2017-02-25 12:50:00

Msiwe na hofu, wekezeni kwenye Injili ya Kristo!


Wapendwa taifa la Mungu, dhamira inayoonekana katika masomo yetu ya leo ni mwaliko wa kutambua huruma ya Mungu na kutokuwa na hofu na wasiwasi.  Tunapojiuliza uwezekano wa kuishi katika uhalisia wa neno hili, ninawaalika tutafakarishwe na sehemu ya maandiko matakatifu kutoka Zab. 23 – ambapo tunasoma, Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu …. na kutoka injili ya Mat. 6:33 – Basi, kwanza utafuteni ufalme wa Mungu na uadilifu wake, na hayo yote mtaongezewa kwa ziada. Katika ufahamu huu na tukitambua kuwa Neno la Mungu ni la kweli basi tunaamini kuwa mwaliko huu wa Mungu leo na Neno lake hauwezi kutudanganya.

Hakika, katika hali ya wasiwasi wa mwanadamu, mtu aweza kuhofia uwezekano wa neno hili. Mwanadamu ana hali ya wasiwasi, mashaka na kutokujiamini. Mtume Paulo anatufundisha akisema ili tuweze kuliishi neno la Mungu katika uhalisia wake hatuna budi kutambua kuwa ni roho ya Kristo inayotuita tuwe huru na inayotuwezesha kutoa jibu katika huo ufuasi – Gal. 5:1,13-18. Wito wa ufuasi hautegemei kusikia sauti ya roho zetu bali twaitwa kusikiliza sauti ya Roho yake Kristo.

Ndugu zangu, tukisoma sehemu ya Maandiko Matakatifu kama ilivyo katika somo la kwanza toka Nabii Isa. 49;14-15 tunaona tamko la kimungu linaloelezea wazi upendo wa Mungu kwa watu wake. Mungu ni Baba, tena Baba ambaye anajali, anayetuona na anayetuondoa katika mahangaiko yetu, kimsingi ni Baba mwenyehe huruma na mapendo.  Katika somo la pili Mtume Paulo anaongea wazi juu ya utume wake na kusema wazi kuwa watumishi wake Kristo ni walinzi wa Mafumbo Matakatifu ya Mungu.

Kwa maana hii, swala la utumishi na uaminifu linawekwa wazi hapa. Ndo maana katika injili Yesu anasema wazi – huwezi kutumikia mabwana wawili na pia tunakumbushwa kutokuwa na hofu na wasiwasi. Mfuasi wa Kristo hawezi kugawanyika.  Na mahali pengine katika injili, Yesu anaweka wazi sifa za kuwa mtume/mfuasi na utume wenyewe – upole na unyenyekevu na anaweka wazi wajibu rasmi akisisitiza kuwaponya wagonjwa – lengo ni kuutangaza ufalme wa Mungu. Kwa namna ya pekee, Yesu anawaagiza Mitume na wafuasi wawekeze katika Injili na kujiepusha na mahangaiko ya kawaida na yasiyo ya lazima katika maisha. Anawakumbusha wategemee nguvu za Kimungu katika utendaji. Nguvu hii ya Mungu ndiyo inayowezesha yote hayo.   

Mwaliko wa Yesu kama  tubuni na kuiamini Injili, mpende adui yako,  kama mkono wako unakukwaza ukate, ni afadhali kuingia ufalme wa Mungu u kigutu kuliko kuukosa, msihangaike mtakula nini au mtavaa nini ni mwaliko wa kufanya mabadiliko na kuwa na mtazamo mpya wa kimaisha. Maisha mapya ya Mtume Paulo baada ya wongofu yaendelee kutupa changamoto sisi sote tunaomtumainia Mungu.

Mtume Paulo anajivunia wazi ushindi wa msalaba wa Kristo. Anasema wazi – mtu akitaka kujisifu, ajisifu katika Bwana. – 1 Kor. 1:31. Mtume Paulo alitimiza wajibu wa kwanza kabisa wa mbatizwa. Kuutangaza ufalme wa Mungu. Na alifanya hivyo. Akajitoa na akatoa yote aliyokuwa nayo kuhubiri neno la Mungu. Angalia somo la pili, Jumapili hii.

Tukisoma katika kitabu cha Mdo. 3:1-10 tunaweza kupata msaada kuelewa vizuri Neno la Mungu la leo. Tunasikia habari ya muujiza wa uponyaji wa kiwete tangu kuzaliwa. Aliwaona Petro na Yohani wakiingia hekaluni. Alitegemea kupata fedha kutoka kwao. Petro anamwambia wazi sina dhahabu wala almasi, bali nitakupa nilicho nacho. Kwa jina la Yesu wa Nazarethi tembea. Wakamshika mkono na mara miguu yake na viungo vikafunguka, akaruka, akasima na kutembea na akaingia hekaluni na Petro na Yohane kuabudu. Hatuna budi kujiuliza leo mahangaiko yetu ya maisha yamejikita katika nini? Sisi tunaomba nini kwa Mungu?

Hali ya wasiwasi ni sehemu ya maisha ya mwanadamu. Katika wasiwasi huo na mashaka hayo kama ya yule kiwete, basi tunaalikwa kutafakari sana leo kuhusu maisha yetu na vipau mbele vyetu vya kiroho na kimwili. Lipo swali moja ambalo laweza kujibika kiurahisi au likazua mjadala endelevu. Ni kipi kinatangulia – punda au mkokoteni? Pengine kama yule kiwete – Yesu angekuwa hapa leo tungeomba nini?

Ndugu zangu, hatuna budi kutambua kuwa usihofu hii ya kibiblia inatualika tuvuke ile hali inayotupelekea kuzama katika tamaa ya vitu au kung’ang’ania vitu hata kufikia kupoteza utu wetu. Tuchukue mfano mdogo kama huu ambapo inapotokea pengine kwa bahati mbaya umevunja simu ya mtu – hakika kitakachofuata ni matusi au kila aina ya neno baya dhidi ya mkosaji. Kitu kinakuwa na thamani zaidi ya mtu. Tunasongwa na wasiwasi wa vitu na kusahau utu wa mtu.Kama tujuavyo ni kweli kwamba ndege wa angani hawalimi, lakini pia hata hivyo Mungu hawapelekei chakula katika viota vyao. Lakini hii isihalalishe kutokufuata utaratibu katika namna ya kutafuta na kutumia vile tuvipatavyo.

Tutafakarishwe tena na mfano huu. Siku moja jioni baada ya baba kurudi kutoka kazini, mtoto alimwomba baba yake amwambiye kiasi anachopata katika saa moja ya kazi anayofanya. Baba akajibu kwa hamaki dola 20. Mtoto akamwomba dola 10. Kama kawaida baba akajibu, ya nini. Baba huyu alihangaika sana kufanya kazi nyingi ili familia yake ipate kuishi vizuri. Na kweli ilikuwa familia iliyojitosheleza kiuchumi. Lakini basi katika hali hii hakuwa na muda wa kuwa karibu na familia yake ambayo aliipenda sana. Muda wa kulala ulipofika kila mmoja akaenda chumbani kwake. Hata hivyo lile ombi likawa linamsumbua sana yule baba.

Usiku wa manane akaamka na kwenda chumbani kwa mwanaye na akashangaa sana kumkuta bado akiwa macho. Bila kusita baba akampatia dola zile 10 alizoomba. Kwa furaha kubwa yule mtoto akapokea na mara akainua mto wake na kutoa dola nyingine 10. Akaweka pamoja na kumpatia baba yake zote. Yule mtoto huku akiwa na furaha kubwa akamwomba baba azipokee zile dola 20 kama malipo ya saa yake moja ya kazi. Huku baba akishangaa, mtoto akamwambia naomba tu nikulipe muda wako wa saa moja ya kazi ili niweze kukaa nawe baba yangu mpendwa. Najua unanipenda lakini nakosa muda wa kukaa nawe. 

Tumsifu Yesu Kristo,

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.