2017-02-25 09:48:00

Papa Francisko: haki ya maji safi na salama ni kwa wote!


Semina ya kimataifa kuhusu haki ya maji iliyoandaliwa na Taasisi ya Kipapa ya Sayansi  kwa kuwashirikisha wataalam 96 kutoka katika sekta ya maji na afya, sehemu mbali mbali za dunia, ili kuchambua maji kama sehemu ya haki msingi za binadamu imemalizika, Ijumaa tarehe 24 Februari 2017 kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Amewashukuru wajumbe wa semina hii kwa kushirikisha uzoefu na mang’amuzi yao ili kuweza kutoa jibu makini kwa watu wanaoishi katika ulimwengu mamboleo.

Maji ni sehemu muhimu sana kwa maisha, ustawi na maendeleo ya binadamu, changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa ni kusimama kidete ili kujenga utamaduni wa utunzaji bora wa maji, kwani maji ni uhai ikiwa kama ubora na usalama wake utazingatiwa na wote. Maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu na kwamba, kila mtu ana haki ya kupata maji safi, salama na yenye ubora! Binadamu anapaswa kujifunza kutumia rasilimali maji kwa unyenyekevu bila kuyachafua. Haki ya maji safi na salama ni kati ya changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba kuna baadhi ya nchi ambazo bado hazijatambua kwamba, maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu na baadhi ya nchi zinapinga maji kuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Rasilimali maji inapaswa kushughulikiwa kikamilifu kwani hii ni sehemu muhimu sana katika mchakato wa maboresho ya maisha ya binadamu sanjari na mapambano dhidi ya umaskini duniani.

Rasilimali maji inapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika sera za kitaifa na kimataifa kutokana na umuhimu wake kwa maisha ya binadamu. Sera hizi ziwe na mwelekeo wa kisiasa na kisheria, kama ilivyokubaliwa na Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2010 mintarafu haki ya maji safi na salama pamoja na afya bora. Wadau mbali mbali wanapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu, kwani hii ni sehemu ya mustakabali wa binadamu kwa siku za usoni. Vijana wa kizazi kipya wanapaswa kufundwa barabara kuhusu umuhimu wa rasilimali maji katika maisha ya binadamu. Baba Mtakatifu anatambua kwamba, ujenzi wa dhamiri nyofu ni dhamana pevu inayohitaji utambuzi, majitoleo na sadaka!

Vita kuu ya Tatu ya Dunia inayopiganwa sehemu mbali mbali, inaweza kuwa ni njia itakayoitumbukiza pia Jumuiya ya Kimataifa katika vita ya dunia kwa ajili ya maji. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, kuna idadi kubwa ya watoto wanaofariki dunia kutokana na magonjwa yenye uhusiano na maji; kuna mamilioni ya watu wanaotumia maji yasiyo safi wala salama! Kumbe, Jumuiya ya Kimataifa haijachelewa kuchukua hatua madhubuti ili kutambua na kulinda maji kwa ajili ya mafao ya wengi. Utunzaji bora wa maji ni sehemu muhimu sana ya haki msingi za binadamu; ikiwa kama watu wataweza kuheshimu haki hii, itakuwa ni rahisi kwa haki nyingine zote kuweza kulindwa na kudumishwa, hapa mwaliko ni kujenga utamaduni wa kutunza maji unafumbatwa katika utamaduni wa watu kukutana, ili kuunganisha nguvu kutoka kwa wadau mbali mbali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi mintarafu rasilimali maji.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, umoja ni nguvu, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itaunganisha nguvu kwa ajili ya mafao ya wengi; itafanikiwa kusikiliza na kujibu kilio cha haki msingi ya maji; ardhi inayopaswa kutunzwa na kuendelezwa zaidi kwa ajili ya mafao ya wengi. Utamaduni wa watu kukutana  utaiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kuwa na maji safi na salama pamoja na uhakika wa ubora wa maji. Mwenyezi Mungu kwa wema na ukarimu wake anapenda watu wote waweze kufaidika na rasilimali maji, lakini hii ni kazi, dhamana na wajibu wa kila mtu anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Kumbe, wajumbe wa mkutano wa kimataifa kuhusu haki msingi ya maji watambue kwamba, wanao mchango mkubwa katika mchakato wa kuhakikisha kwamba, kweli maji yanakuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu, ili kuwasaidia watu kupata maji safi na salama! Hapa kuna haja ya kufanya kazi kwa pamoja na kushikamana katika mapambano ya maji kama sehemu ya haki msingi za binadamu! Lengo anasema Baba Mtakatifu ni kujenga ulimwengu unaosimikwa katika haki, amani, utulivu na mshikamano na wote, bila mtu awaye yote kutengwa! Hii ni dunia ambamo wote wanafaidika na mambo msingi katika maisha ya binadamu, ili kuishi na kukua katika utu. Takwimu za Umoja wa Mataifa kuhusu watu wasiokuwa na huduma ya maji safi na salama; idadi kubwa ya watoto wanaoendelea kupoteza maisha kwa kukosa maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya binadamu ni mambo ambayo wadau mbali mbali wanapaswa kuyazingatia katika kuragibisha mchakato wa maji kuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.