2017-02-24 14:04:00

Mtumainieni Mungu katika maisha yenu!


Desturi ya mwanadamu mahali popote pale duniani ni kujihangaisha na kufanya hiki ama kile kwa ajili ya kupata hakika ya kesho yake; kwamba utakula nini au utavaa nini, kwamba utaboreshaje hali yako ya maisha au mazingiza yanayokuzunguka kuwa na bora zaidi. Juhudi zote hizi ni uthibitisho wa uerevu wa mwanadamu anayetumia vipawa na akili zake kwa ajili ya kujipatia hakika ya usalama wake na mahitaji yake ya kila siku. Juhudi hizi za mwanadamu kwa upande mwingine humgeuza mtumwa na kuelekeza mawazo na fikra zake zote katika kuyatimiza haya yaliyo mahitaji au hamu ya moyo wake huku akiachwa katika kilindi cha giza cha kushindwa kuona lililo la muhimu na la thamani zaidi katika maisha yake.

Ni wazi mmoja anaweza kujikinai kuwa anahangaika kwa ajili ya ustawi wake, mathalani afya yake na uhai wake bila kujisumbua kutafakari ni nini kilicho cha juu zaidi ambacho kinapopewa kipaumbele basi tumaini la kweli hujengeka mioyoni mwetu. Na hili uonekana pale ambapo mmoja anapokwama katika mambo yake kugubikwa na msongo wa mawazo na kukata tamaa kabisa. Neno la Mungu katika Dominika hii ya leo linatupatia mwanga na kung’amua kile ambacho tunapaswa kukichuchumilia na kukipatia kipao mbele katika mahangahiko yetu ya kila siku. Si chakula, mavazi au ridhiki ya kila siku; hivyo vyote hutufikia kwa njia mbalimbali zilizofichika ndani ya mwenyezi Mungu. Tunaalikwa kufumbua macho yetu na kuiona thamani yetu mbele ya Mwenyezi Mungu na kujitegemeza kwake. Ni wito kufikia hali ya kuona na kuing’amua thamani ya utu wetu na hivyo kuweka tumaini letu kwa Mungu kwa uhakika kwamba hatotuangusha. Neno la Kristo linatuonesha fursa mbalimbali za kidunia kwa viumbe vyote ambazo zinaonesha jinsi Mwenyezi Mungu anavyothamini na kuvilinda viumbe vyake. Yeye anavihakikishia viumbe vyote ustawi katika chakula na mahitaji mengine muhimu, ishara ya upendo wake usio na kipimo.

Tunaweza kuliweka tumaini letu kwa Mungu pale tu tutakapompatia yeye nafasi ya kwanza kwa kuwa Kristo anaonya kwamba hatuwezi “kumtumikia Mungu na mali”. Tumaini letu kwa Mungu ni la hakika na kamwe halituangushi. Tunapata uhakika huo kupitia Neno lake kwa kinywa cha Nabii Isaya asemaye kwamba: “Je, mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake?, naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe”. Huu ni udhihirisho utofauti wa upendo wa kimungu usio na kipimo na upendo wa kibinadamu ulio na kikomo. Maneno haya hujidhihirisha katika namna mbalimbali. Tunaona jinsi ambavyo mwanadamu ni kigeugeu; yeye ambaye anakuonesha tumaini kubwa leo hii na ahadi kedekede lakini asishindwe kugeuka kesho yake. Wanadamu wanageukana hata wale walio katika damu moja.

Tumaini letu kwa mambo ya kidunia kama halitajajengeka katika misingi ya upendo wa kimungu hutuhadaa. Undugu wa kweli unajengwa na kukamilishwa na Fumbo la Umwilisho ambalo kwalo tunaunganishwa tena na Mungu na kuirudisha hadhi ambayo ilifubaishwa na dhambi. Hapa nataka kufafanua kwamba Kristo hakuwa na maana ya kwamba tusitafute chakula au mavazi, la hasha! Hayo ni mahitaji muhimu ya kibinadamu ila kama hayajajengeka katika tumaini kwa Mungu, kama hayajajengeka katika hamu kama anayokuwa nayo mzaburi anayesema “nafsi yangu yamngoja Mungu peke yake kwa kimya” huwa si lolote. Kwa maneno mengine, mahangaiko yetu ya kila siku yanapaswa kuchagizwa na kutufikisha katika tumaini hilo ambalo kwa hakika halitatuangusha.

Jamii ya mwanadamu ambayo haiangalii thamani ya utu wa mtu inajifunua leo hii katika sura mbalimbali. Jamii hii inaujeruhi na kuusambaratisha kabisa utu wa mwanadamu. Tunaona jinsi ambavyo wanasiasa na watawala mbalimbali wanatengeneza taratibu ambazo hazimwangalii mwanadamu bali katika uchochoro wa ubinafsi zinaangalia maslahi ya mtu mmoja mmoja. Hivyo si shida kupitisha sheria zinazoridhia utoaji wa mimba kwa kisingizio cha haki ya mwanamke na hali mbaya ya kiuchumi, huu kimsingi ni utamaduni wa kifo! Hatujiulizi kwamba pale watu wote watakapotekeleza hilo mwanadamu huyu ataishia wapi kama si kuangamia na kupotea kabisa duniani? Kwa hakika mahangaiko yetu katika kujitafutia ulinzi na usalama huu wa kidunia hutuacha vipandevipande.

Zao la jamii kama hii ni mwanadamu aliyeraruriwa vipandevipande mithili ya nguo chakavu iliyonaswa na mtambo fulani. Baba Mtakatifu Francisko anaonya katika waraka wake wa Kitume: “Furaha ya Injili” juu ya migawanyiko hii. Halifa huyu wa Petro anaiona jamii iliyogawanyika na kudai haki za binadamu fulani hata kama utu au hadhi ya binadamu wengine inasambaratishwa. “Inakuwaje suala la kikokongwe maskini kufa hoehai mtaani si habari ya kutilia uzito wakati suala la kupungua kwa nukta moja tu katika masoko ya hisa linapewa uzito mkubwa?” (EG 53), anahoji Askofu huyu mkuu wa Roma. Jamii inajikinai kuhifadhi haki za binadamu ilihali hakuna haki bali ni haki kwa wale wenye uwezo kiuchumi au kisiasa, watu ambao wanahangaika kila siku kwa ajili ya kutafuta uhakika wa maisha yao ya kesho. Tunapoteza utu na matokeo yake tunashindwa hata kuiona sura Mungu katika binadamu wenzetu. Mazingira haya ni aghalabu kutupatia fursa ya kuliweka tumaini letu kwa Mungu. Tumaini letu linabaki katika madaraka na mali za kidunia ambazo kwa macho hutuhakikishia kesho yetu na kutoa tumaini lenye kulaghai.

Mtume Paulo anawaonya Wakorinto na pia anatuonya sisi katika migawanyiko hii. Yeye anapong’amua kwamba Wakorinto hawaangalii kipawa cha Mungu na nguvu zake bali katika uwezo na majigambo ya kibinadamu hasiti kuwaonya na kuwaonesha njia ya kweli iliyojificha katika kuyaona yote tuyatendayo ni kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu na kwamba tunawezeshwa na Yeye mwenyewe. Yeye anamkumbusha kila mmoja wetu akisema: “mtu na atuhesabu hivi, tu watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri za Mungu”. Mwakilishi anapaswa kubaki mwaminifu katika neno lake yeye anayemtuma. Mmoja anakubali kumwakilsha mtu kwa sababu anamwamini na hana wasiwasi kwamba hatamwangusha. Vinginevyo ni vigumu kukubali uwakilishi huo. Hivyo sisi sote tunapojiweka katika tumaini na kuwa mawakili wa Mungu tutajenga pamoja, kuthaminiana na kuheshimiana. Kwa njia hii tutaepuka majanga ya kibinadamu na kuweka tumaini letu katika kweli.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.