasali namna gani. Mathalani wanahoji, endapo Mungu anajua kila kitu, kwa nini nimworodheshee mahitaji yangu. Hata Yesu anasema: “Maana Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba.” Kwa hiyo sala ni kama kumlazimisha Mungu afanye mambo tunayotaka sisi kinyume cha hadhi yake ya upendo kwa wanawe. Kumbe kusali ni kuongea na Mungu mpendwa wetu. Mtu hawezi kulazimishwa kuzungumza na mpendwa wake, bali inakuja yenyewe tu. Kuhusu namna ya kusali, Yesu anasema: “Msipaukepayuke kama watu wa mataifa yaani wapagani.” Wakati wa Yesu kulikuwa na namna mbili za sala: Ile ya hadharani, iliyofanyika mara mbili kwa siku. Saa tatu asubuhi na saa tisa alasiri pale inapofanyika sadaka hekaluni. Hapo mtu mwingine yeyote popote alipo alisimama na kusali. Hatari yake ilikuwa ni kusimama popote pale hata sokoni na kuanza kusali ili uonekane. Siku za leo hatari hii kwa mkristu haipo kabisa, kwani mara nyingi mkristu anasali katika kificho au pengine hasali kabisa akiona aibu ya kuchekwa.

Aidha Yesu anasema: “Basi wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako.” Chumba hicho ni tamieion yaani katika upweke, pasipo na sauti wala mwanga. Hapo kuna mwanga na sauti moja tu nayo ni Mungu. Sala inakufanya umwone mwingine kama anavyoonekana na Mungu. Yesu anasema: “na Baba yako aonaye sirini atakujazi.” Sala ya binafsi inanifanya niyaone matatizo yangu, na fikra zinazonihuzunisha, na namna yangu ya kutaka haki itendeke. Muujiza unaofanyika hapo ni kuniwezesha mimi kuyaona mambo kama anavyoyaona Mungu na kuyatolea maamuzi anayonidokezea Mungu katika sala. Hali hii inafika katika ukimya katika kuangalia mwanga wake na kusikia neno lake. Hapo Mungu atatujazi picha yake na namna yake ya kutenda. Kwa hiyo kama tukisali pindi tuna hasira dhidi ya ndugu hapo Mungu anatupatia picha yake na tunamwona kama ndugu na kumpenda kama Mungu anavyompenda.

Nguzo ya tatu ya imani na dini ya kiyahudi ni Mfungo. Yesu anasema: “Tena mfungapo” Wayahudi wenye msimamo mkali waliweza kufunga mara mbili kwa juma, hadi Warumi walikuwa na msemo: “Unafunga kama myahudi.” Ingawaje Yesu alikuwa Myahudi, lakini anazungumza mara mbili tu juu ya mfungo. Mosi, pale anapowatetea wanafunzi wake wasiofunga, na pili ni Injili ya leo anaposema: “mfungapo.” Paulo katika barua zake, hatamki kabisa mfungo. Kwa hiyo yawezekana mfungo umeingia katika kanisa kwa njia ya wamonaki wa karne za kwanza. Neno hili mfungo limeongezwa katika injili Yesu alipoulizwa na wafuasi wake: “Kulikoni sisi tulishindwa kumtoa pepo huyu?” Yesu aliwajibu: “Shetani huyu hawezi kutoka isipokuwa kwa sala,” na wao wakaongeza “na mfungo.”

Mfungo wa Mkristo hauna maana ya maombolezo, ya huzuni bali ni furaha. Yesu anasema: “Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso.” Kwa hiyo mfungo kwa mkristu ni sikukuu kwani Yesu anataka tuwe na furaha. Mfungo unaompendeza Mungu ni ule unaotokana na upendo. Ule ambao mmoja anaacha kula chakula kwa ajili ya kumpa furaha mwingine. Hapo mfungo unakujazi, kwani unasafisha moyo kutokana na mambo ya ulimwengu huu na hutengeneza upendo. Mfungo wa kweli ni ule unaoturudishia hadhi ya uwana kwa sababu unatufungulia moyo kwa upendo wa ndugu. Ama kweli: “Mnirudie mimi, kwa machozi, kulia na maombolezo” na tufanane na Mungu.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.